Pages

Pages

Pages

Sunday 19 April 2015

BODABODA ZAUA WATU 220 SIKU 90



Na Kizitto Noya
Wakati wimbi la ajali likiendelea kutikisa nchi, watu 220 wamefariki dunia kwa ajali za bodaboda nchini kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu, Kamanda wa Usalama barabarani, Mohamed Mpinga amesema.
Kamanda Mpinga alisema hayo jana mjini Kibaha alipokuwa akifunga mafunzo kwa ajili ya madereva 1,000 wa bodaboda mkoani Pwani, yaliyofadhiliwa na Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Moto (AAT) kwa kushirikiana na asasi ya Fia ya nchini Uingereza.
Kwa mujibu wa kamanda Mpinga, vifo hivyo vimetokana na ajali 668 zilizotokea nchi nzima katika kipindi hicho cha miezi mitatu na ambazo zimesababisha majeruhi 618.
“Takwimu zinaonyesha kuwa mafunzo hayo ya madereva wa bodaboda, yamefanikisha kupunguza idadi ya ajali kutoka 1,449 zilizotokea kati ya Januari na Machi mwaka 2014, hadi ajali 668 kati ya Januari na Machi mwaka huu 2015,” alisema Kamanda Mpinga.
Katika kipindi hicho pia kumekuwa na punguzo katika idadi ya majeruhi wanaotokana na ajali za bodaboda kutoka majeruhi 1,304 mwaka jana 2014 hadi majeruhi 618 mwaka huu.”
Sababu ya vifo
Kamanda Mpinga alibainisha kuwa pamoja na idadi ya ajali na majeruhi kupungua, vifo vimeongezeka na hili limetokana na madereva wa bodaboda kutofuata sheria, kanuni na taratibu.
“Ukiangalia vifo vingi vilitokana na madereva kutofuata sheria, kanuni na taratibu na hasa kutovaa kofia ngumu. Sasa unaweza kuona kuwa bado tuna kazi nzito ya kuhakikisha vifo navyo vinapungua.
Kamanda Mpinga aliwataka madereva waliomaliza mafunzo ya awamu hiyo ya tano, kutumia vema elimu waliopata ili kushiriki katika jitihada za Serikali na wadau wengine kukomesha tatizo la ajali za barabarani.
Awali akimkaribisha kamanda Mpinga, Rais wa AAT Nizar Jivani alisema mafunzo ya madereva hao 1,000 wa Mkoa wa Pwani, ni mwendelezo wa mafunzo ya muda mrefu yaliyoanzia katika mkoa wa Dar es Salaam, ambako madereva 4,000 walihitimu.
Aliwataka madereva hao kuwa mabalozi katika vita dhidi ya ajali za barabarani ili kufikia lengo la kampuni hiyo kupunguza ajali kwa asilimia 50.
Mwakilishi wa Fia , Monalisa Adhikari, alisema taasisi hiyo ya Uingereza, itaendelea kutoa ufadhili wa mafunzo hayo kadiri mahitaji yanavyoongezeka.

“Fia inatilia maanani sana mafunzo hayo na itaendelea kutoa ufadhili kadiri mahitaji yanayoongezeka,” alisema.
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment