Pages

Pages

Pages

Sunday 21 September 2014

RASIMU YA TATU YA KATIBA KUKABIDHIWA LEO, ITAWEKWA HADHARANI KESHO!


Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Uandishi wa Katiba itakayopendekezwa wakiwa kazini.


Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Bunge hilo, Samuel Sitta, leo anatarajiwa kukabidhiwa Rasimu ya Tatu ya Katiba mpya, kabla ya kuwekwa hadharani kesho.
Ratiba ya Bunge hilo inaonesha

kuwa tangu Jumanne iliyopita, Kamati ya Uandishi inayoongozwa na Andrew Chenge na Mgeni Hassan Juma na sekretarieti yake, ilikuwa na jukumu la kuandika rasimu hiyo ambayo ilipaswa kukamilika jana.
Baada ya kazi hiyo, Kamati hiyo ya Uandishi, inatarajiwa kuwasilisha rasimu hiyo kwa Bunge Maalumu la Katiba kesho na hivyo kupitia bunge hilo kwa umma wa Watanzania.
Rasimu hiyo ya Tatu itakayokabidhiwa leo saa 8:00 mchana, inatarajiwa kubeba sehemu kubwa ya maudhui ya Katiba inayopendekezwa, ambayo itapigiwa kura ya maoni na Watanzania baada ya Uchaguzi Mkuu ujao.
Kwa mujibu wa Ratiba hiyo, kesho na keshokutwa, wajumbe wa Bunge Maalumu watapata muda wa kuitafakari rasimu hiyo ya Katiba, kabla ya kurejea bungeni Jumatano na Alhamisi ijayo kuhakiki na kujadili ibara za rasimu hiyo.


MarekebishoIjumaa ijayo ratiba inaonesha kuwa Kamati ya Uandishi itarejea kibaruani kufanya marekebisho ya mwisho ya Ibara za Rasimu ya Mwisho ya Katiba.
Aidha, Septemba 27, Kamati ya Uandishi itawasilisha Rasimu ya Mwisho ya Katiba bungeni, ambapo Jumapili kamati za Bunge Maalumu la Katiba, zitajielimisha kuhusu Rasimu ya Mwisho ya Katiba na taratibu za upigaji kura.
Kura ya kupata Katiba inayopendekezwa, kwa mujibu wa ratiba hiyo, inatarajiwa kuanza kupigwa kuanzia Jumatatu ya Septemba 29 mpaka Oktoba 2.

Wakati mchakato huo ukiwa katika hatua za mwisho, ule uoga wa kukosekana kwa theluthi mbili za kura kutoka Tanzania Bara za Zanzibar, uliosababishwa na kutokuwepo kwa baadhi ya wajumbe kutoka kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umeanza kuondoka.
Tayari Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha Rose Migiro, ameshatoa tamko kuonesha kuwa wajumbe wa Ukawa, waliosusa wakitarajia kukwamisha kupatikana kwa Katiba inayopendekezwa, hawatakuwa na athari.
Kwa mujibu wa Dk Migiro, idadi ya wajumbe wote walikuwa 630, na Ukawa waliosusa ni 130 tu ambao ni sawa na asilimia 21 ya wajumbe wote.
Kwa maana hiyo wajumbe waliobaki ni 500, sawa na asilimia 79 ya wajumbe wote ambao ni zaidi ya theluthi mbili tayari. Dk Migiro aliweka wazi kuwa wajumbe wanaotoka Tanzania Bara ni 348 na kati yao, 125 wanatoka kundi la 201.

Kwa Zanzibar, takwimu hiyo inaonesha wapo wajumbe 152 ambao kati yao 64 wanatoka kundi la 201.

No comments:

Post a Comment