Pages

Pages

Pages

Saturday 4 April 2015

WENYE ULEMAVU WAILILIA SERIKALI


Na Hastin Liumba, Tabora
WAJUMBE wa Baraza la Watoto wenye ulemavu mkoani Tabora wamepaza sauti zao na kuiomba serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto kuwatengea bajeti ya kutosha itakayosaidia kuwezesha vituo, shule na vyuo  ili kujikwamua.


Kilio hicho kimetolewa katika semina ya Wajumbe wa Baraza la Watoto wenye ulemavu iliyofanyika mjini hapa na kuhudhuriwa na watoto wenye ulemavu wanaosoma katika shule mbalimbali zilizoko katika halmashauri zote za mkoa huu.

 Akizungumza katika semina hiyo Mwenyekiti wa watoto hao Glory John ambaye ni mlemavu wa macho alisema watoto walio wengi wenye ulemavu hapa nchini wameshindwa kuendelea au kuendelezwa kutokana na serikali kutoweka kipaumbelea cha kuwezesha kundi hilo katika bajeti yake ya wizara.

Alisema watoto wenye ulemavu ni kama watoto wengine na baadhi yao wana uwezo mkubwa kiakili kuliko hata watoto wasio na ulemavu, lakini wengi wa watoto hao wametelekezwa majumbani na wengine wamefichwa ndani na wazazi au walezi wao.

Mbaya zaidi hata zile shule zinazopokea watoto wenye ulemavu bado zinakabiliwa na changamoto nyingi sana ikiwemo suala la waalimu, watumishi wasio waalimu, miundombinu isiyo rafiki, vyumba vya madarasa, vifaa vya kufundishia na bajeti finyu.

Alisema katika takwimu za watoto wote wenye ulemavu katika mikoa mbalimbali hapa nchini ni asilimia 2 ya watoto hao wanaopelekwa katika shule hizo, lakini ukiangalia huko mitaani wapo watoto wengi wenye ulemavu ila wananyimwa fursa hiyo ya kupata elimu.

‘Sisi walemavu tuna mkosi gani, kwani tulitaka tuwe hivi tulivyo, kwa nini tutelekezwe na jamii, kwa nini tunyimwe haki ya kupata elimu kama watoto wengine, kwa nini tufichwe ndani, jamani tunaiomba jamii na serikali kwa ujumla ituhurumie, itujali, itusomeshe, isitufiche ndani.” alieleza Grace.

Naye mweka hazina wa Baraza hilo Mpanzi Nicholous ambaye ana uoni hafifu alisema serikali imesahau kabisa uwepo wa watoto wenye ulemavu ndio maana wizara husika na halmashauri zote hazioni umuhimu wa kutenga bajeti.

 Aidha alishauri serikali kuliangalia upya suala hilo na kuweka kipaumbele cha kumwinua mtoto mlemavu sambamba na kuongeza shule na vyuo vinavyotoa elimu kwa watoto wote wenye ulemavu ili angalau kila wilaya au mkoa kuwe na shule maalumu kwa watoto hao.

Aidha wajumbe wengine katika baraza hilo Mwajuma Said, Abas Amur na Said Shabani walieleza huduma za afya kwa watoto walio wengi wenye ulemavu ni mbaya sana wakati wenzao wanapata huduma hizo bila tatizo huku wakiiomba serikali izifanyie kazi changamoto zote.

No comments:

Post a Comment