Pages

Pages

Pages

Monday 25 May 2015

CCM IKIMTEMA LOWASSA URAIS, INANG’OKA IKULU!


Lowassa wakati akiwa Waziri Mkuu.
Picha mbalimbali zinazomuonyesha Lowassa akiongea na makundi mbalimbali ya wafuasi.

Na Daniel Mbega
“MKAKATI wasukwa kuwaondoa Lowassa na Membe urais 2015”, “CCM yamtolea uvivu Lowassa urais 2015”, “Mkakati wa kumfukuza Lowassa CCM waiva”, “CCM yamuonya tena Lowassa”, “CCM haitaruhusu wanunua urais 2015”.
Naam. Hivi ni baadhi tu ya vichwa vya habari ambavyo kwa miaka takriban mitano sasa vimekuwa vikipamba magazeti na mitandao ya kijamii kuhusu harakati za muda mrefu za Chama cha Mapinduzi (CCM) ‘kumzuia’ Mbunge wa Monduli na waziri mkuu mstaafu, Edward Ngoyayi Lowassa, asiwanie urais mwaka 2015 kupitia chama hicho.


Na katika kipindi hiki ambapo kasi ya kujipanga kwa kuwania kuteuliwa imepamba moto, siyo ajabu kuona maandiko mengi yakimponda kada huyo wa CCM na kumkatisha tamaa kabisa asitie mguu kwenye kinyang’anyiro hicho.
Yawezekana CCM – au baadhi ya watu ndani ya CCM – wana sababu zao za kumwekea kauzibe Lowassa, lakini binafsi naamini kuna mkorogano ndani ya chama hicho, mkorogano ambao hauna tofauti na mwaka 1995 na hata 2005.
Tungekuwa kwenye michezo, tungesema ‘Kombe liko wazi’, lakini kwa sasa tunasema kiti cha urais kitakuwa wazi baada ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza muda wake Oktoba 2015.
Waliozuiwa na mkwara wa kifo wa Sheikh Yahya Hussein mwaka 2010, sasa wamenyoosha makucha yao, lakini wanafanya kila namna kuwazibia wengine na zaidi inaonekana vita ya vigogo wa CCM wengi imehamia kwa Lowassa.
Mwenzenu mpaka nashangaa. Kwani Lowassa ametenda dhambi gani kubwa kiasi cha CCM kumchukia? Hivi ana damu ya kunguni au nyota ya Punda?
Yeye mwenyewe amekaririwa akisema: “Natazamwa na CCM kila kona!” Yaani kila anachokifanya, CCM lazima waseme, wamwekee vikwazo, wazushe kashfa na mambo mengine kadha wa kadha.
Lowassa ana fedha za kutosha. Hilo halina ubishi. Lakini fedha hizi zisiwe chanzo cha kuleta chokochoko na vikwazo kwake kugombea.
Maswali ya namna gani alivyozipata – kwa kisingizio cha hoja ya Mwalimu Julius Nyerere – kwa sasa hayana msingi sana hasa inapotokea kwamba hakuna mtu yeyote mwenye ushahidi wa tuhuma za ufisadi dhidi yake.
Wapo baadhi ya watu wanaotaka kuuaminisha umma wa Watanzania kwamba Lowassa ni fisadi wa kutupa, kwamba anatumia fedha kununua ‘upendo’ kwa wananchi wa kada zote na mambo kadha wa kadha.
Mbona hawawawekei vikwazo wale waliotajwa kwenye orodha ya ukwapuaji wa fedha za Akaunti ya EPA na hata Escrow? Wanawaogopa?
Kuna mambo mawili kwa Lowassa. Anakubalika kwa sababu alijijengea msingi muda mrefu na mikakati yake ni ile yenye kuzaa matunda. Halafu pili, amekuwa karibu na wananchi na ndiyo maana makundi yote ya kijamii yanamuunga mkono kiasi kwamba amekuwa kimbunga ndani ya CCM.
Haikunishangaza wakati yeye mwenyewe alipotamka kwamba ‘Huwezi kuzuia mafuriko kwa mikono’. Ndiyo. Huwezi kuzuia nguvu ya umma kwa sababu hivi sasa kila kona unayopita habari ya mjini ni Lowassa kuwa rais!
Vyombo vya habari vyenyewe vimeandika sana kuhusu kukubalika kwa Lowassa na wananchi, hata kama ndani ya CCM hawamtaki.
