Pages

Pages

Pages

Thursday 16 April 2015

MUHIMBILI KUZIBUA MISHIPA YA MOYO KWA DAKIKA 45

Mshauri mwelekezi wa magonjwa ya moyo kutoka Marekani, Profesa Peter Obrien (kulia) akiongoza timu ya madaktari wa upasuaji wa moyo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam kumfanyia mgonjwa uchunguzi na kuzibua mishipa ya moyo, hospitalini hapo jana. Picha na Anthony Siame. 
Na Florence Majani, Mwananchi
Dar es Salaam. Huenda Watanzania wanaougua magonjwa ya moyo wakaepuka kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya matibabu baada ya tiba ya kuzibua mishipa ya moyo iliyoziba kufanyika kwa mara ya kwanza nchini.
Asilimia kubwa ya Watanzania wamepoteza maisha kutokana na magonjwa ya moyo yanayosababishwa na mtindo wa maisha ikiwamo mshtuko wa moyo na kuharibika kwa valvu za moyo.
Akizungumza wakati timu ya madaktari ikiendelea na tiba hiyo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jana,  Mkuu wa Idara ya  Tiba na Upasuaji wa Moyo, Profesa Mohamed Janabi alisema  hayo ni mapinduzi makubwa na yenye tija katika sekta ya afya.
“Tanzania imeandika historia ya pekee na huenda kasi ya kupeleka wagonjwa nje ya nchi ikapungua kwa kiasi kikubwa kwa sababu wale wote wenye matatizo haya watapatiwa tiba hapa hapa,” alisema.
Idara ya Tiba na Upasuaji itashirikiana na  wataalamu kutoka Marekani na India kuhakikisha wanafanya uchunguzi, kutoa tiba kwa wagonjwa wa moyo na kufundisha madaktari wa nchini.
Akielezea jinsi matibabu yanavyofanyika, Profesa Janabi ambaye pia ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya Moyo alisema, tiba hiyo inatumia kifaa maalumu kiitwacho ‘stent’ ambacho huingizwa hadi kwenye moyo na kuzibua mishipa ya damu iliyoziba.
Alieleza kuwa, mtambo maalumu uitwao ‘Cath Lab’ huingizwa mwilini mwa mgonjwa na kusaidia kuona iwapo kuna tatizo la moyo kabla ya kuweka kifaa hicho cha kuzibua mishipa ya kusambaza damu kwenye moyo.
 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hussein Kidanto alisema, ujio wa tiba hiyo una manufaa makubwa kwani Watanzania.
Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo kutoka Kituo cha Afya cha Virginia, Marekani, Peter O’Brien alisema, fursa ya kuwafunda madaktari wa Kitanzania ni ya muhimu kwake kwani inampa ujuzi zaidi hata kujifunza jinsi nchi nyingine zinavyotoa tiba ya moyo.
 “Watanzania hawana budi kuacha tabia hatarishi zinazosababisha magonjwa haya kama vile, kuvuta sigara, kula vyakula vya kusindikwa na vyenye mafuta mengi, pia wafanye mazoezi,” alisema.
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment