Pages

Pages

Pages

Tuesday 10 March 2015

BASATA YATOA ELIMU KWA WASANII KUHUSU KATIBA INAYOPENDEKEZWA

Na Mwandishi Wetu
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kupitia programu yake ya Jukwaa la Sanaa wiki hii limetoa elimu kwa wasanii kuhusu maudhui ya katiba inayopendekezwa hasa ibara ya 59 ya katiba hiyo inayohusu sekta ya Sanaa.

Akizungumza katika programu hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa BASATA ulioko Ilala Sharif Shamba, Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba (BMK) aliyewakilisha wasanii Bw. Paul Mtenda alisema kwamba kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania katiba inayopendekezwa imeibeba tasnia ya Sanaa kitu ambacho ni mwanzo mzuri katika kupata sera na sheria bora za kuisimamia sekta.
“ Kitendo cha katiba pendekezwa kutambua uwepo wa Sanaa ni mwazo mzuri katika kupata sera, sheria na kanuni zilizo bora za kuisimamia sekta hii. Maana kupitishwa kwa katiba lazima kubadilishe sheria na kanuni mbalimbali zilizopo” alisema Mtenda.
Aliongeza kwamba, wasanii hawana budi kuisoma katiba inayopendekezwa na kuelewa maudhui yaliyomo na wasikubali kuwa wa kuhadithiwa na kuruhusu watu wengine kuwasemea na kuwaamulia.
Katika hili alisema kwamba wasanii toka mchakato wa kuandika katiba mpya ulipoanza wamekuwa wakipaza sauti ili nafasi ya Sanaa itambuliwe kikatiba sasa ni wakati wa wao kuhakikisha wanayasoma maudhui yote yaliyomo katika katiba inayopendekezwa na kuyaelewa vema ili kutumia sanaa kuwaelimisha wengine.
“Tulipaza sauti sana ili Sanaa itambuliwe na katiba inayopendekezwa, sasa tumefanikiwa. Kazi iliyopo ni kuisoma na kuielewa vema ili sasa tuweze kuwaelimisha na wengine kuhusu maudhui yaliyomo maana mwisho wa siku kila mmoja atakuwa na maamuzi yake kulingana na uelewa” alisisitiza Mtenda.
Akizungumzia ibara ya 59 inayozungumzia hakimiliki, hataza na hakibunifu kwa wasanii, Mtenda alisema kwamba bado kuna kazi kubwa ya kufanywa na wasanii pia wadau wa Sanaa ili kuhakikisha kunakuwa na sera, sheria na kanuni bora zaidi katika kuisimamia sekta ya Sanaa.

“Kutambuliwa kwa Sanaa katika katiba ni suala moja lakini suala la kuwa na sera, sheria na kanuni zilizo bora ni suala jingine. Wasanii lazima tuendelee kuyapigania haya” aliongeza. 

No comments:

Post a Comment