Miongoni mwa vichwa vya habari ni hivi: “Lowassa atikisa urais 2015”, “Kumbe Lowassa ni tishio CCM”, “Lowassa aongoza urais”, “Lowassa amtesa Kikwete”, “CCM hoi kwa Lowassa... sasa Lowassa ana nguvu kuliko chama”, “Moto wa Lowassa sasa waitikisa CCM” na vingine kadha wa kadha.
Binafsi naamini kitu kimoja ambacho kiko dhahiri kwa wanaompinga Lowassa: wanaogopa kuumbuliwa kutokana na madudu wanayoyafanya.
Viongozi wengi wa serikali ni wazembe, na uzembe ni adui namba moja wa Lowassa, kama ilivyokuwa kwa Mbunge wa zamani wa Monduli, wajina wake Edward Moringe Sokoine.
Nchi hii kwa mahali tulipofikia, tunahitaji tupate kiongozi dikteta kidogo na mwanadiplomasia kidogo – sifa alizonazo Lowassa.
Tunataka kiongozi ambaye atakuwa na uamuzi mgumu, asiyelea uozo na anayeweza kuweka vipaumbele na kuvisimamia.
Jenerali Idi Amini Dada alikuwa dikteta, wengi tunamchukia kwa matendo yake yasiyo ya kibinadamu, lakini mimi nampenda kwa kitu kimoja tu: alikuwa halei uozo. Alipata kusema: “Wewe ni waziri, una mamlaka, ofisa wako wa chini anavurunda halafu unasubiri mpaka Jenerali Amini aje amwajibishe. Basi hufai hata kushika nafasi hiyo!”
Naam. Lowassa anaweza kuondoa ombwe hili la uzembe na kuwanyorosha wale wanaodhani ni miungu-watu hata pale wanaposhindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo. Anaweza, si tumeona katika kipindi alichokaa kwenye uwaziri mkuu?!
Tupo kwenye umaskini mkubwa, watu wanateseka bila sababu ya msingi. Vijana wanashabikia tu kama wehu, wengine ni wasomi lakini wanapelekwa kama upepo, wakisikia hiki "hewala", wakisikia kile "sawa", wakiambiwa hivi "alhamdulilah", wakiambiwa kile "poa tu". Hawataki kuchambua na kuielewa siasa kwamba kwenye siasa kuna majungu, fitna, kuchongeana, uchu wa madaraka na mali na mambo mengi.
Sina haja ya kuyataja aliyoyafanya Lowassa katika kipindi chake cha miaka miwili na mwezi mmoja na siku nane alichokaa pale Magogoni, lakini kwa kifupi tu ni kwamba, yeye si mtu wa kupoteza mwelekeo na anasimamia kile anachokiamini. Halafu siyo kigeugeu na siyo mvivu.
CCM inayafahamu yote haya na imekuwa ikifanya kila jitihada kuhakikisha inakwamisha harakati zake. Watu wameibuka na sababu kadha wa kadha kama Lowassa ni fisadi; ana utajiri mkubwa, sijui alikataliwa na Mwalimu Nyerere na kadhalika. Msimsingizie Mwalimu Nyerere kuhalalisha fitna zenu bwana.
Sasa wameibuka na hoja nyingine ambayo kwayo naona ni ya unyanyapaa mkubwa. Eti Lowassa ni mgonjwa na hivyo hastahili kuchaguliwa.
Hapa ndugu zangu mnamkosea Mungu. Hivi mmesahau ule wimbo wa Selemani Kungubaya wa Salamu za Wagonjwa? Anaimba hivi: “Ajuaye Bwana Mungu kwa mzima kuwa mfu, mgonjwa kuwa salama…”
Naamini uzima wa mtu anayeujua ni Mungu. Leo hii mnaomsema kwamba anaumwa, kesho mnaweza kutangulia mbele za haki mkamwacha anadunda na afya njema kabisa.
Kwa hakika, CCM msifanye makosa kwa chuki zenu kumtema Lowassa katika kinyang’anyiro hiki. Mwacheni apite kwenye vikao vyote na wanachama waamue wenyewe.
Wanafunzi, viongozi wa dini na makundi mbalimbali yanayojitokeza kumuunga mkono hayajakosea.
Mkifanya makosa ya kumtema, hakika mtawafuata ZAPU na wengineo.
Kazi yangu kusema, ni haki yangu ya Kikatiba.
Wasalaam.

0656-331974
Makala hii ni kwa hisani ya gazeti la WAJIBIKA la Mei 25, 2015

No comments:

Post a Comment