Pages

Pages

Pages

Tuesday 24 March 2015

SIKIKA: SERIKALI INAPASWA KUMALIZA TATIZO SUGU LA UKOSEFU WA DAMU SALAMA NCHINI

Displaying DSC_0324.JPG

Sikika inasikitishwa na taarifa za kukosekana kwa damu salama katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Damu salama ni moja kati ya dawa muhimu kwa kuwa inakidhi vipaumbele vya afya katika  jamii kama ilivyobainishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Ni dawa muhimu na ya kipekee kwa kuwa pindi inapohitajika kutumika hakuna mbadala wala haiwezi kutengenezwa kiwandani. Hivyo, uwepo wa damu salama katika hospitali zetu ni jambo la lazima.

Nchini Tanzania, Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) uliopo chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, una wajibu wa kuhamasisha watu ili kujitolea damu. Vile vile, mpango huu una wajibu wa kuhakikisha kuwa damu salama pamoja na bidhaa zitokanazo na damu zinapatikana katika vituo vyenye dhamana ya kutoa huduma za damu.
                                  
Ijapokuwa NBTS imeweza  kuongeza upatikanaji wa damu salama kutoka chupa 12,500 (2005) hadi chupa 160,000 (2013) kwa mwaka, hata hivyo, ukusanyaji wa damu bado upo chini ya mahitaji halisi ya nchi ambayo ni kati ya chupa 400,000 hadi 450,000 kwa mwaka kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani. NBTS imekuwa ikikusanya takribani asilimia 38 tu ya mahitaji ya damu salama nchini kwa mwaka, hivyo kusababisha upungufu wa kudumu wa damu salama katika vituo vyenye dhamana ya kutoa huduma za damu nchini.

Kumekuwepo na taarifa katika vyombo mbalimbali vya habari kwa majuma kadhaa sasa, kuhusu upungufu mkubwa wa damu katika vituo vyenye dhamana ya kutoa huduma za damu nchini. Uhitaji wa damu salama nchini ni mkubwa kutokana na kuongezeka kwa tatizo la upungufu wa damu mwilini unaosababishwa na malaria na matatizo ya uzazi hasa wakati wa ujauzito na kujifungua. Tanzania ni moja kati ya nchi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara zenye idadi kubwa ya vifo vya watoto na wanawake. Inakadiriwa kuwa karibu asilimia 28-30 ya vifo vya kina mama vinatokana na upungufu wa damu mwilini. Hii inaweza kuonekana katika matumizi ya damu salama nchini ambayo karibu asilimia 80 ya damu inayokusanywa inatumika kwa wanawake na watoto, wakati asilimia 20 inatumika kwa matumizi mengine kama upasuaji, ugonjwa wa selimundu (sickle cell anaemia) na tiba ya saratani. Kwa hiyo upatikanaji wa damu salama kwa wakati unazuia kuongezeka kwa ugonjwa na hata vifo na hivyo kuboresha afya za wananchi.
Ni kutokana na umuhimu huu wa damu salama, Sikika iliamua kuangalia kwa undani ukubwa wa tatizo hili, sababu na namna linavyoweza kutatuliwa ili kuboresha upatikanaji wa damu salama nchini.

Katika utafiti wetu tulibaini kuwa, kuna upungufu mkubwa wa damu salama katika vituo vingi vya kutolea huduma hiyo. Kwa mfano katika wilaya ya Simanjiro, mahitaji ya damu salama kwa mwaka ni chupa 145 hata hivyo wamekuwa wakipokea chini ya nusu ya mahitaji yao. Mwaka 2013 walipokea chupa  74 tu, na kati ya mwezi Februari na Machi mwaka huu hawakuwa na akiba kabisa kwani mara ya mwisho kupokea damu ilikuwa mwezi Septemba mwaka 2014.

Hali hiyo pia ilionekana katika wilaya ya Mpwapwa, ambapo kati ya mwezi Februari na Machi 2015 hawakuwa na akiba ya damu salama. Mahitaji yao kwa mwaka ni chupa 1,400, hata hivyo wamekuwa wakipokea wastani wa chupa 20 kwa mwezi ambazo ni sawa na chupa  240 tu kwa mwaka ikiwa ni mara 6 pungufu ya mahitaji yao.

Kwa  mkoa wa Dar es salaam, hali ni kama ilivyo katika mikoa mingine ambapo, vituo vyote vilivyotembelewa vilikutwa na upungufu mkubwa wa damu salama kutokana na kupatiwa damu pungufu na NBTS. Kwa mfano, hospitali ya Wilaya ya Temeke imekuwa ikipokea  damu salama inayokidhi mahitaji ya hospitali kwa asilimia 20% tu kwa mwaka, huku hospitali ya Amana ikiwa inapatiwa asilimia 40% tu ya mahitaji yake.  Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambayo imekuwa ikishugulikia mgonjwa  makubwa na sugu, nayo imekuwa  ikipatiwa damu salama kwa takribani asilimia 50 - 60 ya mahitaji yake. Uhaba wa damu salama umekuwa sugu nchini kote kutokana na kuwa vituo vyote vinategemea NBTS katika kupatiwa bidhaa hiyo.

Sikika inatambua na inaamini  Serikali inatambua kuwa, chanzo kikubwa cha uhaba sugu wa damu salama nchini ni upungufu wa fedha unaoikabili NBTS. Hii inasababisha NBTS kushindwa kutekeleza majukumu yake muhimu kama vile kufanya kampeni za kuhamasisha wananchi kuchangia damu kwa hiari pamoja na kununua vitendanishi vya kutosha kwa ajili ya kupima, kuhifadhi na kutengeneza bidhaa zingine zitokanazo na damu salama. Kwa takribani miaka 10,  bajeti ya NBTS kwa  zaidi ya asilimia 80% imekuwa ikitoka kwa wafadhili, hususani Serikali ya Marekani, kupitia Mpango wa dharura wa  UKIMWI (PEPFAR) ambao wamekuwa wakipunguza ufadhili wao unaofikia  kikomo mwaka huu 2015. Serikali imekuwa ikichangia asilimia 20 tu ya bajeti ya NBTS  huku ikishindwa kuziba pengo lililokuwa linaachwa na wafadhili, jambo ambalo ndio chanzo kikubwa cha NBTS kushindwa kukusanya damu salama ya kutosha nchini. Kwa mfano, Mahitaji ya damu salama nchini ni chupa 100,000 hadi 112,000 kwa muhula kiasi ambacho NBTS imeshindwa kukusanya hata nusu ya kiasi hicho. Mathalani, katika kipindi cha mihula miwili iliyopita (Oktoba – Disemba 2014 na Januari – Machi 2015), NBTS imeweza kukusanya kiasi cha chupa 34,000 tu ambacho ni sawa na asilimia 17 ya mahitaji ya damu salama kwa kipindi hicho.

Kushindwa kwa NBTS kukusanya damu salama ya kutosha, kumepelekea baadhi ya vituo vya huduma kutumia damu wanayoikusanya kutoka kwa familia, ndugu na jamaa za wagonjwa badala ya kuipeleka katika vituo vya kanda au taifa kwa ajili ya kupima, kuhifadhi na kutengeneza bidhaa zingine zitokanazo na damu salama. Hii ni hatari kiafya, kwani huweza kusababisha maambukizi ya magonjwa na pia kuchangia matumizi mabaya ya damu kwa  kuwa vituo vya huduma havina mashine na utaalamu wa kutosha hususani katika kutengeneza bidhaa zingine zitokanazo na damu.

Kama ilivyo kwa bidhaa zingine,  uhaba wa damu salama kwa kiasi kikubwa umekuwa ukisababisha baadhi ya watoa huduma za afya kujihusisha na vitendo vya rushwa - ‘’kuuza damu kwa wagonjwa’’ kutokana na ongezeko la mahitaji ya damu huku upatikanaji wake ukiwa ni mdogo.

Sikika, tumefurahishwa na tunapongeza jitihada za wadau mbalimbali kama taasisi za kidini na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa kuandaa kampeni za kukusanya damu. Jitihada hizi ni nzuri katika kutatua tatizo kwa muda mfupi lakini kunahitajika mpango endelevu ambao utaiwezesha NBTS kutimiza wajibu wake ipasavyo.

Tunaitaka Serikali kuwajibika katika kutatua tatizo la damu salama nchini. Ni jukumu la Serikali kuiwezesha NBTS kifedha badala ya  kutegemea wafadhili na watu binafsi. Serikali ipange bajeti inayotosha pamoja na kutoa fedha kwa wakati kwa Mpango huu ili kuuwezesha kukusanya na kusambaza damu salama inayokidhi mahitaji ya nchi. Tunaamini kuwa, iwapo Mpango wa Taifa wa Damu Salama utakuwa na fedha za kutosha na zinazotolewa kwa wakati hakutakuwa na Upungufu wa damu salama nchini.  




Mr. Irenei Kiria, Mkurugenzi wa Sikika, S.L.P 12183 Dar es Salaam,
Simu: +255 222 666355/57, Nukushi: 2668015, Barua pepe: info@sikika.or.tz,
Twitter: @sikika1, Facebook: Sikika Tanzania, Tovuti: www.sikika.or.tz


No comments:

Post a Comment