Pages

Pages

Pages

Thursday 1 January 2015

HAKYANANI, MVUA ZA MWAKA HUU BALAA!

Displaying IMG_1090.JPG
Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt Agnes Kijazi akiongea na vyombo vya habari kuhusiana na mwelekeo wa utabiri wa hali ya hewa kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Februari 2015.

Displaying IMG_1079.JPG
Wanahabari wakichukua taarifa inayotolewa na Dkt. Kijazi katika ukumbi wa mikutano TMA.

A: UTANGULIZI
Taarifa hii inatoa tathmini ya mvua za vuli (Oktoba – Disemba, 2014) na mwelekeo wa mifumo ya hali ya hewa na mvua kwa kipindi cha miezi Januari hadi Februari, 2015.

B: MATUKIO YA MVUA KIPINDI CHA OKTOBA – DISEMBA, 2014
Katika msimu uliopita wa mvua za Vuli Oktoba hadi tarehe 30 Disemba, 2014, maeneo mengi ya nchi yalipata mvua za wastani hadi juu ya wastani isipokuwa maeneo machache ya mikoa ya Tanga, Dar Es Salaam, Dodoma (Hombolo), Kilimanjaro (Same), Njombe, Mtwara na Lindi ambayo yalipata mvua za chini ya wastani.
Mvua za vuli na za msimu ziliambatana na vipindi vya mvua kubwa katika nyakati mbali mbali kama inavyooneshwa kwenye jedwali Na. 1:
Matukio ya mvua hizi ambayo yaliambatana na vipindi vifupi vya upepo mkali, yalisababishwa na kuimarika kwa ukanda wa mvua magharibi mwa nchi ambao uliambatana na kuwepo kwa makutano ya upepo katika maeneo ya mikoa iliyotajwa hapo juu. Aidha hali hii ilipelekea baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Tabora na Arusha kupata mvua za mawe zilizo ambatana na upepo mkali na kusababisha uharibifu wa mali hususan katika eneo la Tumbi mkoani Tabora. Mifumo iliyopo ya hali ya hewa inatarajiwa kusababisha vipindi vya ongezeko la mvua katika baadhi ya maeneo ya Magharibi, nyanda za juu Kusini-magharibi na mikoa ya kusini mwa nchi.

JEDWALI NA. 1
Tarehe iliyopimwa      Kituo                   (Mkoa)                       Mvua iliyopimwa (mm)
30/12/2014                  Bandari               (Dar es Salaam)       69.3
29/12/2014                  Mahenge             (Morogoro)               42.8
                                                                      Mbeya                        40.6
28/12/2014                 Hombolo              (Dodoma)                  56.0
27/12/2014                  Mpanda                (Katavi)                     54.8
27/12/2014                  Nyiberekera         (Mara)                       35.8
26/12/2014                 Tumbi                    (Tabora)                   119.6
26/12/2014                 Tabora                   (Tabora)                     40.3
25/12/2014                 Bukoba                  (Kagera)                     31.8
25/12/2014                 Singida                  (Singida)                     31.1
24/12/2014                 Singida                   (Singida)                    83.6
24/12/2014                 Babati                     (Manyara)                  64.8
23/12/2014                 Mbozi                     (Mbeya)                      39.0
                                       Zanzibar                (Zanzibar)                  93.9
                                       Mahenge                (Morogoro)               60.1

D: MWELEKEO WA MVUA JANUARI – FEBRUARI, 2015.
Hali ya joto la juu ya wastani katika eneo la Tropikali ya Bahari ya Pasifiki linatarajiwa kuendelea kwa kipindi cha miezi ya Januari hadi Februari, 2015.
Kutokana na mwelekeo wa mifumo ya hali ya hewa inayotarajiwa, mvua za kipindi cha Januari hadi Februari, 2015 zinatarajiwa kuwa kama ifuatavyo:
(i) Maeneo yanayopata misimu miwili ya Mvua
Maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka hususan nyanda za juu Kaskazini mashariki, pwani ya Kaskazini, kanda ya Ziwa Viktoria na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, mvua katika maeneo haya zinatarajiwa kuisha mwishoni mwa mwezi Disemba, 2014. Hata hivyo matukio ya mvua za nje ya msimu yanatarajiwa katika kipindi cha miezi ya Januari 2015. Hali hii inatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, kusini mwa mkoa wa Pwani na baadhi ya maeneo ya mikoa ya Arusha, Manyara, Kagera, Geita, Shinyanga na Mwanza. Maeneo mengine yaliyosalia yanatarajiwa kuwa makavu kwa ujumla.
(ii) Maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua - Mvua za Msimu kipindi cha (Januari, – Februari, 2015)
Maeneo ya Magharibi mwa nchi, kanda ya kati, nyanda za juu Kusini-magharibi, Kusini mwa nchi na pwani ya kusini yanapata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka. Katika kipindi cha miezi ya Januari hadi Februari, 2015 maeneo hayo yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
Kanda ya Magharibi (Mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa):
Mvua zimeshaanza na zinatarajiwa kuwa za wastani katika maeneo hayo.
Kanda ya kati (Mikoa ya Singida na Dodoma):
Mvua zimeshaanza na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani.
Nyanda za juu Kusini-Magharibi: (Mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe na kusini mwa Morogoro):
Mvua zimeshaanza na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi.
Maeneo ya kusini na pwani ya kusini (mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara)
Mvua zimeshaanza na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi.
Izingatiwe kuwa pamoja na kuwapo kwa uwezekano wa matukio mengi ya mvua kubwa katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua juu ya wastani, hali hiyo pia inaweza kujitokeza katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.
Matukio ya Vimbunga katika eneo la kusini magharibi mwa Bahari ya Hindi yanatarajiwa kuchangia katika mwenendo wa mvua nchini. Maeneo ambayo hali ya mvua inaweza kuathiriwa zaidi na vimbunga ni pamoja na kanda ya kati, Nyanda za juu Kusini Magharibi, Magharibi mwa nchi na maeneo ya ukanda wa Pwani.

E: HALI YA JOTO
Viashiria vya mwenendo wa hali joto vinaonesha kuwa maeneo mbalimbali nchini yataendelea kuwa na joto juu ya wastani katika kipindi cha Mwezi Januari hadi Februari, 2015. Hali ya ongezeko la joto pia inatarajiwa katika maeneo ya magharibi na kusini magharibi mwa nchi ambayo mpaka sasa yamekuwa na joto la wastani. Wananchi katika maeneo husika wanashauriwa kuchuka hatua stahiki kujikinga na athari za kiafya na mazingira zinazoweza kusababishwa na ongezeko la joto linaloendelea.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa taarifa za mwelekeo wa mvua na hali joto nchini.

Dkt. Agnes L. Kijazi

MKURUGENZI MKUU

No comments:

Post a Comment