Pages

Pages

Pages

Friday 12 December 2014

WATANZANIA MILIONI 11 KUSHIRIKI UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA

Mkurugenzi wa uchaguzi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Khalist Luanda
Watanzania milioni 11,491,661 kati ya milioni 18,587,742 (asilimia 62) wamejiandikisha kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Jumapili ijayo.

Mikoa ya Katavi na Kagera imefanya vizuri kwa kuandikisha wapigakura wengi zaidi huku mikoa ya Dar es Salam na Kilimanjaro ikiandikisha idadi ndogo.

Hayo yalibainishwa jana na Mkurugenzi wa uchaguzi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Khalist Luanda, wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma.

Luanda alisema Watanzania hao ni sawa na asilimia 62 ya walioandikishwa wanatokana na taarifa za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ambayo yalionyesha kwamba asilimia 40 ya Watanzania wote wana umri  kuanzia miaka 18 na kuendelea.

Akizungumzia kuhusu mikoa iliyofanya vizuri, alisema Katavi umeandikisha wapigakura asilimia 79 wakati Kagera ni asilimia 78.

Kwa mujibu wa  Luanda, mikoa iliyoandikisha wapigakura wachache ni Dar es Salaam asilimia 43 na Kilimanjaro asilimia 50.

Luanda alibanisha kuwa Halmashauri zilizovuka lengo ni ya Mji wa Mpanda(107%) na Mji wa Babati (101%) wakati zilizoandikisha kwa asilimia ndogo ni Kilindi (21%) na Same (22%).

“Katika uchaguzi huo karatasi za kupigia kura zitaandaliwa na Halmashauri husika na ambayo itakuwa sifa ya jina la mgombea, jina la chama, nembo ya chama na Nembo ya halmashauri na ingizo jipya ni Nembo ya Chama ili kuwasaidia wale wasiojua kusoma,” alisema Luanda.

Alivionya vyama vya siasa vinavyotoa vitisho kwa wagombea kuacha vitendo hivyo, badala yake viwahamasishe wapiga kura wao kujitokeza kwa wingi kupiga kura.

Alisema, vituo vya kupiga kura vitafunguliwa saa  mbili asubuhi na kufungwa saa 10 jioni huku akiwaasa wapiga kura kufika Kwa wakati vituoni kwani wale watakaochelewa watapoteza fursa hiyo.

Kuhusu idadi ya wagombea waliopita bila kupingwa, Luanda alisema bado wanajumlisha na idadi hiyo na itatolewa wakati wa kutangaza matokeo ya ujumla baada ya uchaguzi huo.

Alisema pia bado wanakusanya taarifa za mapingamizi yaliyopita na yaliyokataliwa na yatatolewa katika matokeo ya ujumla.

 CCM, CHADEMA WACHUANA ARUSHAUshindani mkubwa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa Halmashauri ya Jiji la Arusha, upo kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambavyo kila kimoja kimesimamisha wagombea 154 wa nafasi za mwenyekiti na wajumbe wao.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, Mkurugenzi wa Jiji hilo, Juma Iddi, alisema kutokana na ushindani, kumekuwa na mhemko mkubwa wa uchaguzi huo kama ambavyo unakuwa katika uchaguzi mkuu.

Alisema chama kinachofuatia kwa kusimamisha wagombea wengi ni ACT Tanzania ambacho kina wagombea 11, huku Chama cha Wananchi (CUF) kikiwa na wagombea watano, TLP pamoja na NCCR-Mageuzi wagombea mmoja mmoja kwa kila mtaa.

Aidha alisema katika mitaa mitatu wagombea wa nafasi za uenyekiti kupitia CCM wameshinda bila kupingwa isipokuwa uchaguzi utakaofanyika utakuwa kwa ajili ya wajumbe.
Akizungumzia kuhusu ulinzi siku ya kupiga kura, alisema wamekubaliana na viongozi wa vyama  ya siasa ambavyo vinashiriki katika uchaguzi huo kuwa waongeze idadi ya wasimamizi, polisi, mgambo na askari wa jiji.

Alisema kwa mujibu wa taratibu za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, msimamizi wa uchaguzi ameteua waandikishaji wa orodha ya wapiga kura 154, wasimamizi wasaidizi ngazi ya mitaa 154 na wasimamizi wasaidizi ngazi ya kata 25 na wasimamizi wasaidizi ngazi ya halmashauri 17.

Alisema jumla ya watu 113, 627 wamejiandikisha kupiga kura kwa siku saba kuanzia Novemba 23 hadi 29 mwaka huu na hadi kukamilika kwa zoezi hilo ikiwa ni sawa na asilimia 58 ya watu waliokadiriwa.

Jumla ya watu 196,399 walikadiriwa kujiandikisha kupiga kura katika uchaguzi huo.

Alitoa rai kwa wananchi wote waliojiandikisha kwenda kupiga kura katika vituo walivyoandikisha mapema Desemba 14, mwaka huu, na kwamba vituo vitakuwa vimefunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10: 00.

Hata hivyo, alisema watu watakaokuwa wamesimama kwenye foleni za kupigia kura hadi wakati wa mwisho wa kufunga kupiga kura yaani saa 10:00 wataendelea kupiga kura mpaka watakapomaliza na kisha kazi ya kuhesabu kura itaanza mara moja na kutangaza matokeo.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment