Pages

Pages

Pages

Sunday 24 May 2015

KUMBUKUMBU ZANGU: SIMBA ILIVYOFIKA FAINALI YA KOMBE LA CAF MWAKA 1993


Hiki ndicho kikosi cha Simba kilichofika fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993. Kocha Abdallah Hussein 'Kibadeni' ni wa tatu kushoto waliosimama, anafuatiwa na Often Martin, Razack Yussuf 'Careca', George Lucas 'Gazza', Idd Selemani 'Meya', Damian Morisho Kimti, Abdul Ramadhan 'Machine', George Magere Masatu, Ramadhan Maufi 'Lenny', kocha msaidizi Etenne Eshente kutoka Ethiopia na Meneja wa Timu Abdulrahman Muchacho.
Waliochuchumaa ni Kassongo Athumani, Selemani Pembe, Edward Cyril Chumila, Dua Said, Fikiri Magoso, Malota Soma 'Ball Juggler' na Mohammed Mwameja.

Na Daniel Mbega
Simba ilikuwa inashiriki kwa mara ya kwanza, au niseme Tanzania ilikuwa inawakilishwa kwa mara ya kwanza kwenye michuano hii ya tatu ya kuwania Kombe la CAF lililotolewa na mfanyabiashara wa Nigeria, Chifu Moshood Abiola, ambaye alikuwa katika harakati za kuwania urais wa nchi hiyo kabla haujavurugwa na Jenerali Sani Abacha.
Msimu huo wa 1993 kikosi cha Simba kilichokuwa kinanolewa na Abdallah Hussein 'Kibadeni' aliyesaidiwa na Etenne Eshente kutoka Ethiopia kilikuwa na wachezaji hawa: Mohammed Mwameja, Mackenzie Ramadhani, Often Martin (Ushirika), Deo Mkuki (Pamba), Twaha Hamidu, Selemani Pembe, Fikiri Magosso, George Masatu, Godwin Aswile,  Kassongo Athumani, Ramadhani Lenny, George Lucas, Hussein Marsha, Abuu Omar, Idd Selemani, Joachim Masumbuko, Damian Kimti, Edward Chumila, Nico Kiondo, Malota Soma, Bakari Iddi, Abdul Ramadhani Mashine,  Razak Yusuf 'Careca' (Coastal Union), David Mihambo (Reli), Mbuyi Yondani (Reli), Feruzi Teru (Milambo), Dua Said (Small Simba), Rashid Abdallah Magongo (Breweries - Ndovu), Michael Paul na Thomas Kipese. 
Simba ilianza kampeni zake katika raundi ya kwanza kwa kupambana na Ferroviario de Maputo ya Msumbiji kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza Februari 20, 1993, ambapo timu hizo hazikufungana. Ziliporudiana tena Machi 6 mjini Machava, Msumbiji, timu hizo zilifungana goli 1-1. Hivyo, Simba ikasonga mbele kwa sheria ya goli la ugenini.
Katika raundi ya pili ya michuano hiyo, Simba ilikumbana na Manzini Wanderers ya Swaziland. Mchezo wa kwanza uliofanyika Mei 22, 1993 mjini Dar es Salaam, Simba ilishinda kwa goli 1-0, ambalo lilifungwa na Malota Soma 'Ball Juggler' katika dakika ya 14.
Ziliporudiana Juni 6, 1993 mjini Manzini, Simba tena ilitoa kipigo cha goli 1-0 na kufanikiwa kuingia robo fainali ya michuano hiyo. Timu nyingine zilizoingia robo fainali ni Gor Mahia (Kenya), Insurance (Ethiopia), Al-Harrach (Algeria), Zamunta (Niger), Mbilinga (Gabon), Atletico Sports Aviacao (Angola) na Stella Abidjan (Ivory Coast).
Kwenye robo fainali, Simba ilikumbana na Al-Harrach ya Algeria. Mchezo wao wa kwanza ulifanyika mjini Dares Salaam Septemba 5, 1993 ambapo Simba iliichabanga Al-Harrach kwa magoli 3-0 yaliyofungwa na Edward Chumila (mawili) na Abdul Mashine. Simba iliingia nusu fainali ingawa ilifungwa magoli 2-0 mjini Algiers, Septemba 18, 1993.
