Pages

Pages

Pages

Friday 8 May 2015

WASIRA AJIPIGIA MSTARI URAIS 2015

Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira (kushoto) akizungumza alipokuwa akifanyiwa mahojiano maalumu na waandishi wa gazeti la Mwananchi, ofisini kwake Dar es Salaam.Picha na Emmanuel Herman 
Na Florence Majani, Mwananchi
Dar es Salaam. Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira amesema kama chama chake, CCM, kitampa fursa ya kuwania wadhifa wa urais, atasimama kwenye mstari wa uadilifu na ufanisi ili kulinda heshima ya cheo hicho.
Akizungumza na Mwananchi baada ya kupokea tani 7,492 za mbolea kutoka kwa watu wa Japan jana Dar es Salaam, Wasira alisema pamoja na kwamba CCM bado haijapuliza kipenga cha kuwania nafasi hiyo, lakini kikimteua basi ana uhakika wa kuwashinda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). “Nina nguvu kwenye chama changu...mimi ni mwadilifu, sina makundi yoyote. Nina hakika nitakuwa rais bora,” alisema.
Wasira, ambaye ni Mbunge wa Bunda alisema wadhifa wa urais hauangalii umri, sura au fedha bali uwezo wa kuongoza na uadilifu.
Alisema umri mkubwa siyo kigezo cha kuwa rais bora, kwani hata rais wa sasa wa Nigeria ana miaka 72.  Akifafanua, alisema kama angekuwa na afya dhaifu au kukosa akili timamu, basi hicho kingeweza kuwa kigezo cha kuukosa urais.  “Mimi siyo mbunge dhaifu na simhofii yeyote kisiasa. Nina hakika na usafi wangu kiakili, kimwili na uwezo wa kuongoza,” alisema.
Katika kujiweka kwenye mstari wa kukubalika, mbunge huyo aliukosoa uchambuzi wa mchambuzi Julius Mtatiro katika gazeti hili uliomtaja kama mmoja wa viongozi wenye kauli za  ‘kidikteta’.
Alisema, “Inapotokea nikasema ukweli, basi nisituhumiwe kuwa ni dikteta. Penye ukweli unatajwa ukweli, penye uongo, ukweli huwekwa bayana.
“Mtatiro anadai mimi nimewahi kutoa kauli za vitisho, hilo siyo kweli bali mimi ni msema kweli na huo ndiyo utawala bora.”
Kuhusu jimbo lake kuwaniwa na Mbunge wa Viti Maalumu wa CCM, Esther Bulaya, Wasira alisema, “Sina hofu juu ya mbunge huyo, kwanza siyo saizi yangu. Hata nisipogombea (Esther) hatashinda, namruhusu agombee nina uhakika hawezi kushinda.”
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment