Pages

Pages

Pages

Sunday 10 May 2015

KUMBUKUMBU ZANGU: MECHI 6,068 ZA LIGI KUU ZILIZOZAA MABAO 10,838

Kikosi cha Cosmopolitan, mabingwa wa soka Tanzania mwaka 1967. Kushoto anaonekana kocha wa timu hiyo Mansour Magram.

NA DANIEL MBEGA
LIGI Kuu ya soka Tanzania Bara kwa msimu wa 2014/2015 imehitimishwa rasmi Jumamosi Mei 9, 2015 kwa michezo saba iliyotimiza jumla ya mechi 182, huku mabao 15 yakifungwa siku ya mwisho na kufanya jumla ya mabao 346 kwa msimu mzima, ukiwa ni wastani wa mabao 1.9 kwa kila mechi.

Kwa kuangalia katika kumbukumbu za utafiti wangu, hadi kufikia jioni ya Jumamosi Mei 9, 2015, jumla ya mechi 6,068 zilikuwa zimechezwa katika harakati za kusaka ubingwa wa Tanzania tangu Ligi ya Taifa ilipoanza mwaka 1965.
Mechi hizo zilizaa jumla ya mabao 10,838, huku mabao mengine yakiwa yamepatikana kwa njia ya matuta, hasa katika kipindi cha 1965 hadi 1976 ambapo Ligi ya Taifa ilikuwa inaendeshwa kwa mtindo wa mtoano.
Mfumo halisi wa Ligi yenye kutoa pointi kwa kila mechi ulianza mwaka 1977 na ulianzishwa na mkimbiaji wa zamani wa Tanzania, ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka nchini (FAT), Chabanga Hassan Dyamwale, ambapo mshindi alikuwa akipata pointi mbili wakati timu zilipotoka sare ziligawana pointi moja moja.
Mfumo huo wa kutoa pointi mbili kwa mshindi ulibadilika mwaka 1994/95 ambapo sasa timu zilizoshinda zikaanza kupewa pointi tatu. Hii ilitokana na mabadiliko ya Sheria za Soka za Kimataifa ikiwa ni katika kuzipa hamasa timu zifanye vizuri zaidi uwanjani kwa ushindani.
Huwezi kuamini nikisema kwamba, mpaka sasa hakuna hata timu moja ambayo imewahi kuwepo kwenye Ligi miaka yote tangu mashindano hayo ya kusaka bingwa yalipoanzishwa. Hakuna hata moja.
Miamba ya soka Tanzania, Simba na Yanga, ingawa ndiyo iliyocheza mechi zaidi, haijapata kushiriki mashindano hayo katika nyakati fulani hasa kwenye miaka ya 1960 na mwanzoni mwa miaka ya 1970.
Kwa mfano; mwaka 1967 Simba (Sunderland wakati huo) na Yanga zilijitoa kwenye Ligi kwa sababu mbalimbali. Mwaka 1970 na 1971 Simba haikufuzu kwa hatua ya mwisho ya Ligi hiyo baada ya kushindwa kwenye Ligi ya Mkoa wa Pwani. Ikumbukwe kwamba, wakati huo kuliendeshwa mashindano ya mikoa na mabingwa wa mikoa hiyo ndio waliofuzu kwa ngazi ya Taifa.
Hata mwaka 1975 wakati Mseto ilipotwaa ubingwa, ikiwa klabu ya kwanza kupeleka taji hilo nje ya Dar es Salaam, Simba haikuwemo baada ya kushindwa kufurukuta kwenye Ligi ya Mkoa wa Pwani. Lakini pamoja na Yanga kushiriki, haikuweza kutetea ubingwa wake baada ya kushuhudia fainali ikizikutanisha timu zote za mikoani, Mseto ya Morogoro na Nyota Mtwara.

Dondoo:
- Bao la kwanza kabisa la Ligi ya Taifa lilifungwa Juni 5, 1965 katika mechi ambayo Manchester United ya Tanga iliifunga Sunderland pia ya Tanga 1-0.
- Mchezaji Martin wa Coop United ndiye wa kwanza kufunga mabao matatu ‘hat trick’ kwenye Ligi. Alifunga mabao matatu katika ushindi wa timu yake wa mabao 5-1 dhidi ya African Sports Desemba Mosi, 1967.
- Kitwana Ramadhan Manara ‘Popat’ ndiye mchezaji wa kwanza kubadilisha namba na kung’ara zaidi uwanjani. Alikuwa kipa wa Cosmopolitan na Taifa Stars hadi mwaka 1965 alipoamua kuhamia kwenye ushambuliaji na kuwa mwiba kwa ngome za wapinzani.
- Mseto iliwahi kutoa kipigo cha mbwa mwizi kwa mahasimu wao Nyota Afrika ya Mtwara baada ya kuifunga mabao 15-2 kwenye mechi ya Ligi ya Taifa ngazi ya Kanda. Hii ilikuwa Mei 22, 1977 ambapo mabao ya Mseto yalifungwa na Edward Hiza, Hassan Shilingi (mawili), Juma Mensah, Haji (manne), Ahmad Omar, Kassam (manne), na Vincent Mkude (mawili). Mabao ya Nyota Afrika yalifungwa na Mkenda na Joseph.
- Kwa mara ya kwanza masuala ya soka kwenda mahakamani ilikuwa mwaka 1982 wakati Simba ilipoweka pingamizi kuzuia mechi za Ligi ya Taifa zisiendelee mpaka rufani yake kuhusu usajili ijadiliwe. Mechi zilisimama, lakini baadaye zikaendelea baada ya Simba ‘kupigiwa magoti’ na kufuta pingamizi hilo.
- Yanga iliwahi kutumia dakika 88 kukomboa bao bila mafanikio. Hii ilikuwa Mei 26, 1990 wakati bao la Mavumbi Omar la meta 40 katika dakika ya pili lilipoweza kuipa ushindi Simba.
- Neno ‘Uteja’ lilianza kutumiwa zaidi kwenye soka mwaka 1990 na mashabiki wa klabu za Coastal Union na African Sports za Tanga wakimaanisha Simba na Yanga walikuwa wateja wao kwa sababu timu hizo kila zilipotia pua Mkwakwani zilipata kipigo.
- LĂ©opold ‘Tussle’ Mukebezi na Mecky Maxime ndio wachezaji pekee walioweza kudumu katika klabu moja maisha yao yote ya soka. Mukebezi alichezea Balimi ya Bukoba miaka ya 1970 hadi mwanzoni mwa 1980, wakati Maxime aliichezea Mtibwa Sugar hadi alipostaafu 2010.
Fuatilia www.brotherdanny.com kila siku kwa dondoo mbalimbali za michezo
-------------------------------

No comments:

Post a Comment