Pages

Pages

Pages

Friday 3 October 2014

HATARI: SHEIKH AMWAGIWA TINDIKALI SONGEA


Sheikh Nasibu Ally Lwambano ambaye anadaiwa kumwagiwa tindikali mkoani Ruvuma 
Na Joyce Joliga, Mwananchi
Songea. Watu wasiofahamika wamemwagia tindikali, mkazi wa Kijiji cha Kitanda Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Sheikh Nasib Ally (80) na kumpofua jicho lake la kushoto.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Mskhiela alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 10 alfajiri wakati sheikh huyo alipokuwa akioga nyumbani kwake.
“Sheikh alikuwa akioga nyumbani kwake ikiwa ni maandalizi ya kwenda kuswalisha swala ya alfajiri. Walitokea watu, wakammulika kwa tochi na kisha kumwagia maji yanasadikiwa kuwa ni tindikali na kumuunguza,” alisema.
Kamanda Mskhiela alisema mara baada ya tukio hilo wahusika walikimbia na kumwacha sheikh huyo akilia kutokana na maumivu makali na ndugu na majirani walijitokeza kumsaidia na kumpeleka Hospitali ya Peramiho ambako hakupatiwa matibabu hapo kwa kuwa hospitali hiyo haina daktari bingwa wa macho.
Badala yake Sheikh Ally alipelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma ambako anaendelea na matibabu. Hata hivyo, alisema hali yake bado ni mbaya kwani jicho lake la kushoto limeharibiwa vibaya na halina uwezo wa kuona.
Alisema polisi imetuma wapelelezi katika kijiji hicho ambao wanaendelea na uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo.
“Hadi sasa chanzo cha tukio hakijajulikana, pia hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa kuhusiana na tukio hilo,” alisema.
CREDIT: MWANANCHI

1 comment: