Pages

Pages

Pages

Thursday 14 August 2014

WAZANZIBARI WAGOMEA UTEUZI WA MGOMBEA MWENZA!


Baada ya kuamua kuleta mageuzi ya vyama vingi vya siasa, ilikuwa lazima kubadili baadhi ya vifungu vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Rais aIiteua Kamati ya kutazama Katiba yetu na kufanya mapendekezo yanayotakiwa. Kamati hiyo iliongozwa na Ndugu Mark Bomani.

Kati ya mapendekezo yake mengi, moja lilihusu Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Kamati ilipendekeza kwamba badala ya utaratibu wa sasa wa kuwa na Makamu wa Rais wawili, Waziri Mkuu wa Serikali ya Muungano na Rais wa Zanzibar, inafaa tuwe na Makamu mmoja tu. Na jinsi ya kumpata Kamati ilipendekeza tufuate utaratibu wa Kimarekani ambayo, mtu aliyeteuliwa na Chama chake kuwa mgombea wa urais, atakuwa na mwenzake wanamwita “Running Mate” na endapo mgombea huyo atachaguliwa na wananchi kuwa rais basi huyo mgombea mwenzake ndiye atakuwa Makamu wa Rais.

Lakini kamati ikapendekeza kwamba kutokana na historia ya nchi yetu, itafaa Chama kikiteua Mgombea urais kutoka upande mmoja wa Muungano, basi kiteue Mgombea mwenza kutoka upande wa pili wa Muungano; na katiba iseme hivyo.

Watu wengi, mimi nikiwa miongoni mwao, waliona kuwa mapendekezo haya ni mazuri. Lakini tukawa tukisikia minong’ono kwamba “Wazanzibari” hawapendi pendekezo hili la kupata Makamu wa Rais kwa njia ya kuwa na Mgombea Mwenza. Wanataka utaratibu wa sasa uendelee, ambapo Rais wa Zanzibar akisha kuchaguliwa anakuwa moja kwa moja Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Utaratibu huu hata sasa una matatizo. Rais wa Zanzibar huchaguliwa na Wazanzibari watupu, ili awe Rais wao; lakini anakuwa pia Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano bila kuchaguliwa na Watanzania wa Bara. Kama Rais wa Jamhuri ya Muungano hayupo kwa sababu yoyote ile, huyu ataweza kushika nafasi yake, kwa mujibu wa Katiba, lakini bila kuchaguliwa na wapiga kura wa Tanzania nzima. Ni dhahiri kwamba utaratibu huu una walakini, na ingawa mpaka sasa haujatuletea matatizo makubwa, ni wazi kwamba hata bila mfumo wa vyama vingi, siku moja tungelazimika kuubadili.

Lakini ni dhahiri zaidi kwamba katika hali ya vyama vingi hatuwezi kuendelea na utaratibu wa sasa. Mkiwa na vyama vingi vya siasa, na Serikali zaidi ya moja, hamna budi mkubali kwamba inawezekana Chama kinachoongoza Serikali ya Muungano kinaweza kisiwe ndicho kinachoongoza Serikali ya Zanzibar.

Kwa hiyo tukibaki na utaratibu wa sasa, ambapo Rais wa Zanzibar anakuwa kwa moja ni Makamu wa Jamhuri ya Muungano tunaweza kujikuta katika hali ambapo Rais wa Jamhuri anatoka katika chama cha upinzani! Na endapo Rais hayupo kwa sababu yoyote huyu anaweza akashika nafasi yake ingawa alikataliwa na wapiga kura katika uchaguzi uliopita!

Mapema mwezi Desemba 1992, Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ilikutana Dodoma kwa ajili ya kuzungumzia suala hili pamoja na mengine. Viongozi wa chama na Serikali Waliniomba nami niende nikatoe maoni yangu. Nikaenda.

Mkutano wa faragha: Tulikuwa na kikao cha faragha cha viongozi wakuu wote wa Chama na Serikali, na wengine wa nyongeza. Mambo yaliyokuwa yametayarishwa yakazungumzwe katika Halmashauri Kuu yalikuwa ni hilo la utararibu wa kuchagua Makamu wa Rais na mengine. Lakini Rais alieleza kuwa walikuwa wamezungumza pia suala la vipindi na muda wa kuwa Rais wa Jamhuri ya Tanzania. Rais alieleza kuwa walikuwa wamekubaliana kwamba vipindi vya kuwa Rais ni lazima vitamkwe, lakini walikuwa hawajafikia uamuzi viwe vingapi - vingapi.

Awali baadhi ya Viongozi wa Chama - walikuwa wameanza kampeni za kutaka Rais Mwinyi aongezewe vipindi vya muda wa kuwa Rais. Nilipotambua hivyo nilikuwa nimekwenda mara moja kwa Rais na kumsihi azizime kampeni hila; na viongozi wahusika nilitafuta nafasi nao nikawaomba wasilifufue jambo hili. Nikadhani tumeelewana hivyo. Kwa hiyo nilishtuka niliposikia kuwa kumbe suala hilo la vipindi vya urais- bado linazungumzwa, na ati bado uamuzi wa vipindi vingapi haujafikiwa! Kwa hiyo nilirudia tena kueleza umuhimu wa kukubali kwamba suala hili tumekwisha kuliamua, na hatari ya kuanza kulizungumza upya.

Sababu ya kufanya muda ambao mtu ye yote anaruhusiwa kuwa Rais utamkwe na uwe ni sehemu ya Katiba ilikuwa ni kuutoa uamuzi huo mikononi mwa Rais mwenyewe, au kikundi cho chote cha Chama au Dola. Si uamuzi mwepesi, kwa Rais wala kwa washauri wake.

Plato, Myunani wa kale, alipendekeza kuwa mafilosofa ndio wanaofaa kuwa watawala wa nchi, maana wana sifa mbili muhimu: kwanza, Wana uwezo wa kutawala, na pili, hawapendi kutawala. Kwa hiyo, Jamhuri ya Plato itakuwa na sheria ya kuwalazimisha mafilosofa kutawala kwa zamu; na mtu zamu yake ya kutawala ikiisha, atafurahi sana kurudia shughuli zake za falsafa ambazo ndizo hasa anazozipenda.

Lakini nchi zetu hazitawaliwi na mafilosofa wa Plato; watawala wetu ni wanasiasa wa kawaida ambao wanapenda sana kutawala hata kama hawana uwezo wa kutawala; na ambao wako tayari hata kuhonga ili wachaguliwe kuwa watawala, na wakisha kuchaguliwa hawatoki bila kulazimishwa. Si busara kuwaachia wao wenyewe ndio wawe waamuzi wa lini waache kuwa watawala.

Lakini hata kwa viongozi wanaotambua kuwa uongozi ni wajibu, na ukisha kutimiza wajibu wako ni vizuri kuondoka, si rahisi kuamua kama wajibu wako ni kuondoka au ni kuendelea. Na sababu za kusita zinaweza zikawa nzuri kabisa. Na katika hali halisi ni vigumu zaidi kwa washauri wa Rais kumwambia kuwa amekwisha kutimiza wajibu wake na kwa maoni yao inafaa aondoke amwachie mtu mwingine. Wao wanazo sababu nyingi zaidi, nzuri na mbaya, za kumtaka aendelee, na watamshauri hivyo. Kwa hiyo ni jambo la busara kabisa uamuzi wa muda wa kuwa Rais ufanywe mara moja, na ukisha kufanywa uwe ni sehemu ya Katiba ya Nchi na uheshimiwe.

Na hivyo ndivyo tulivyofanya. Suala hili lilikwisha kuamuliwa zamani, na sasa ni sehemu ya Katiba yetu uamuzi huo inafaa uheshimiwe. Rais Mwinyi ndiye Rais wa kwanza kuchaguliwa kwa mujibu wa Katiba hiyo. Yeye akisema kuwa vipindi viwili havitoshi na akataka view vitatu; rais wa pili atasema viindi vitatu havitoshi na atataka view vine; na kadhalika na kadhalika mpaka tufiie Ngwazi wa Tanzania. Hilo si jambo la kuzungumzwa, na limefanyiwa uamuzi wa mwisho. Kuhusu suala la utaratibu wa kuchagua Makamu wa Rais, Kamati, Kuu ya CCM ilikuwa imeamua kupendekeza kwa Halmashauri Kuu ya Taifa kwamba tuendelee na utaratibu wa sasa, kama "Wazanzibari" wanavyopendelea! Bila maelezo ya kuridhisha. Katika kutoa maoni yangu nilipendekeza na kusisitiza kuwa tukubali mapendekezo ya Kamati ya Bomani.

