Utangulizi
Mheshimiwa Dkt. Rehema Nchimbi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;
Waheshimiwa Mawaziri;
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya, Wabunge, Wenyeviti na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya na Miji;
Waheshimwa Madiwani;
Wazee Wangu;
Ndugu wananchi;
Kuna
methali ya Kiswahili isemayo hakuna refu lisilokuwa na ncha. Hatimaye
ziara yangu ya Mkoa wa Dodoma imefikia mwisho. Ziara hii niliyoianza
tarehe 28 Agosti, 2014 imenifikisha kwenye wilaya zote za Mkoa wa
Dodoma. Madhumuni ya ziara yangu yalikuwa kuona shughuli za maendeleo.
Kuona tulipofanikiwa na pale ambapo pana matatizo tupatafutie ufumbuzi.
Nimefarijika sana na hatua kubwa za maendeleo ambazo kila wilaya
imezifikia. Nimejionea maendeleo makubwa katika sekta na nyanja
mbalimbali za maisha ya wananchi wa mkoa huu. Hongereni sana. Aidha,
nimeona au kusimuliwa kuhusu
changamoto kubwa na ndogo
zinazowakabili, ambazo zikiweza kupatiwa ufumbuzi ufanisi utaongezeka na
kasi ya kujiletea maendeleo itakuwa kubwa zaidi.
Elimu
Natoa
pongezi nyingi kwa viongozi na wananchi wa Mkoa wa Dodoma kwa juhudi
kubwa mnazofanya na mafanikio mliyopata au mnayoendelea kupata katika
kuendeleza elimu Mkoani kwenu. Kwa ajili hiyo basi idadi ya wanafunzi
katika ngazi za awali, msingi na sekondari imekuwa kubwa kuliko wakati
mwingine wo wote katika historia ya nchi yetu. Hivi sasa Mkoani Dodoma
kuna wanafunzi wa Awali 47,427, wa Shule za Msingi 391,475 na wa
Sekondari 59,035 ukilinganisha na wanafunzi wa Awali 55,524, wa Shule za
Msingi 152,366 na wa Sekondari 24,288 mwaka 2007.Jukumu lililoko mbele
yenu na mbele yetu pia ni kutatua matatizo yanayoikabili sekta ya elimu
mkoani. Pamoja na kupanda kuliko ilivyokuwa mwaka 2012, kiwango cha
ufaulu cha asilimia 38.2 kwa shule za msingi na asilimia 55.4 kwa shule
za sekondari kwa mwaka 2013 ni chini ya wastani wa taifa wa asilimia
50.61 kwa shule za msingi na asilimia 58.25 kwa shule za sekondari.
Hivyo mnayo kazi kubwa ya kufanya ili kufikia kiwango cha ufaulu cha
asilimia 60mwaka huu na asilimia 80 mwakani. Ongezeni bidii.
Napenda
kuwahakikishia kuwa sisi katika Serikali kuu tutaendelea kutimiza
wajibu wetu kuhusu elimu. Tutaendelea kuleta walimu, vitabu na vifaa vya
kujifunzia na kufundishia. Hali kadhalika tutaendelea kutoa pesa
zitakazoboresha miundombinu ya shule na nyumba za walimu. Kwa upande wa
walimu tumefanikiwa kutosheleza mahitaji ya walimu wa masomo ya sanaa
kwa shule zote za sekondari. Kwa baadhi ya Wilaya kuna ziada ya walimu
hao. Hii ndiyo hali ilivyo kote nchini. Hata hivyo, kuna upungufu mkubwa
wa walimu wa sayansi jambo ambalo ni tatizo la kitaifa.
Mkoa
wa Dodoma una mahitaji ya walimu 4,076.Waliopo ni walimu 3,250, kati
yao walimu 2,482 wa sanaa na 645 wa sayansi. Kuna jumla ya upungufu wa
walimu 949 wa sayansi na ziada ya walimu 123 wa sanaa. Walimu wa ziada
kwa masomo ya sanaa wapo Wilaya za Mpwapwa (34), Bahi (55), Dodoma Mjini
(86) na Kongwa (92). Upungufu wa walimu wa sanaa upo Wilaya za Chamwino
(103), Chemba (9), na Kondoa (32). Upungufu wa walimu wa sayansi upo
wilaya zote. Hivi sasa kitaifa tuna pengo la walimu 23,500 na uwezo wa
vyuo vyetu ni kuzalisha wanafunzi 2,500 kwa mwaka. Tumedhamiria
kulikabili tatizo hili kwa nguvu zote na maarifa yetu yote. Sina
wasiwasi kwamba tutafanikwia kama ilivyokuwa kwa changamoto nyingine
nyinig.
Kuhusu ujenzi wa maabara katika shule
za Sekondari za Kata, narudia kuwakumbusha viongozi wa Wilaya na Mkoa wa
Dodoma kwamba muda wa miaka miwili tuliopeana mwaka 2012 unaisha mwezi
Novemba, 2014. Na, kupitia kwenu nawakumbusha viongozi wa Mikoa yote na
Wilaya zote nchini ifikapo Novemba mwaka huu tutaulizana. Hatutaacha
kubanana na kama hapana budi kuwajibishana.
Tunaendelea
kuboresha upatikanaji wa vitabu kwa wanafunzi wa shule za msingi na
sekondari. Mpaka sasa uwiano wa kitabu kwa wanafunzi umefikia 1:3.
Tutaendelea kutenga fedha zaidi ili kila mwanafunzi awe na kitabu chake.
Suala la nyumba za walimu nalo ni jambo ambalo tunalipa umuhimu.
Tunaendelea kuanzia mwaka wa jana kutekeleza mpango wa kuzipatia
shilingi milioni 500kila Halmashauri kwa ajili ya ujenzi huo.
Halmashauri za Wilaya ya Mkoa wa Dodoma zitaingizwa kwenye awamu
zinazofuata na fedha pia zitaongezwa.
Nimefurahishwa
na utekelezaji wa mpango wa utoaji chakula cha mchana kwa wanafunzi
mashuleni katika Wilaya za Chamwino, Bahi, Kondoa, Mpwapwa na Chemba.
Huu ni mpango unaofadhiliwa na Shirika la Chakula Duniani (WFP). Hapa
nchini Mpango wa Chakula wa WFP za Mikoa 4 ya Dodoma, Singida, Arusha na
Manyara. Jumla ya shule 640 za mikoa hiyo zinafaidika na mpango huu upo
katika Wilaya 16. Ni mpango mzuri ambao manufaa yake ni kuwaongezea
watoto mazingira mazuri ya kufuatilia na kuelewa masomo. Hivyo,
tuusimamie vizuri ufanikiwe. Ni vizuri viongozi wa Mkoa na kila
Halmashauri mkajipanga vizuri ili mpango huu mzuri uweze kuwepo kila
Wilaya na uweze kuendelea punde WFP watakapoacha kugharamia mpango huo.
Maana jukumu la kuhakikisha lishe ya watoto wetu ni letu wenyewe.
Mkoa
wenu unakabiliwa na tatizo kubwa sana la watoto wanaoanza darasa la
kwanza kutomaliza darasa la saba na wanaoanza kidato cha kwanza
kutomaliza kidato cha nne. Tatizo hili lipo katika kila Wilaya. Takwimu
za Mkoa zinaonesha kuwa kati ya wanafunzi 54,301 waliosajiliwa darasa la
kwanza mwaka 2007, ni wanafunzi 39,387 tu ndiyo walifanya mtihani wa
kuhitimu darasa la saba mwaka 2013. Hii ina maana kuwa wanafunzi 14,914
hawakufanya mtihani ambao ni sawa na asilimia 27.5. Na kwa upande wa
sekondari, kati ya wanafunzi 16,023 walioandikishwa kidato cha kwanza
mwaka 2010, ni wanafunzi 12,693 ndiyo waliofanya mtihani mwaka 2013.
Wanafunzi 3,330 hawakufanya mtihani huo, sawa naasilimia 21. Idadi hii
ni kubwa mno, haikubaliki. Haiwezi kuachwa kuendelea lazima ikomeshwe.
Narudia
kusisitiza agizo langu nililotoa mwezi uliopita kwamba, kuanzia sasa
Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule ni lazima watoe taarifa za mahudhurio ya
wanafunzi kwa Maafisa Elimu wa Wilaya kila miezi mitatu. Maafisa Elimu
wa Wilaya nao watalazimika kutoa taarifa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri
ambae nae atawasilisha kwenye vikao vya Baraza la Madiwani la
Halmashauri mwezi mmoja baada ya kupokea taarifa hizo. Halmashauri
hazina budi kuchukua hatua stahiki, kijamii na kisheria, kuhakikisha
kuwa watoro wanarudi shuleni. Wazazi wa watoto hao au mtu ye yote
atakayebainika kuhusika na utoro huo abanwe ipasavyo.
Maji
Kama
mjuavyo, kuwapatia wananchi wa Tanzania maji safi na salama karibu na
wanapoishi ni moja ya malengo ya msingi ya Sera na shughuli za serikali
na Chama tawala. Katika ziara yangu nimeshuhudia utekelezaji wake.
Nimeweka mawe ya msingi ya ujenzi wa miradi ya maji na nimezindua miradi
ya maji iliyokamilika. Jitihada zetu hizo zimetuwezesha kuwapatia maji
asilimia 75.4 ya wakazi wa Mijini naasilimia 50.6 ya wakazi wa vijijini
mkoani Dodoma. Lengo la kitaifa ni kuwapatia maji asilimia 90 ya wakazi
wa mijini na asilimia 65 ya wakazi wa vijijini ifikapo 2015.
Kwa
hapa Dodoma kiwango hicho cha upatikanaji maji kina maana ya kufanya
kazi ya ziada ili kuweza kufikia lengo. Miradi inayoendelea kutekelezwa
sasa mijini na vijijini hapa Mkoani itakapokamilika itawezesha kufikia
lengo. Rai yangu kwa viongozi ni kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo
ikamilike kwa wakati ili wananchi wapate maji safi na salama mapema.
Vile
vile, nawaomba kusimamia na kuwaelimisha wananchi juu ya utunzaji wa
vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla wake. Viongozi, waache
kulalamika juu ya uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji. Sheria
zipo, mamlaka mnayo chukueni hatua ili kulinusuru taifa letu dhidi ya
uharibifu wa mazingira.
Umeme
Tumeongeza,
maradufu, juhudi za kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme nchini.
Shabaha yetu ni kuwawezesha asilimia 30 ya Watanznaia waweze kupata
umeme ifikapo mwaka 2015. Tayari tumeshavuka lengo hilo kwa kufikia
asilimia 36. Kwa Mkoa wa Dodoma katika mwaka huu wa fedhashilingi
bilioni 43.8 zimetengwa kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini. Fedha
hizi zitawezesha zaidi yavijiji 193 kupatiwa umeme katika Mkoa huu. Kila
Wilaya niliyoitembelea kuna miradi kadhaa ya umeme inayoendelea
kutekelezwa. Ndugu zetu Wilaya ya Bahi walinilalamikia kuwa wao wamepewa
vijiji vinne tu. Nikawasiliana na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo ambae ameahidi kuwa watafanya masahihisho stahiki.
Maombi yangu kwa viongozi wenzangu wahimizeni wananchi waunganishe umeme
majumbani na kwenye shughuli zao za kiuchumi na kibiashara.
Barabara
Ujenzi
wa miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, umeme na
simu ni mambo tuliyoyapa kipaumbele cha juu. Nilisema hivyo katika
hotuba yangu ya kwanza tarehe 30 Desemba, 2005 na kurudia katika kupindi
chote cha uongozi wangu mpaka sasa. Kwa upande wa barabara lengo letu
ni kuunganisha mikoa yote kwa barabara za lami na kuimarisha baraba za
mikoa, wilaya na Vijiji ziweze kupitika wakati wote. Katika ziara yangu
ya Mkoa wa Dodoma nimeshuhudia mafanikio makubwa ya utekelezaji wa lengo
hilo. Nimeweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya lami kutoka
Mayamaya hadi Bonga. Hali kadhalika, nilizindua kukamilika kwa ujenzi wa
barabara ya lami kutoka Dodoma hadi Fufu. Nimeambiwa kuwa zimebaki
kilometa 25 kwa upande wa Fufu hadi Iringa ili kukamilisha ujenzi wa
barabara yote ya Iringa hadi Dodoma yenye urefu wa kilometa 260 kwa
kiwango cha lami. Bila ya shaka mtakubaliana name kuwa ujenzi wa
barabara ya Dodoma – Babati unatoa fursa ya iana yake kwa maendeleo ya
mji wa Dodoma na Mkoa huu kwa jumla. Jipangeni kuitumia fursa hiyo.
Kule
Kongwa niliweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya lami kutoka
Mbande, Kongwa hadi Mpwapwa na Kibakwe. Napenda kurudia kuwatoa hofu
ndugu zangu wa Mpwapwa na Kibakwe kuwa ujenzi wa barabara ile unaendelea
na ndiyo maana pale njia panda ya Kongwa tulifanya shughuli za kuweka
jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Mbande, Kongwa, Mpwapwana siyo
uzinduzi wa barabara ya lami kutoka pale hadi Kongwa.
Nimefarijika
sana kuona jinsi barabara za mkoa na Wilaya zikiendelea kuimarishwa.
Kwa kweli ilikuwa jambo la faraja kubwa kwangu kusikia kuwa vijiji vyote
vya mkoani vinafikika kwa barabara. Ni ushindi mkubwa. Napenda
kuwaahidi kuwa tutaendelea kuwapatia fedha kutoka Mfuko wa Barabara ili
mzidi kuziimarisha barabara zenu. Bahati nzuri Mfuko huo tumeuongezea
sana uwezo wake kutoka shilingi bilioni 56.1 mwaka 2005/2006 hadi
shilingi bilioni 751.7 hivi sasa.
Tulipokuwa
wilayani Mpwapwa niliweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja jipya la
Gulwe linalounganisha majimbo ya mpwapwa na Gulwe. Tulipokuwepo pale
palijitokeza mawazo mazuri kuhusu namna ya kuikinga reli ya kati ambayo
imekuwa inaharibiwa mara kwa mara wakati wa mvua katika maeneo ya
Godegode, Gulwe, Msagali na Kilosa. Ulitolewa ushauri kwamba kama
yakijengwa mabwawa katika mito inayovuka reli hiyo katika maeneo hayo.
Mabwawa hayo yatapunguza wingi na kasi ya maji hivyo kuinusuru reli.
Nilivutiwa na mawazo hayo na kuufikisha ujumbe kwa Waziri wa Uchukuzu
Mheshimiwa Harrison Mwakyembe ambaye aliniambia kuwa ni jambo
linalofanyiwa kazi. Nilizungumza pia na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo
Pinda asimamie kuhakikisha kuwa jambo hili muhimu linafanyika.
Tulikubaliana kuwa Wizara ya Maji, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya
Kilimo, Chakula na Ushirika nao washiriki katika mpango huu kwani ni
wadau muhimu wa mabwawa hayo. Hali kadhalika viongozi wa Mikoa ya
Morogoro, Dodoma na Manyara wahusike.
Natambua
kuwepo maombi ya kutaka barabara kadhaa za Wilaya ziwe za mkoa ili
zisimamiwe na TANROADS. Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa John Magufuli
amesikia na zipo baadhi ambazo amezitolea majibu ya kukubali na nyingine
anaendelea kutafakari nini afanye. Bila ya kuingilia atakachoamua
napenda kusisitiza kuwa msingi mkuu unaoifanya barabara kuwa ya mkoa na
hivyo kushughulikiwa na TANROADS ni kuunganisha Wilaya moja na nyingine.
Barabara inayoanzia na kuishia ndani ya Wilaya haina sifa hiyo hata
kama ni ndefu kiasi gani. Nalisema hili kwa sababu umeanza kuzuka mtindo
wa Halmashauri kutaka kukwepa wajibu wao. Pale ambapo wamezidiwa ujuzi
na uwezo waseme TANROADS itawasaidia lakini wasikwepe majukumu yao.
Kilimo na Mifugo
Masoko ya Mazao ya Kilimo
Viongozi, Wazee wangu na Ndugu Wananchi;
Hongereni
kwa mafanikio mliyopata mwaka huu katika kilimo. Mkoa umezalisha tani
687,122 za mazao ya chakula wakati mahitaji yenu ni tani 494,331.
Hivyokuna ziada ya tani 192,791. Hiki ni kielelezo tosha kwamba juhudi
zenu za kuleta mageuzi ya kilimo zinafanikiwa. Mkoa wenu una zaidi ya
matrekta makubwa na madogo 1,756. Kati ya matrekta hayo Wilaya ya Kongwa
ina matrekta 728. Hongereni sana na endeleeni kuongeza matumizi ya zana
bora na pembejeo za kisasa za kilimo mpate mafanikio makubwa zaidi.
Nilipoingia
mkoa huu kutokea mkoa wa Morogoro kilio kikubwa cha wakulima kilikuwa
soko la mahindi kwa maana ya kukosekana mnunuzi anayetoa bei nzuri kwa
wakulima. Wapo watu binafsi wanaonunua mahindi ya wakulima kwa bei ndogo
sana. Kilio hicho nilikikuta Mkoa wa Morogoro na Tanga kabla ya hapo.
Nilizungumza na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Mheshimiwa
Mhandisi Chiza kuhusu jambo hilo. Akamtuma Katibu Mkuu Mama Sofia Kaduma
na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula Ndugu Walwa
waje kujiunga na msafara. Ndugu Walwa alieleza kuwa walichelewa kuanza
ununuzi katika ukanda wa kati lakini sasa wako tayari kufanya hivyo. Ni
matumaini yangu kuwa hatua hiyo italeta nafuu kwa wakulima. Naomba
tufanye kazi kwa karibu na NFRA tuwasaidie panapobidi ili wafanikishe
jukumu lao. Ni jambo lenye maslahi kwa wakulima, kwa Wakala na Taifa kwa
jumla.
Migogoro ya Wakulima na Wafugaji
Wazee wangu;
Nilipokuwa
Kibaigwa, Kongwa nilipokea malalamiko yenye mvumo mkubwa kutoka kwa
ndugu zetu wanaofanya shughuli za kilimo katika Wilaya ya Kiteto.
Wanalalamikia kufukuzwa, kupigwa, kuuawa, kuchomewa moto nyumba, matreka
na kuporwa na kunyang’anywa mali zao na ndugu wa jamii ya wafugaji.
Wapo waliokuwa wanadai kuwa walikuwa wanaishi huko kwa zaidi ya miaka
thelathini hivyo kujikuta wanaambiwa ondoka, nyumba zinachomwa moto,
mali zinaharibiwa ni mambo magumu sana kuelewa. Nilipokuwa Mkoa wa
Morogoro nilipokea malalamiko kutoka kwa wakulima dhidi ya wafugaji
kwamba mifugo imekuwa mingi mno kupita kiasi na kwamba wanaharibu mazao
ya wakulima.
Nilipokuwa Morogoro nilisema mambo
ambayo ningependa kuyarudia tena leo. Kwanza, kwamba, ardhi
hainongezeki lakini watu wanaongezeka na shughuli zinazohitaji kutumia
ardhi zinaongezeka. Kwa sababu hiyo wanadamu hawataweza kufanya kila
kitu anachotaka katika ardhi hiyo hiyo aliyonayo. Hivyo analazimika
kupanga matumizi bora ya ardhi. Yaani anatakiwa kupanga atafanya nini,
wapi katika ardhi yake. Kwa ajili hiyo nimewataka viongozi wa vijiji,
Wilaya na Mkoa kuwa na mpango wa matumizi ya ardhi kwa shughuli
mbalimbali katika maeneo yao ya uongozi. Kwa upande wa ardhi inayotengwa
kwa ufugaji hawana budi kujua ina uwezo wa kubeba mifugo mingapi na ya
aina gani. Mgao huo ukishafanywa lazima usimamiwe kwa dhati. Ikifanyika
hivyo mtakuwa na hakika na kila hatua ya maendeleo inayochukuliwa na
kuepusha migogoro kati ya wakulima na wafugaji. Hapatakuwa na migogoro
kwa sababu kila mmoja atakuwa na eneo lake la kutosha kufanyia shughuli
zake. Pia hapatakuwa na migogoro kwa vile baada ya ukomo wa uwezo wa
mifugo inayoweza kubebwa na ardhi iliyotengwa kujulikana na kuzuia
mifugo zaidi isiruhusiwe kuingia.
Najua wakati
mwingine wenye mifugo wakiambiwa hivyo wanaona wanabaguliwa na kunyimwa
haki yao kama raia. Si hivyo, hawajanyimwa haki ya uraia ya kuishi po
pote upendapo. Kilichofanyika ni kuweka utaratibu mzuri wa raia kutumia
haki yake hiyo kwa manufaa yake na jamii yote. Inampa fursa za uhakika
kustawisha mifugo yake na kumuepusha na ugomvi na wengine.
