Pages

Pages

Pages

Thursday 1 January 2015

MBUNGE ATUHUMIWA KUGAWA ZAWADI KWA MBIO ZA MWAKANI

Catherine Magige
Mbunge wa Viti Maalum kupitia UVCCM Mkoa wa  Arusha, Catherine Magige, amelalamikiwa kwa kuwagombanisha viongozi wa Jumuiya ya Wanawake wa CCM (UWT)mkoa wa Arusha kutokana na kinachodaiwa ni mbio zake za ubunge kupitia jumuiya hiyo mwakani.


Mgongano huo unadaiwa kutokana na ukiukwaji wa kanuni kulikofanywa na mbunge huyo kwa kugawa zawadi za vitenge na mchele kwa  ajili ya sikukuu ya Krismasi kwa viongozi wa jumuiya hiyo wilaya na mkoa bila kuutaarifu uongozi wa jumuiya hiyo.

Kufuatia hatua hiyo, viongozi wa kamati ya utekelezaji wa jumuiya hiyo mkoa wa Arusha iliwasiliana na Magige na kumzuia  kugawa zawadi hizo.

Pia, kamati hiyo imemfungia ofisi kwa kubadilisha kitasa cha mlango na kumsimamisha kazi Katibu wa UWT mkoa wa Arusha, Stamili Dendegu, kwa tuhuma za kumruhusu Magige kugawa zawadi hizo na kumkaimisha ofisi katibu wa UWT wilaya ya Arusha, Fatma Hassan.

Akizungumzia hatua hizo jana mara baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati ya utekelezaji Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Arusha Flora Zelote, alikanusha kusimamishwa kazi kwa katibu huyo wala kuwapo kwa kikao kilichomjadili yeye.

Alipoulizwa sababu za kumtoa nje ya kikao katibu huyo ambaye ni mjumbe halali iwapo hakukua na ajenda ya kumjadili mwenyekiti, alikataa kujibu na kuhoji mwandishi alitoa wapi taarifa hizo.

Aidha, alipoulizwa kuhusu mgogoro uliosababishwa na madai kuwa Magige amegawa zawadi bila ya kuishirikisha jumuiya, alijibu kwa kifupi kuwa si kweli na wala hakukua na kikao kama hicho.

“Mimi ninakwambia hatuna tofauti na katibu wala nini na wala hatujamjadili yeye kuhusu suala lolote hata hilo la mbunge Catherine na wala hatujamfungia ofisi na kumkaimisha mtu mwingine,” alisema Zelote.

Naye Dendegu alikiri kuwapo kwa kikao hicho cha kumjadili yeye na kuwa alifukuzwa katika kikao hicho na baadaye aliitwa na kutaarifiwa kusimamishwa kazi na kutakiwa kukabidhi ofisi kwa katibu wa UWT wilaya ya Arusha.

Alisema alipohoji sababu za kuchukuliwa hatua hizo, alisema alijibiwa kuwa anatuhumiwa kutoa siri za vikao mbalimbali, lakini anachokitambua yeye ni kuhusu kauli yake katika kikao kilichomjadili Magigek uhusu kutoa zawadi kinyume cha utaratibu.

Alisema siku chache alipokea mbunge akimlalamikia kuhusu kauli aliyoitoa ya ukiukwaji wa kanuni za utoaji wa zawadi kwa viongozi wa jumuiya hiyo na kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa mkoa wa CCM.

“Mimi Catherine aliwahi kunipigia akanilalamikia nilivyozungumza juu ya zawadi alizozigawa bila utaratibu na aliniambia kuwa taarifa zote za kikao kile anazo, hivyo alitaka nimthibitishie mimi nilikataa kwa hiyo siyo suala la siri za vikao kama ni siri wao ndiyo wa kwanza kutoa maana angezipataje taarifa za kikao chetu,” alisema Dendegu.

Magige alisema yeye hatambui tuhuma hizo na wala hahusiki katika ugomvi huo kwa kuwa yeye siyo kiongozi wa nafasi yoyote katika jumuiya hiyo, bali yeye ni mbunge wa vijana.

Aliongeza kuwa pamoja na kwamba yeye ni mbunge wa vijana, anaruhusiwa kufanya shughuli zozote kwa vijana, lakini pia kwa akina mama kupitia UWT bila kuzuiwa na mtu yeyote.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment