Pages

Pages

Pages

Monday 3 November 2014

CHADEMA YASEMA IMEMCHOKA SHIBUDA

Magare John Shibuda, Mbunge wa Maswa Magharibi (Chadema)

Na Elizabeth Zaya
Mbunge wa Maswa Mashariki Sylivesta Kasulumbai (Chadema), amemshukia Mbunge wa Maswa Magharibi John Shibuda (Chadema) kwamba amewatelekeza wananchi wake kwa kutotekeleza ahadi  alizowaahidi.

Kadhalika, amesema Shibuda mbali na  usaliti kwa wananchi, lakini pia ni msaliti wa chama chake hususani kwa kusaliti maoni ya wananchi waliyoyatoa kwa iliyokuwa tume ya mabadiliko ya Katiba.

Akihutubia wakazi wa Kata ya Malampaka,katika ziara ya Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Kasulumbai alisema Shibuda amekuwa kama kinyonga ambaye wakati wote huweza kubadilika.

Kasulumbai alisema kwa kitendo ambacho Shibuda  amekionyesha kwa wananchi wake na  chama chake hawako tayari kumpa nafasi tena.

Kasulumbai ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema  Kanda ya Ziwa Mashariki inayoundwa na  mikoa ya Simiyu, Shinyanga na  Mara, alitumia nafasi hiyo kuwatangazia vijana na  mtu yeyote wa Chadema ambaye yuko tayari kuwania nafasi ya ubunge katika Jimbo  hilo kujiandaa mara moja kuwania jimbo hilo.

“Shibuda amewasaliti wananchi wake, amesahau wananchi walimwamini wakampa kura akashinda kwa kishindo lakini hajaja hata kuwatembelea, ameshindwa kutekeleza ahadi za wananchi amewaacha kama yatima,”  alisema na  kuongeza:

“Ni adui namba moja wa maendeleo ya wananchi, anajikomba komba kwa vigogo na  kusababisha maendeleo mengi ya wananchi kukwama, nilikuwa mmojawapo wa watetezi wake kipindi chama kilipotaka kumwadhibu kutokana na  matendo yake hayo, lakini kwa sasa nimechoka na  ninasema bora aadhibiwe na  nawatangazia vijana na  mtu yeyote wa Chadema anayetaka kugombea jimbo  hili ajiandae.”

Mwenyekiti mstaafu wa baraza la vijana la Chadema (Bavicha), John Heche, alisema kwa usaliti ambao Shibuda ameifanya ni halali yake kuadhibiwa na  chama.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment