Pages

Pages

Pages

Thursday 11 December 2014

BODI YAHAHA KUMNASUA TIBAIJUKA NA ESCROW


BODI ya Wadhamini ya Shule ya Sekondari ya Barbro Johansson (JOHA TRUST), imesema fedha zilizotolewa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow kiasi cha sh. bilioni 1.6, kwenda kwenye akaunti ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ziliombwa na Bodi hiyo kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na mabweni ya shule hiyo.

Akizungumza kwenye mkutano wa wazazi wa wanafunzi wa shule hiyo Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Salmon Odunga, alisema mchango huo wa sh. bilioni 1.6 uliotolewa na James Rugemalira kupitia mwanzilishi wa shule hiyo, Profesa Tibaijuka.

Alisema bado hawajaamini na wanashindwa kuelewa kwa nini Profesa Tibaijuka, anatakiwa kuwajibishwa kwa nafasi yake serikalini, wakati alipokea kiasi hicho cha fedha kwa niaba ya shule.

“Jambo hili linatuchanganya na kuwakatisha tamaa wananchi wa kawaida wanaojitolea kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo kusaidia sekta ya afya, maji vijana walemavu watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu katika taifa hili changa,” alisema.

Alisema Rais Kikwete alione jambo hili kwani ikiwa ni michango ya maendeleo inayopokelewa na viongozi kwa niaba ya wadau wao itatafsiriwa kama zawadi zao binafsi, kuna hatari ya kuzorotesha maendeleo.

Alisema Bodi ilimwomba Profesa Tibaijuka kuwaomba baadhi ya wafanyabiashara mashuhuri nchini kuunga mkono shughuli za asasi hiyo kwa michango ili kuweza kukamilisha ujenzi wa madarasa ya shule hiyo na James Rugemalira alikuwa miongoni mwa watu hao.

“Tuliomba mchango huo kwa barua Aprili 4, mwaka 2012 kupitia kampuni ya Mabibo Beer Winers and Spirits Limited na mapema Februari mwaka huu bila kutaja kiasi, Rugemalira alimjulisha mwanzilishi Profesa Tibaijuka kwamba yuko tayari kutoa mchango kwa sharti la yeye (Tibaijuka) kufungua akaunti Benki ya Mkombozi ili aweke mchango wake na aweze kuuchukua na kuupeleka akaunti ya shule,” alisema Odunga.

Aliongezea kuwa Profesa Tibaijuka alifungua akaunti hiyo Februari tatu mwaka huu na kupokea mchango huo wa jumla sh. bilioni 1.6 kwa niaba ya shule na Februari 12, mwaka huu fedha ziliingizwa kutoka kwa kampuni ya VIP Engineering.

Odunga alisema kuwa Februari 13 mwaka huu Bodi ya Wadhamini wa Barbro ilikaa katika kikao chao na kupokea taarifa ya mchango huo mkubwa kutoka kwa Rugemalira kupitia kampuni yake ya VIP Engineering na bodi ilikubali na kuamua mchango huo utumike kulipa sehemu ya deni la shule katika Bank M.

Alisema Profesa Tibaijuka aliagizwa na shule hiyo kuhamisha fedha hizo kutoka akaunti yake ya Mkombozi kwenda akaunti ya Bank M kulipa mkopo huo. “Hii inajibu maswali yaliyoulizwa kuwa kwa nini fedha hizo zilihama kwa haraka kutoka Benki ya Mkombozi kwenda Bank M,” alisema.

Alisema ili kutekeleza Master plan ya Joha Trust ilikuwa imechukua mkopo wa sh. bilioni mbili kutoka Bank M kwa ajili ya ujenzi wa bweni kubwa lenye uwezo wa kuweka vitanda 163 hadi kufikia Aprili 14 mkopo huo ulipolipwa wote deni lilikuwa limezaa riba na gharama nyingine hadi kufikia sh. bilioni 2.7 na mchango uliotolewa na Rugemalira ulilipa sehemu ya mchango,”alisema.

Hata hivyo, alisema shirika halina utaratibu wa kuwahoji wafadhili wa ndani na nje ya nchi kwanza ili kuthibitisha chanzo cha fedha zao wanawachangia, misaada yote wanapokea iwe midogo hata mikubwa imekuwa ikipokelewa kwa nia njema.

CREDIT: MAJIRA

No comments:

Post a Comment