Pages

Pages

Pages

Saturday 4 April 2015

NENDA YANGA, NENDA AFRIKA

Washambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe (mbele) na Simon Msuva wakishangilia kwa pamoja bao la tatu la timu hiyo lililofungwa na Tambwe katika mechi ya kwanza dhidi ya Platinum jijini Dar es Salaam ambapo Yanga ilishinda 5-1.

...TAZAMA, UMEBAKI WEWE, WEWE TU KUTULETEA RAHA

Na Daniel Mbega
WAWAKILISHI pekee wa Tanzania michuano ya klabu barani Afrika, Yanga, wako mjini Zvishavane huko Zimbabwe kutafuta sare ama ushindi dhidi ya timu ya Platinum ya huko ili kufukuzu kwa robo fainali ya Kombe la Shirikisho.

Yanga wataingia uwanjani leo hii wakijivunia ushindi wao wa mabao 5-1 walioupata jijini Dar es Salaam Machi 21 na safari ya basi ya kilometa 385.4 kutoka Harare hadi Zvishavane inaonekana haitawazuia kufika hatua hiyo ya juu baada ya miaka mingi.
Ule mzimu wa kujisahau kwa sababu wana faida ya mabao mengi uliojitokeza katika mechi ya raundi ya kwanza dhidi ya maafande wa Botswana Defence Force unaweza usijirudie kwani makocha wa timu hiyo, Hans van Der Pluijm na Charles Boniface Mkwasa, wamewajengea saikolojia nzuri wachezaji wao ambao sasa watatafuta ushindi kwa bidii zote.
Katika hatua iliyopita, Yanga walishinda 2-0 nyumbani dhidi ya BDF, na walipokwenda Gaborone hata baada ya kpata bao la kuongoza, wakajisahau na kujikuta wakifungwa mabao 2-1, hivyo kuchafua rekodi yao.
Mkwasa anasema kikosi chake kiko tayari kucheza kwenye uwanja wowote na Platinum ambayo iliing'oa Sofapaka ya Kenya kwa jumla ya mabao 4-2 katika mzunguko wa kwanza.
“Tunajifua kwenda kupambana na kushinda, hatufikirii matokeo ya sare wala kufungwa, tumewaambia wachezaji wakapambane kutafuta mabao mengi zaidi nchini Zimbabwe kama tulivyofanya hapa katika mechi ya kwanza,” alisema Mkwasa.
Yanga ndiyo timu pekee yenye dhamana ya kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya kimataifa baada ya timu nyingi zote kufungashiwa virago kwenye mzunguko wa kwanza.
Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Azam ilitolewa na El Merreikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 3-2 na wanamaji wa Zanzibar, KMKM, wakatolewa na timu nyingine kutoka huko huko Sudan kwa jumla ya mabao 2-1.
Polisi Zanzibar ilitolewa kwenye Kombe la Shirikisho baada ya kfungwa jumla ya mabao 8-1 na CF Mounana ya Gabon.
Haijawahi kutwaa ubingwa wa Afrika, Kombe la Washindi wala hili la Shirikisho, lakini Yanga ina uzoefu mkubwa wa mechi za kimataifa ikiwa imeanza kushiriki tangu mwaka 1969.
Itakumbukwa kwamba, mwaka huo 1969 iliposhiriki kwa mara ya kwanza Klabu Bingwa Afrika, ilianza kwa kuitoa Fitarikandro ya Madagascar kwa jumla ya mabao 4-3 katika hatua ya awali na katika raundi ya kwanza ikainyuka Saint George ya Ethiopia kwa jumla ya mabao 5-0.
Ni mwaka huo ambao klabu ya TP Englebert ya Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo) ilibadili jina na kuitwa TP Mazembe.
Baada ya kuvuka hatua hiyo, Yanga ikijivunia wachezaji kama kipa Elias Michael 'Spring', Omar Kapera, Awadh Gessani, Mohammed Hussein Hassan 'Msomali', Hassan Gobos, Maulid Dilunga, Omar Zimbwe, nahodha Abdulrahman Juma na wengineo, ikatinga robo fanaili na kukutana na timu ngumu ya Afrika, Asante Kotoko ya Ghana, iliyokuwa ikitamba na kipa wake mrefu Emmanuel Okalla.
Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Kumasi, timu hizo zilifunga bao 1-1, matokeo ambayo yalipatikana pia jijini Dar es Salaam, na kwa ajabu ya wengi, Yanga ikatolewa kwa shilingi!
Mwaka 1970 tena katika mashindano hayo, Yanga ilianza na US Fonctionnaires ya Madagascar kwenye raundi ya kwanza na kuitoa kwa jumla ya mabao 6-4, na ilipotinga raundi ya pili ikaitoa Nakuru All Stars ya Kenya kwa jumla ya mabao 3-2, hivyo kutinga robo fainali kwa mara ya pili ambako ilikutana tena na Asante Kotoko ya Ghana.
Matokeo ya mchezo wa kwanza mjini Kumasi yalikuwa 1-1, ziliporudiana mjini Dar es Salaam zikafunga tena 1-1, hivyo CAF ikaamuru mchezo huo upigwe katika uwanja huru, ambapo walikwenda kuchezea Addis Ababa, Ethiopia na Kotoko wakashinda kwa mabao 2-0.
Mwaka 1971 Yanga iliitoa Lavori Publici ya Somalia kwa mabao 2-0, lakini ikajitoa raundi ya pili baada ya kupangwa kukutana na Coffee FC ya Uganda kutokana na uhusiano wa kisiasa baina ya Tanzania na Uganda kuwa mbaya hasa baada ya Jenerali Idi Amin Dada kuipindua serikali ya Milton Obote.
Mwaka 1972 Yanga ikarudia raundi ya kwanza ya Klabu Bingwa baada ya kutolewa na AS Saint Michael ya Madagascar kwa jumla ya mabao 2-1 na mwaka 1973 ikatolewa katika hatua hiyo hiyo na El Merreikh ya Sudan kwa umla ya mabao 3-2.
Katika michuano ya mwaka 1975, Yanga ilipita moja kwa moja na kuingia raundi ya pili ambako ilikutana na Enugu Rangers ya Nigeria. Matokeo katika mchezo wa kwanza huko Nigeria yalikuwa suluhu, lakini ziliporudiana jijini Dar es Salaam zikafungana bao 1-1, hivyo Enugu ikafuzu kwa sheria ya bao la ugenini. Ndio mwaka huo ambao Kombe la Washindi lilianza kushindaniwa.
Katika mashindano ya mwaka 1982, Yanga ilianza raundi ya awali kwa kucheza na Tetil Pungue ya Msumbiji, ambapo iliitoa kwa jumla ya mabao 4-1, lakini katka raundi ya pili ikatolewa na Al Ahly ya Misri kwa jumla ya mabao 6-1. Mwaka huo Al Ahly ilitwaa ubingwa kwa kuifunga Asante Kotoko mabao 4-1.
Mashindano ya mwaka 1984 ndiyo yaliyoleta utata zaidi. Kwanza ilitolewa na Gor Mahia kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya sare ya bao 1-1 nyumbani na kukubali kipigo cha bao 1-0 huko Nairobi.
Kwenye mchezo ule wa Dar es Salaam inaelezwa kwamba maofisa wa klabu hiyo walipanga kuwahonga waamuzi kutoka Ethiopia ili 'waibebe', wakagoma na habari zikafika CAF, ambapo maofisa wawili walifungiwa maisha kujihusisha na kandanda.
Mashindano ya mwaka 1988 Al Ahly ya Misri kwamara nyingi ilikatisha safari ya Yanga kwa kuifunga jumla ya mabao 4-0 katika raundi ya kwanza, lakini mzimu wa timu za Misri kwa Yanga ukajirudia tena mwaka 1992 baada ya kutolewa na Ismaili kwa jumla ya mabao 3-1 ingawa Yanga ilikuwa imefuzu hatua ya awali kwa ushindi wa mabao 7-2 dhidi ya Saint Louis ya Shelisheli.
Katika Kombe la CAF mwaka 1994, Yanga ilishindwa kufurukuta baada ya kutolewa na Moroka Swallows ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 2-1,
Hii siyo mara ya kwanza kwa Yanga kupambana na timu za Zimbabwe, kwani mwaka 1995 katika Kombe la Washindi vijana hao wa Jangwani waliondolewa kwenye robo fainali na Blackpool kwa jumla ya mabao 4-2. Katika raundi ya kwanza, Yanga ilicheza na Vaal Reef Professionals ya Afrika Kusini na kuitoa kwa mabao 4-3, mechi ambazo ndizo zilizowapa ulaji Bakari Malima 'Jembe Ulaya' na Shaaban Nonda 'Papii' na kutua 'Bondeni'.
Kwenye raundi ya pili Yanga ikaitoa Tamil Cadets Club ya Mauritius kwa mabao 4-2.