Jambo
la pili, nililolisisitiza kule Morogoro ambalo napenda kulirudia tena
hapa leo ni kuwa ndugu zetu wanaofuga wahakikishe kuwa mifugo yao haili
mazao ya wakulima. Kwa kweli jambo kubwa linalozua chuki, uadui na
ugomvi baina ya wakulima na wafugaji ni mifugo kula mazao ya wakulima
shambani. Kama hili halitokei sioni mazingira ya kuwepo mgogoro kati ya
wakulima na wafugaji. Kila mmoja ataendelea na shughuli zake na kuwa
rafiki wa mwenzake. Nilipokuwa Morogoro niliwaomba wafugaji wapitishe
azimio kuwa mwaka huu hakuna hata robo eka ya shamba itakayoliwa na
kuteketezwa. Ikiwa hivyo, sidhani kama kutakuwa na mgogoro kati ya
wakulima na wafugaji.
Kuhusu yaliyotokea Kiteto
kati ya wakulima na wafugaji nalo ni suala la uhusiano na uongozi. Kama
watu wameishi huko na kufanya shughuli zao kwa zaidi ya miaka 30 kuna
namna bora zaidi za wao kuondoka au kuwaondoa. Viongozi wanayodhamana
kubwa ya kuona kuwa watu wa nchi hii hawafanyiwi vile. Nimezungumza na
Waziri Mkuu ili tuangalie uwezekano wa mkutano kati ya viongozi wa Mikoa
yaManyara, Morogoro na Dodoma inayojumuisha Wilaya za Mpakani wakutane
na kuzungumza namna ya kuondoa uadui na kuwafanya watu waishi pamoja na
kushirikiana.
Afya
Nawapongeza
kwa hatua kubwa mliyopiga katika kuboresha sekta ya afya kwa kupeleka
huduma karibu zaidi na wananchi. Mkoa wa Dodoma una mtandao wa hospitali
8, vituo vya afya 41 na zahanati 316. Nafurahishwa pia na jitihada za
kuwashirikisha wananchi katika ujenzi wa zahanati na vituo vya afya
vipya ili kutimiza azma yetu ya kusogeza huduma za afya ndani ya eneo la
mzingo wa kilometa 5wanapoishi wananchi.
Huko
nyuma niliagiza kwamba kila Halmashauri ya Manispaa, Mji na Jiji ambayo
iko Makao Makuu ya Mkoa, ijenge hospitali yake ili kuiwezesha hospitali
ya Mkoa kufanya shughuli za rufaa za Mkoa. Manispaa ya Dodoma mko nyuma
katika kutekeleza agizo langu hili. Tengeni eneo la ujenzi wa hospitali
ya Manispaa na wekeni kwenye bajeti yenu ili tuijenge.
Pia
upo wajibu wa kisera kuhakikisha kuwa kila Wilaya ina hospitali ya
Wilaya. Katika Mkoa wa Dodoma Wilaya za Kongwa, Bahi, Chamwino, Chemba
na Dodoma Mjini hazina hospitali za Wilaya. Nimewataka waanze ujenzi wa
hospitali hizo. Waweke mahitaji yao kwenye mipango ya maendeleo ili
itafutiwe fedha.
Nawapongeza kwa jitihada
mnazofanya za kuhamasisha akina mama kujifungua katika zahanati, vituo
vya afya na hospitali. Taarifa yenu inaonesha kwamba asilimia 79 ya
akina mama wajawazito wanajifungulia katika vituo vya kisasa vya kutoa
huduma ya afya na chanjo ya watoto mmefikisha asilimia 96. Msibweteke
ongezeni uhamasishaji ili akina mama wote wajifungulie kwenye vituo vya
afya na watoto wote wapate chanjo. Kwa ajili hiyo, napenda kushauri kuwa
ujenzi wa sehemu ya akina mama wajawazito kusubiria kabla ya kujifungua
(maternity waiting homes) ufikirieni kwa uzito unaostahili. Wenzenu wa
Morogoro wamelifanya kuwa sehemu ya mipango yao ya kuendeleza afya ya
akina mama wajawazito. Inasaidia kuokoa maisha ya mama wajawazito
kunaweza kusaidia Mkoa huu pia na kwingineko nchini.
Aidha,
tuendelee kuhimiza mapambano dhidi ya ugonjwa ya UKIMWI katika maeneo
yetu. Japo takwimu zinaonyesha kuwa maambukizi ya UKIMWI kimkoa
yanapungua toka asilimia 3.4 mwaka 2008 hadi asilimia 2.9 mwaka 2012,
lengo letu ni kutokuwa na maambukizi mapya kabisa. Ongezeni juhudi ili
lengo letu hilo tulifikie.
