Pages

Pages

Pages

Sunday 17 August 2014

WAZEE DAR WAWATAKA UKAWA WARUDI BUNGENI

Mzee Alhaji Sheikh Bakari Chiwaka (kulia) akisisitiza umuhimu wa maridhiano katika mchakato wa Katiba Mpya na kuwa Katiba bora itapatikana kwa uongozi bora na wa kidemokrasia nchini. Kushoto ni Kepteni Mstaafu Alhaji Mohamed Ligora.
WAZEE 05Kepteni Mstaafu Alhaji Mohamed Ligora akisisitiza (katikati) umuhimu wa kupata Katiba bora ya nchi wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam. Kushoto ni Mzee Sheikh Yahaya Ngoma na kulia ni Mzee Alhaji Sheikh Bakari Chiwaka. (Picha zote na Eleuteri Mangi-MAELEZO)
 
 Na Immaculate Makilika –MAELEZO_DAR ES SALAAM
WAZEE  wa Mkoa wa Dar es salaam wamewaomba Umoja wa Katiba wa Wananchi (UKAWA) kurudi Bungeni ili kuendelea na mchakato wa majadiliano ya Rasimu ya Katiba Mpya yanayoendelea.
Wazee hao wamesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wakizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya siasa nchini pamoja na Bunge la Katiba Mpya linaloendelea mjini Dodoma.
Akizungumza kwa niaba ya  Wazee wenzake  Kepteni Mstaafu Alhaji Mohamedi Ligora , amesema kuwa Tanzania ni nchi nzuri na watu wake ni wazuri ni vema  UKAWA na wenzao  wakarudi Bungeni kujadiliana ili watimize matakwa ya kidemokrasia.
Amesema kuwa wananchi wa Tanzania hawataki kufananishwa  na nchi zingine zilizofanya makosa na kupata matatizo kutokana na mambo kama haya ambayo yalisababisha wananchi wao kuzikimbia nchi zao kwa mambo ambayo wangeweza kukaa chini na kumaliza wenyewe kwa ajili ya maslahi ya umma.
Kapteni Mstaafu Alhaji  Ligora amesema kuwa suala la mchakato ni suala la kidemokrasia, hivyo ni vyema  UKAWA wakatumia fursa hiyo waliyonayo kwa kurudi Bungeni na kuendelea na majadiliano kuhusu Rasimu ya Katiba hali itakayosaidia kupatikana kwa Katiba Mpya ambayo itakuwa na manufaa kwa wananchi wa Tanzania.
Aidha, amewaomba wajumbe walio Bungeni na wale walio nje ya Bunge kuacha kuwazomea UKAWA badala yake wawasihi warudi katika chombo rasmi cha kuboresha Rasimu ya Katiba Mpya.
 Naye Mzee Ali Bakari Muki, amewataka UKAWA kuheshimu misingi ya demokrasia lakini pia amewapongeza wabunge walioitikia wito wa  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kurudi Bungeni na kuendelea na majadiliano kuhusu Katiba kwani ndio Jukwaa pekee la kuwapatia wananchi Katiba bora.
Kwa upande wake  Mzee  Yahaya  Ngoma amewataka viongozi wote hasa UKAWA kuheshimu na kudumisha jitihada zilizofanywa na  waasisi wa Taifa hili akiwemo Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere pamoja na Sheikh Abeid Amani Karume kwa kuzingatia misingi na kanuni za uongozi bora kwa kutumia  njia ya majadiliano pale panapokuwa na mawazo tofauti baina yao.
Halikadhalika, Alhaji Sheikh Bakari Chikawa  amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuridhia kuanza kwa mchakato wa Katiba Mpya na kusisitiza ni moja ya tunda la uongozi bora na demokrasia nchini.
Aidha, ameongeza kuwa UKAWA ni vema wakatumia fursa hiyo ya demokrasia kwa kuwawakilisha vema wananchi wa Tanzania ili kuhakikisha wanapata Katiba Bora.
Alhaji Chikawa amewaomba  UKAWA kurudi Bungeni kwani kunyume na hivyo ni watakua wametenda dhambi na madhara yake ni makubwa sana, na kusisitiza kuwa mazungumzo ni muhimu na  yakipuuzwa basi kuna madhara.

No comments:

Post a Comment