Dar es Salaam. Wakati kukiwa hakuna taarifa za majopo ya uchunguzi yaliyowahi kuundwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu wa Dar es Salaam, Suleiman Kova katika matukio mbalimbali, jana aliunda jopo jipya kuchunguza kifo cha mtuhumiwa kinachohusishwa na kipigo cha polisi.
Jana, Kamanda Kova alitangaza jopo
hilo la wapelelezi kuchunguza kifo cha Liberatus Matemu (55) aliyefia
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akidaiwa kupigwa na polisi katika
Kituo cha Stakishari na maiti yake kukataliwa na nduguze.
Kabla
ya kufariki Jumapili iliyopita, Matemu alikuwa chini ya ulinzi katika
kituo hicho kilichopo wilayani Ilala ambako alikaa kwa siku nane.
Jopo hilo linaundwa huku kukiwa hakuna taarifa zozote za uchunguzi zilizotolewa na kamanda huyo kuhusu matukio yaliyotangulia.
Majopo mengine
Julai
23, mwaka huu, Kova aliunda timu ya wataalamu saba kuchunguza kashfa ya
viungo vya binadamu vilivyookotwa Mbweni Mpiji, wilayani Kinondoni
ambavyo vilidaiwa vilikuwa vikitumiwa katika Chuo Kikuu cha Kimataifa
cha Tiba na Afya (Imtu) lakini hadi sasa wananchi hawajajulishwa kuhusu
majibu ya uchunguzi huo.
Mei 21, mwaka huu, Kova
aliunda jopo la wapelelezi liliongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Jaffari Mohamed kuchunguza kifo cha aliyekuwa
Meneja Biashara ya Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji
(Ewura), Julius Gashaza aliyedaiwa kujinyonga na hadi leo taarifa za
uchunguzi huo hazijatangazwa.
Januari 7, mwaka huu,
Kamanda Kova aliunda jopo la wapelelezi wanane walioongozwa na Mohamed
kuchunguza tukio la kutekwa Mwenyekiti wa Chadema, Wilaya ya Temeke,
Joseph Yona na matokeo yake hayajawekwa wazi.
Uchunguzi mpya
Akizungumza
jana, Kova alisema jopo la kuchunguza kifo tata cha Matemu litaongozwa
na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Costantine
Masawe.
Alisema taarifa za awali zinaonyesha kwamba
marehemu alikuwa na ugomvi mkubwa kati yake na mtu mwingine ambaye
wamekuwa wakishambuliana kila wanapokutana.
Kamanda Kova
alisema ameona ni bora uchunguzi huo ufanyike ili kuondoa utata na
kupata taarifa kamili kuhusu ugomvi uliosababisha kushambuliana mara kwa
mara.
Kova alisema uchunguzi huo unafanywa ili
kuangalia Matemu alivyokamatwa, alivyokaa mahabusu, alivyopelekwa katika
Hospitali ya Amana na baadaye katika Hospitali ya Muhimbili.
“Uchunguzi
huu utahusisha madaktari bingwa wanaohusika na uchunguzi wa miili ya
watu waliokufa katika mazingira yenye utata,” alisema.
Alisema
jopo hilo pia litamhusisha mwanasheria wa familia ya Matemu na
mwanasheria mwingine kutoka serikalini ili kuhakikisha kunakuwa na
ukweli na uwazi.
Uchunguzi wa mwili leo
Mwanasheria
wa familia ya marehemu Matemu, Benedict Baligiye alisema mwili wa
marehemu utafanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Muhimbili leo.
“Tukipata taarifa ya uchunguzi ndipo ndugu wataanza kufanya maandalizi ya mazishi,” alisema.
CREDIT: MWANANCHI: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Kova-aongeza-idadi-ya--tume--D-Salaam/-/1597296/2439458/-/12neje7/-/index.html
CREDIT: MWANANCHI: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Kova-aongeza-idadi-ya--tume--D-Salaam/-/1597296/2439458/-/12neje7/-/index.html
No comments:
Post a Comment