Pages

Pages

Pages

Thursday 4 September 2014

CCM YAPANGUA MAKATIBU WAKUU 16


Na Thobias Mwanakatwe, Dar es Salaam

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewahamisha  makatibu wake wa mikoa 16 kutoka katika vituo vyao vya kazi na mwingine  kupewa likizo ya miezi miwili. Uhamisho huo umesainiwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Septemba 1 mwaka huu.

Vyanzo vya habari kutoka ndani ya chama hicho vimebainisha kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Itikadi na Uenenzi, Nape Nnauye, alipelekewa jalada namba CMMM/OKM/M.11/Vol.7/1/ ya ukurasa wa 106 na Katibu Mkuu wa chama hicho kujulishwa kuhusu uhamisho wa makatibu hao.

Makatibu hao waliohamishwa  ni Joyce Masunga kutoka mkoa wa Mwanza kwenda  Pwani, Alphonce Kinamhala kutoka Katavi kwenda Arusha, Janeth Kayanda kutoka Bukoba Mjini kwenda Tabora na Gustav Muba kutoka Tanga kwenda Geita.

Wengine ni Katibu wa CCM  Pwani, Sauda Mpambalyoto ambaye anakwenda Kusini Unguja, Mary Chatanda kutoka Arusha kwenda Singida, Evelyne Mushi kutoka Kagera kwenda Katavi, Naomi Kapambala kutoka Singida kwenda  Kigoma.

 Idd Ame kutoka Tabora kwenda Kagera, Shija Othman Shija kutoka Kusini Pemba kwenda Tanga, Mwangi R. Kundya kutoka Mjini kwenda Mbeya, Mohamed Nyawenga anahamishiwa Mjini kutoka Kigoma, Adamu Ngalawa kutoka Shinyanga kwenda Mara.

Maganga Sengelema kutoka Mbeya kwenda Shinyanga, Mary Maziku kutoka  Geita kwenda Dodoma na Bernard Nduta kutoka Dodoma kwenda Mwanza.
Aidha, Zainab Shomari aliyekuwa Katibu wa  CCM mkoa wa Kusini Unguja,  amepewa likizo ya miezi miwili.

Hata hivyo, uhamisho wa Mary Chatanda aliyekuwa Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha umeelezwa kwamba huenda umetokana na yeye kudaiwa kujihusisha na vurugu zilizotokea jijini Arusha wakati wa uchaguzi wa Meya wa jiji hilo.

Uhamisho huo pia umezua maswali mengi kutoka kwa wanachama, mashabiki na wapenzi wa chama hicho wakihoji inakuwaje ufanyike katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa baadaye mwaka huu na mkuu mwaka 2015.

Kinana alipotafutwa kuelezea sababu za makatibu hao kuhamishwa simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno (sms) hakujibu.

Vilevile  Nnauye, alipotafutwa,  simu yake ilikuwa ikiita tu bila kupokelewa na alipotumiwa sms hakujibu.
CHANZO: NIPASHE     

No comments:

Post a Comment