Mwaka 1996 APR ndiyo iliyofupisha safari ya Yanga katika hatua ya awali tu kwa kuifunga jumla ya mabao 4-0, na mwaka 1997 safari ya vijana hao wa Jangwani ikaishia Uganda kwa Express FC ambayo mwaka huo ilibadili jina na kujiita Express Red Eagles. Yanga ilifungwa bao 1-0 ugenini licha ya suluhu ya nyumbani.
Mwaka 1998 ndio angalau Yanga ilifanya maajabu kwa kucheza hatua ya Ligi Ndogo. Ilianza kwa kuitoa Rayon Sport ya Rwanda kwa faida ya bao la ugenini baada ya kutoka 2-2 Kigali na kulazimishwa sare ya 1-1 dar es Salaam; kwenye raundi ikakumbana na Coffee FC ya Ethiopia na kuishindilia jumla ya mabao 8-3.
Katika hatua ya robo fainali (makundi) ikavurunda mno na kuishia kuburuza mkia baada ya kufungwa mechi nne na kuambulia sare mbili tu.
Kwara United ikafaidika na mgogoro ndani ya Yanga 1999 baada ya kuiondoa kwa jumla ya mabao 4-0 kwenye Kombe la CAF, ambapo Yanga ilikubali kuchapwa mabao 3-0 nyumbani katika mchezo wa Machi 28, ambao inadaiwa kwamba kulikuwa na hujuma.
Kwenye Kombe la Washindi 2000, Zamalek ya Misri ikaitoa Yanga kwa jumla ya mabao 5-1.
Mwaka 2001 kwenye Ligi ya Mabingwa Yanga ilianza kwa kuitoa Highlanders ya Zimbabwe baada ya mchezo wa marudiano kuvunjika. Awali timu hizo zilitoka sare ya 2-2 jijini Dar es Salaam.
Katika raundi ya pili, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ikaifunga Yanga jumla ya mabao 6-5.
Mwaka 2006 kwenye Ligi ya Mabingwa, Yanga ilitolewa na Zanaco ya Zambia kwa jumla ya mabao 3-2, lakini mwaka 2007 ilirudia kidogo kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwakama si kutolewa na Esperance ya Tunisia kwa jumla ya mabao 3-0. Ilianza kwa kuifunga AJSM ya Mutsamudu Comoro mabao 5-1 katika mchezo ambao haukuwa na marudiano, kwenye raundi ya pili ikaitoa Petro Atletico ya Angola kwa jumla ya mabao 3-2.
Baada ya kutolewa na Esperance, ilibidi icheze hatua ya Intermediate dhidi ya timu zilizotolewa kwenye Kombe la Shirikisho ili ifuzu robo fainali ya kombe hilo, lakini ikachapwa na El Merreikh ya Sudan mabao 2-0.
Kwenye Kombe la Shirikisho mwaka 2008, Yanga ilianza kwa kuitoa AS Adema ya Madagascar kwa mabao 2-1, lakini ikaondolewa na Al Akhdar ya Libya kwa mabao 2-1 pia.
Mwaka 2009 Yanga ikashiriki Ligi ya Mabingwa ambapo ilivuka raundi ya kwanza kwa ulaini baadaya kuichabanga Etoile d'Or (Mirontsy) ya Comoro kwa jumla ya mabao 14-1 (ikishinda 8-1 nyumbani na 6-0 ugenini), lakini Al Ahly ya Misri ikawa mwiba kwake baada ya kuifunga jumla ya mabao 4-0 kwenye raundi ya pili.
Mwaka 2000 Yanga iliyaaga mapema mashindano ya Ligi ya Mabingwa baada ya kutolewa na FC Saint-Eloi Lupopo ya Congo Kinshasa kwa jumla ya mabao 4-2.
Katika mashindano ya Kombe la Shirikisho mwaka 2011, Yanga ikatolewa mapema na Dedebit ya Ethiopia kwa kufungwa jumla ya mabao 6-4.
Mwaka 2012 katika Ligi ya Mabingwa, yanga ilitolewa na Zamalek ya Misri katika raundi ya awali kwa jumla ya mabao 2-1.
Mwaka 2014, licha ya kupata ushindi mnono wa jumla ya mabao 12-2 dhidi ya Komorozine ya Comoro kwenye raundi ya awali, safari yake ikarudia Cairo kwa Al Ahly baada ya kutolewa kwa mikwaju ya penalti kufuatia matkeo ya jumla kuwa sare ya 1-1 (Yanga ilishinda 1-0 nyumbani, ikafungwa 1-0 ugenini).
Wengi wanajiuliza, mwaka huu wakongwe hao watavuna nini?


0656-331974
IMECHAPWA MARA YA KWANZA NA GAZETI LA SUPASPOTI

No comments:

Post a Comment