Katika nusu fainali , Simba, ambayo tayari ilikuwa imeahidiwa kupewa magari aina ya Isuzu KIA kwa kila mchezaji na kiongozi kutoka kwa mfadhili wao  mkuu, Azim Dewji, endapo wangelitwaa kombe hilo, safari hii iliamua kuonyesha nia ya kuyapata magari hayo. Ilikuwa inapambana na Atletico Sports Aviacao ya Angola, iliyoifunga Gor Mahia ya Kenya kwa jumla ya magoli 4-2 katika robo fainali.
Mchezo wa kwanza baina ya Simba na Atletico ulifanyika mjini Dar es Salaam Oktoba 17, 1993 na Simba ilishinda kwa magoli 3-1. Edward Chumila alifunga bao la kwanza na la tatu, wakati lile la pili Aviacao walijifunga. Bao la Waangola hao lilifungwa na Nello. Ziliporudiana mjini Luanda Oktoba 31, 1993 timu hizo hazikufungana na hivyo Simba ikawa imeingia fainali.
Kwenye hatua ya fainali ndiko kulikokuwa na kazi ngumu. Ilikutana na Stella Abidjan ya Ivory Coast na mchezo wao wa kwanza ulifanyika mjini Abidjan Novemba 14, 1993 na timu hizo zilitoka sare ya 0-0, lakini ziliporudiana mjini Dar es Salaam Novemba 27, 1993 Stella iliifunga Simba magoli 2-0 na kutwaa kombe hilo la CAF. Magoli ya Stella yalifungwa na Kouame Desire (dk.17) na Jean Boli Zozo (dk. 77).
Baada ya mechi hiyo, Simba walitaka kukata rufaa CAF kulalamika kwamba wachezaji wawili wa Stella, N'Guessan Serges na Jean Boli Zozo walikuwa wanachezea klabu ya Paris Saint Germain ya Ufaransa. Mhariri wa michezo wa gazeti la Mfanyakazi, James Nhende na mwandishi wake, Francis Lucas, waliandika katika gazeti toleo la Desemba 8, 1993 kuwa wachezaji hao walikiri wenyewe kuwa walikuwa wanaichezea PSG ambayo ilikuwa inaongoza Ligi Kuu ya Ufaransa.
Hata hivyo, Mtanzania mmoja aliyekuwa akifanya kazi katika Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), Bwana Bishota, aliyekuwa akifanyia kazi mjini Abidjan, aliishauri Simba isikate rufaa dhidi ya mchezaji Boli Zozo, kwani mchezaji huyo wa Stella ni tofauti na Boli Zozo wa timu ya Eistre ya ufaransa iliyokuwa inashiriki Ligi Daraja la Pili nchini humo.
Zaidi ya hayo, klabu hiyo ya Eistre ilikwishaijulisha Simba kwamba mchezaji wao Boli Zozo Laurent alikuwa Ufaransa na alicheza katika mchezo wa ligi siku hiyo ambayo Simba ilikuwa inapambana na Stella.
Gazeti la Dimba toleo la Jumapili ya Desemba 5, 1993 lilikuwa limeandika kuwa mchezaji Boli Zozo wa Eistre ingawa alifanya mazoezi Ijumaa ya Novemba 26, 1993 na timu yake hiyo ya Ufaransa, lakini Jumamosi alikosekana kwenye mechi, hivyo kuleta wasiwasi kuwa huenda alikuja Dar es Salaam kuichezea Stella.
Klabu ya Eistre ilisema kuwa mchezaji wao alifanya mazoezi na timu yake Ijumaa ya Novemba 26, 1993 na pia alikuwa mazoezini Novemba 28, hivyo isingewezekana awe Dar es Salaam Novemba 27, siku ambayo pia alicheza mechi ya ligi.
Kwa ujumla kulikuwa na utata mkubwa wa jina la Boli, kwani walikuwepo akina Boli wengi waliokuwa wakicheza soka ya kulipwa nchini Ufaransa, na wote walikuwa wanatoka Ivory Coast. Baslie Boli ndiye aliyekuwa akijulikana zaidi na alikuwa nyota katika timu kongwe nchini humo ya  Olympique Marseille akifuatiwa na mdogo wake, Roger Boli, ambaye alikuwa anaichezea timu ya Lens nchini humo.

Wakati ambapo yule wa Eistre alikuwa akiitwa Boli Zozo Laurent, huyu wa Stella alikuwa Boli Zozo Jean. Kwa hali hiyo Simba wakabwaga manyanga na kuruhusu tonge kuponyoka mdomoni.

WASILIANA NAMI KUPITIA SIMU/WHATSAPP/TELEGRAM 0656-331 974

No comments:

Post a Comment