Kikao cha Halmashauri Kuu: Nilikuwa sikukusudia, wala niiikuwa sikusudiwi na wale walioniita, kuhudhuria kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa. Nilitumaini kuwa baada ya mazungumzo yetu ya faragha viongozi wetu watapenda kuutazama upya uamuzi wao wa kukataa rnapendekezo ya Kamati ya Bomani.

Lakini nilipoambiwa asubuhi ya, siku ya pili yake kwamba Kamati Kuu itayapeleka rnapendekezo yake katika Halmashauri Kuu vile vile yalivyokuwa, niliomba nipatiwe nafasi nikatoe maoni yangu mbele ya Halmashauri Kuu ya Taifa na kueleza kwa nini naamini kuwa viongozi wetu watafanya makosa wakikataa mapendekezo ya Kamati ya Bomani.

Pamoja na mambo mengine, nilieleza kuwa sehemu moja ya mapendekezo ya Kamati ya Bomani, ile inayosema Mgombea akitoka upande mmoja mwenziwe atoke upande mwingine wa Muungano, inakusudiwa kuisaidia Zanzibar. Maana ukiacha Mwenzi wa Mgombea urais achaguliwe kutoka upande wo wote wa Muungano, uwezekano wa wote wawili, Rais na Makamu, kutoka Tan­zania Bara ni mkubwa sana. Mapendekezo ya Kamati ya Bomani yalikuwa yanahakikisha kwamba mmoja wa viongozi wetu wakuu hao akitoka Bara mwingine atatoka Visiwani. Kwa hiyo ni vigumu sana kuona kwa nini "Wazanzibari" wanapinga utaratibu huu.

Na ukiuliza sababu unaambiwa kuwa ni"nyeti"!.Nikaonya: ikiwa "Wazanzibari" wataendelea na msimamo huu usioeleweka wala kuelezeka, maana ati ni "nyeti", Watanzania Bara wataanza kununa. Nikasema nimeanza kusikia minong’ono ya manung’uniko ‘mitaani’. Nilirudia tena kutoa maoni yangu kuhusu vipindi vya urais.

Baada ya hapo niliondoka nikarudi Butiama. Baadaye niliambiwa kwamba mjadala uliofuata haukuwa mzuri sana; na viongozi wetu badala ya kulizungumzia suala la uchaguzi waziwazi kabisa na kulifanyia uamuzi, waliondoka katika Halmashauri Kuu kwa “janjajanja", wakalipeleka katika Bunge kuomba wapewe muda wa miaka miwili ya kulitafakari! Na Bunge likakubali! Wabunge wakapitisha utaratibu wa kuchagua Rais na kuahirisha utaratibu wa kuchagua Makamu wake mpaka hapo viongozi wetu watakapopata ndoto nzuri zaidi - baada ya miaka miwili!

Baadaye viongozi wetu walinitumia wajumbe kuja kunieleza upya msimamo wa Serikali, na kuniomba nielewe. Nakumbuka vizuri sana mmoja wa wajumbe hao, mtu msema kweli sana, alinikosoa kwa kwenda katika Halmashauri Kuu ya Taifa na kutaja minong'ono ya "mitaani"! Nakumbuka pia kwamba nilisisitiza: Waambieni Viongozi wetu: Tatizo si mimi, tatizo ni "Wazanzibari" na wale wanaounga mkono msimamo wao. Hao ndio wanaofaa kutumiwa ujumbe; mimi ni mwelezaji tu wa tatizo lililopo ikiwa tutaendelea na huu msimamo "nyeti" usiokuwa na maelezo.

Wazee hawa waliendelea kuja kuniona au Msasani au Butiama. Baadaye suala la Zanzibar kuingia katika OIC likazuka. Hili nalo viongozi wetu wakaliombea bungeni, na wakapewa muda wa mwaka mmoja wa kulitafakali! Suala la kuvunja Katiba ya Nchi yetu!


REJEA: NYERERE, J.K.; UONGOZI WETU NA HATMA YA TANZANIA

No comments:

Post a Comment