Nawapongeza pia kwa
kuvuka lengo letu la kuhakikisha kwamba asilimia 30 ya Watanzania
wanajiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii ifikapo 2015. Ninyi
mmekwishafikisha asilimia 47.9. Hata hivyo, ziko Wilaya kama za Kondoa,
Chemba na Manispaa ya Dodoma ambazo ziko chini sana. Ongezeni jitihada
ili wananchi wengi zaidi wapate huduma ya mfuko huo.
Ugonjwa wa Ebola
Ndugu wananchi;
Tangu
mwezi Aprili, 2014 nchi za Afrika Magharibi hususan nchi ya Guinea,
Siera Leone, Liberia na Nigeria zimekumbwa na mlipuko mkubwa wa ugonjwa
hatari wa Ebola. Taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha
kuwa tayari watu 3,500 wameambukizwa na tayari zaidi ya vifo 1,900
vimetokea. Asilimia 40 ya vifo hivi vimetokea ndani ya wiki tatu hadi
kufikia tarehe 3 Septemba, 2014. Ebola ndiyo virusi hatari zaidi duniani
kuliko hata UKIMWI. Ndiyo maana Shirika la Afya Duniani limeutangaza
ugonjwa huu kuwa ni janga la dunia, na inatarajiwa athari zake zinaweza
kuongezeka. Ugonjwa huu husababishwa na virusi vya Ebola na husababisha
wagonjwa wengi kufa kwa vile ugonjwa huu hauna tiba maalum wala chanjo.
Wataalam
wanatuambia kwamba virusi vya Ebola hubebwa na ndege aina ya popo na
wanadamu huupata kupitia kwa wanyama walioambukizwa kwa kuwagusa au
kuwala. Wanyama hao ni pamoja na sokwe, nyani na swala. Maambukizi
kutoka kwa mgonjwa huenda kwa mtu mwingine kwa kugusa damu au majimaji
kutoka mwilini mwa mtu aliyeambukizwa ugonjwa huo au kwa kugusa maiti ya
mtu aliyekufa kutokana na ugonjwa huo. Ugonjwa huu ni hatari sana kiasi
kwamba hata watoa huduma za afya kama madaktari na wauguzi kama
hawakuchukua tahadhari zinazotakiwa wanaweza kuambukizwa na hata kufa.
Mpaka hivi sasa Daktari mmoja aliyekuwa anawahudumia wagonjwa wa Ebola
kule Liberia amekufa.
Dalili za ugonjwa huo ni
pamoja na mgonjwa kuwa na homa kali ya ghafla, kulegea mwili, kuumwa na
kichwa, kuumwa na misuli na kutokwa na vidonda kooni. Dalili hizi
zinaweza kuambatana na kutapika, kuharisha, kutokwa na vipele, kutokwa
na damu ndani na nje ya mwili na kushindwa kufanya kazi kwa figo na ini.
Dalili za ugonjwa huu hujitokeza katika siku 2 hadi 21 baada ya
kuambukizwa.
Tunamshukuru Mungu kwani mpaka
sasa hapa nchini hajapatikana mtu yeyote mwenye ugonjwa huu. Pamekuwepo
na wagonjwa wanne waliohisiwa kuwa na Ebola ambao uchunguzi ulionesha
hawakuwa na ugonjwa huo. Watatu kati ya wagonwja hao walikuwa ni
wagonjwa wa malaria na mmojauchunguzi wake bado unaendelea. Wagonjwa
wawili ni kutoka Dar es Salaam na wawili ni kutoka Geita na Nkasi.
Wagonjwa hawa waliohisiwa walihudumiwa na walifanyiwa uchunguzi kwa
kufuata tahadhari zote za ugonjwa wa Ebola. Hii imeonesha utayari wetu
wa kukabiliana na janga hili. Pamoja na kutokuwepo kwa mgonjwa yeyote
aliyehisiwa au kuthibitika kuwa na ugonjwa huu.
Tumejipanga
vizuri kuzuia ugonjwa huu usiingie nchini. Tumechukua tahadhari na
kujiandaa vilivyo kukabiliana na janga hili kwa kuchukua hatua
zifuatazo:
(i) Tunacho Kikosi Kazi cha Taifa kinachoongozwa na
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Donald Mbando cha kukabiliana na ugonjwa
huu katika ngazi ya taifa hadi Wilaya.
