Pages

Pages

Pages

Thursday 20 November 2014

SHY-ROSE, NDERAKINDO WATIBUANA NAIROBI

Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kutoka Tanzania Shy-Rose Banji.

N Salome Kitomary
Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kutoka Tanzania Shy -Rose Banji (pichani) na Nderakindo Kessy, wanadaiwa kuingia katika mtafaruku wakiwa jijini Nairobi, Kenya katika vikao vya Bunge hilo.


Taarifa za tukio hilo zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii zikieleza kuwa Shy-Rose anashikiliwa katika kituo cha Polisi cha Kamkunji, Nairobi.

Taarifa hizo zimeeleza kuwa sababu za kushikiliwa kwake ni baada ya kumkunja na kumpiga ngumi mbunge mwenzake na chanzo cha ugomvu hakijajulikana.

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kuongeza kuwa Kessy ambaye anatoka NCCR-Mageuzi, alikumbana na kipigo hicho juzi jioni, Jijini Nairobi.

“Tumepokea taarifa kutoka kwa Wabunge wa Rwanda wakinieleza kwamba Nderakindo, amepigwa na mbunge mwenzake (Shy-Rose) na kuumizwa vibaya, tuliomba msaada apelekwe hospitali huku tukiendelea kuzungumza na mwanasheria aliyeko Nairobi tufungue kesi,” alibainisha Mbatia.

Hivi karibuni, Mbunge Nderakindo, alisikika akihojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), kuhusu sakata la baadhi ya wabunge kutaka kumtimua Spika wa Bunge hilo, Dk. Margaret Zziwa, kwa madai ya kushindwa kuwawajibisha baadhi ya wabunge walionyesha utovu wa nidhamu.

Alisema ameshakusanya saini 32 ambazo zinatosha kumuondoa Spika huyo na mmoja wa wabunge wanaolalamikiwa, Shy-Rose.

“Kwa Tanzania kuna saini mbili tu, lengo kubwa la kumuondoa ni sehemu ya mchezo mchafu ili kikundi fulani wamuweke Spika mwingine kwa maslahi ya wachache.”

Kwa muda mrefu kumekuwa na taarifa za kumtuhumu Shy-Rose, kwa kutoa lugha mbaya kwa baadhi ya wabunge, kuwatukana baadhi ya marais wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, ulevi wa kupindukia, kufanya fujo na kuvunja chupa ndani ya ndege na kufungwa pingu wakati wa ziara ya wabunge wa EALA nchini Ubelgiji.

Hata hivyo, alizikana tuhuma hizo akisema siyo za kweli  bali zinakusudi la kumchafua kwa kuwa amekuwa mstari wa mbele kupinga kung’olewa kwa Spika Zziwa.
Aliweka bayana kusudio lake la kuwachukulia hatua za kisheria wabunge wenzake wanaomshutumu.

Jitihada za kumpata Shy-Rose hazikufanikiwa baada ya simu yake ya kiganjani kutopatikana.

Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Abdullah Juma Saadalla, alipoulizwa na NIPASHE juu mtafaruku kati ya wabunge hao wawili wa Tanzania, alithibitisha kutokea akisema chanzo ni kutoelwana, lakini alisema hana taarifa za kukamatwa kwa Shy-Rose.

“Hawakupigana ila wakati Banji anatoka kwenye ukumbi wa Bunge kuelekea kwenye gari, alimgonga mwenzake, bahati mbaya Kessy akafikiri kagongwa makusudi na kwenda polisi kufungua jalada na kupelekwa hospitali,” alisema.

Alisema baada ya taarifa hizo alikutana nao wote wawili kwa nyakati tofauti na kwamba Shy-Rose alidai alimgonga Kessy kwa bahati mbaya na kama mwenzake amekasirika yupo tayari kumuomba msamaha.

Alisema alipokutana na Kessy, alidai alipigwa makusudi na anashughulikia PF3 kwa ajili ya matibabu.

Alipoulizwa Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso, kama wana taarifa za tukio hilo, alisema hawajazipata rasmi zaidi ya kusikia tetesi na kwamba wanafuatilia.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment