Pages

Pages

Pages

Friday 9 January 2015

SERIKALI YAOMBWA KUWAJALI WAHUDUMU WA MAJUMBANI WENYE VVU


Serikali imeombwa kuwajali na kuwapa kipaumbele wahudumu wa nyumbani wa waathirika wa Virusi vya Ukimwi VVU, kwani wamekuwa wakijitolea kwa moyo mmoja kuwasaidia wagonjwa lakini wamekuwa hawawezeshwi.


Mmoja kati ya wahudumu wa nyumbani wa waathirika wa VVU wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Paulina Simon (54) akizungumza juzi aliiomba Serikali iwaangalie kwa jicho la huduma.

Hata hivyo, Paulina amemuomba Rais Jakaya Kikwete amsaidie mtaji wa kuendesha maisha yake kwani anaishi kwenye maisha ya dhiki, japokuwa amekuwa msaada mkubwa wa kuwasaidia wagonjwa hao.

Paulina alisema yeye ni mjane tangu mwaka 1991 na amekuwa akiwahudumia waathirika wa VVU zaidi ya 100 kwa moyo mmoja bila kuwezeshwa kipato chochote na Serikali, hivyo iwajali na kuwawezesha wao wanaohudumia jamii.
 
Alisema anaomba Serikali kupitia Rais Kikwete kumpa msaada ili aweze kujikimu kimaisha kwani kupitia huduma hiyo amekuwa akipatiwa chakula na nauli ya kutoka Mirerani hadi Usa River wilayani Arumeru kuwapeleka wagonjwa.
 
“Nimekuwa niliwahudumia waathirika hawa kwa muda wa miaka saba bila kulipwa mshahara, lakini hiyo haijanishusha ari yangu ya kuwasaidia watanzania hawa ambao wameathirika na VVU,” alisema Paulina.
 
Alisema anawahudumia wagonjwa wa VVU waliopo Mirerani na maeneo ya jirani na kuwahamasisha, ila hivi sasa hawezi kuendesha maisha yake kwani anahitajika kulipa kodi ya nyumba na hana mtaji wa kujikimu maisha yake.
 
“Pale Usa River kwa mwezi mmoja huwa wananipa chakula unga kilo mbili, maharage kilo mbili na mafuta nusu kilo na nauli Sh 9,000 ya kuwapeleka wagonjwa wakapatiwe dawa za ARV,” alisema Paulina.

No comments:

Post a Comment