(ii)Tumekamilisha
mpango wa kitaifa “Ebola Contingency Plan” na tumetenga Shilingi milioni
500ikiwa ni fedha za awali za utekelezaji wa mkakati huo.
(iii)Tumeshaagiza Timu za Maafa za mikoa na wilaya kutekeleza mpango huo.
(iv)Tumesambaza
vifaa “personal protective equipment” kwa watumishi wa afya katika
mikoa yote, wilaya zote, hospitali zote za Rufaa na kanda 37, viwanja
vya ndege vya Julius Nyerere, Kilimanjaro, Mwanza na Zanzibar.
Tumesambaza pia dawa.
(v)Tumetenga kituo maalum tengefu (isolation unit) cha Wilaya ya Temeke na vituo vingine tengefu mikoani.
(vi)
Tumechukua tahadhari kubwa kwenye viwanja vya ndege. Tumekwishafunga
mitambo maalum ya vipima joto na dalili za wagonjwa wa Ebola katika
viwanja vya Mwalimju Nyerere (2), Mwanza (1), Zanzibar (1) na kituo cha
Namanga (1). Tumeagiza pia scanners 5 ambazo zimekwishawasili na
zitafungwa katika viwanja vyetu.
(vii)Tumetoa mafunzo kwa
watumishi wa afya wa mipakani na viwanja vya ndege. Tumetoa mafunzo hayo
kwa watumishi 100 wa Dar es Salaam na 45kutoka mikoa ya Arusha, Kagera,
Rukwa, Mwanza, Kilimanjaro, Kigoma na Zanzibar. Tumepeleka watumishi
watatu nchini Jamhuri ya Kongo kupata mafunzo maalum.
(viii)Tumeanza
maandalizi ya kuboresha maabara zetu ili tuweze kufanya uchunguzi wa
sampuli hapa hapa nchini. Kwa sasa, eneo zima la Afrika Mashariki
tunategemea na tunatumia maabara ya Nairobi.
Viongozi wa ngazi
zote hizi wamepatiwa mwongozo wa utekelezaji. Tunachoomba ni
ushirikiano wa wananchi wote katika kuchukua tahadhari na kutoa taarifa
mapema iwezekanavyo mara tu mnapogundua dalili za ugonjwa huu kwa mtu ye
yote.
Mchakato wa Katiba
Nilipozungumza
na Taifa mwishoni mwa mwezi Julai, nilizungumzia mchakato wa Katiba.
Nilielezea utayari wangu wa kufanya kila liwezekanalo kusaidia
kufanikisha mchakato wa Katiba unaonndelea sasa. Kwa moyo huo, sikusita,
nilipoombwa na Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia (Umoja wa Vyama
vyenye Uwakilishi Bungeni) Mhe. John Momose Cheyo kukutana nao na
kufanya mazungumzo ya mashauriano. Kama mnavyojua tulikutana tarehe 31
Agosti, 2014 Mjini Dodoma. Tumekuwa na mazungumzo mazuri. Tumepeana kazi
ya kufanya na tumekubaliana kukutana tena tarehe 08 Septemba, 2014
kuendelea na mazungumzo yetu. Kinachotia moyo ni ule ukweli kwamba kila
upande umeonesha kiu na utayari wa kuzungumza. Tuyape nafasi mazungumzo
haya yatutoe hapa tulipo na kutusogeza mbele kwa umoja na mshikamano.
CDA
Mwisho,
suala la CDA: Wakati wa kuzindua barabara ya Dodoma – Fufu Mbunge wa
Dodoma Mheshimiwa Malole alielezea kwa uchungu matatizo ya CDA.
Nimewaagiza Wadau wakae tutakutana tarehe 07 Septemba, 2014 tupokee
ushauri. Naomba muwe na subira.
Hitimisho
Wazee wangu;
Narudia
tena kuwashukuru ndugu zangu wa Dodoma kwa mapokezi mazuri na ratiba
nzuri iliyonipa nafasi ya kujifunza mengi kuhusu mkoa wenu. Naondoka
nikiwa na kumbukumbu ya mambo mazuri yanayoendelea kufanyika hapa mkoani
kuinua hali za maisha ya wananchi. Tafadhali ongezeni bidii. Mimi na
wenzangu Serikalini tutaendelea kuwaunga mkono.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment