Pages

Pages

Pages

Wednesday 22 October 2014

MAHAKAMA YAMPA ONYO MDEE NA WENZAKE


Mwenyekiti wa  Baraza la Wanawake  wa Chadema, Halima  Mdee akihutubia kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika juzi katika eneo la Nansio, wilayani Ukerewe, Mwanza. Picha na  Jovither Kaijage 
Na Tausi Ally, Mwananchi
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewataka wadhamini wa Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (35) na washtakiwa wenzake kuwa makini na ratiba zao ili kuepuka kuchelewesha kesi inayowakabili mahakamani hapo.
Hakimu Mkazi, Janeth Kaluyenda alitoa onyo hilo jana muda mfupi baada ya Wakili wa Serikali, Mohamed Salum kuieleza Mahakama kuwa kesi ilikuja kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali na kwamba mshtakiwa Halima Mdee, Renina Peter na Sophia Fangel hawapo.
Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, wadhamini wa Mdee walisimama na kueleza kuwa hakufika mahakamani hapo kwa sababu yuko kwenye shughuli za kichama Kanda ya Ziwa na alipaswa kurejea Dar es Salaam juzi jioni ili kuwahi kesi yake. Mdhamini huyo aliiambia Mahakama hiyo, Mdee alishindwa kufanya hivyo baada ya Ndege ya Fast Jet aliyotarajia kusafiri nayo kuja jijini kuahirisha safari.
Mdhamini wa mshtakiwa Renina Peter, aliieleza Mahakama kuwa hakufika mahakamani hapo kwa sababu alifiwa na baba yake mzazi na kwamba alizikwa jana.
Pia, mdhamini wa mshtakiwa, Sophia Fangel (28) naye aliiambia Mahakama kuwa yeye alikuwa kwenye shughuli za kichama Kanda ya Ziwa na Mdee ambao wote kwa pamoja walishindwa kurejea jijini kutokana Fast Jet kufuta safari siku hiyo.
Wakili wa Serikali, Mohamed Salum aliiambia Mahakama sababu iliyotolewa na wadhamini wa Renina ina msingi, lakini zile zilizotolewa na wadhamini wa Mdee na Sophia hazina msingi na kuitaka Mahakama kuwaonya washtakiwa.
“Mheshimiwa, ukiruhusu hilo la ziara za kichama utakuwa umefungua boksi kwa kila mtu, naomba utoe karipio kali,” alisema Salum.
Wakili Peter Kibatala anayewatetea washtakiwa hao, aliieleza Mahakama kuwa kitu kilichowafanya wateja wake washindwe kufika mahakamani hapo ni kukosa ndege na kwamba licha ya kuwapo kwa hilo wametimiza masharti ya kuwaleta wadhamini wao na siku kesi. Hakimu Kaluyenda baada ya kusikiliza maelezo hayo, aliwaeleza wadhamini wa washtakiwa hao kuwa makini katika ratiba zao ili wasije kuichelewesha kesi hiyo kumalizika.
Aliiahirisha hadi Novemba 5, 2014 na washtakiwa watasomewa maelezo ya awali kwa kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.
Washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni mkazi wa Kinondoni B, Rose Moshi (45), Anna Linjewile (48) mkazi wa Mbezi Luis, Mwanne Kassim (32) mkazi wa Pugu Kajiungeni, Sophia Fangel (28) mkazi Mbezi Beach, Edward Julius (25) mkazi wa Msasani, Martha Mtiko (27) mkazi wa Mikocheni ‘A’ na Beatu Mmari (35) mkazi wa Kinondoni Mkwajuni.
Kwa pamoja washtakiwa hao wanadaiwa kuwa Oktoba 4, mwaka huu Mtaa wa Ufipa, bila kuwa na uhalali walikiuka amri halali ya kutawanyika iliyotolewa na Mrakibu wa Polisi (SP) Emmanuel Tillf kwa niaba ya Jeshi la Polisi.
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment