Mwalimu Julius Nyerere (kushoto) na Sheikh Abeid Amani Karume wakibadilishana Hati za Muungano mwaka 1964
Na Daniel Mbega
WAJUMBE wa Bunge Maalum la Katiba wako Dodoma, wanatumia mabilioni ya
fedha za walipa kodi kwa matarajio ya Watanzania wengi kupata Katiba Mpya.
Hata hivyo, mvutano wa muundo wa serikali ndiyo changamoto kubwa
inayowakabili kiasi cha kushuhudia wajumbe kutoka vyama vya upinzani kuamua
kujitoa na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Tangu walipoondoka katika awamu ya kwanza, mpaka sasa bado wameshikilia
msimamo wao huo kwamba hawatakwenda Bungeni kwa kuwa wanaamini CCM inataka
kuchakachua Rasimu ya Katiba mpya na kupitisha mfumo wa serikali mbili badala
ya tatu kama ilivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na
Jaji Warioba.
Lakini ndani ya msuguano huo, kuna hawa Wazanzibari ambao tangu wakati
wa vuguvugu la kukusanya maoni, walikwishasema kwamba wao wanaitaka Tanganyika
iwepo ndani ya Muungano ili wajue nchi waliyoungana nayo, kwa sababu katika
muungano wa sasa haitajwi kabisa.
Wazanzibari wamekuwa vinara wa kuwasemea Watanganyika katika kuidai
Tanganyika. Lakini wanakwenda mbali kuhusu Muungano ambapo wamependekeza uwe
muungano wa mkataba na siyo kama ulivyo sasa kwa sababu unawaminya wao na
kuwakandamiza. Kwamba hauna ridhaa ya walio wengi.
Ukiingia kwa undani sana unagundua kwamba, kelele zao za kuwapigania
Watanganyika waipate Tanganyika yao – jambo ambalo ni jema kabisa katika
kurejesha utaifa wa Watanganyika – lakini utagundua kwamba kuna mbinu chafu
nyuma yake kwamba mara tu Tanganyika itakapopatikana ama kurejeshwa, basi hoja
yao ya kuukataa muungano itakuwa na nguvu zaidi hasa kwa vile serikali ya
muungano haitakuwa na nguvu zozote zaidi ya kuwasikiliza washirika wa muungano
huo.
Tuseme ukweli kwamba Wazanzibari hawautaki kabisa muungano, bali
wanalazimishwa. Kitendo cha wanaosaidikiwa Waislamu kuchoma makanisa mjini
Unguja kinadhihirisha kwamba upande huo wa Jamhuri ya Tanzania hauutaki kabisa
Muungano, ingawa visingizio vyao ni kwamba, hauwasaidii chochote.
Wazanzibari wanasema Muungano hauwasaidii, lakini kule hakuna mashamba
makubwa ya mchele, mahindi wala viazi, achilia mbali umeme wa uhakika ambao
wanautoa Tanzania Bara wanakodai kwamba kunawakandamiza na kuwanyima uhuru wao.
Lakini Watanganyika wanaung’ang’ania Muungano huo ambao kwa kiasi
kikubwa hauna msaada kwao, pengine kama kuna sababu za kiusalama, kwa sababu
hakuna chochote ambacho Tanzania Bara inakipata kutoka huko.
Wazanzibari wameonyesha dhahiri kwamba wao ni ‘wachoyo’ hasa baada ya
kuwepo kwa tetesi kwamba kuna mafuta huko, wakaona hawawezi kuwagawia na wenzao
wa Bara huku wakisahau kwamba kwa miaka 50 ya Muungano tangu uliposainiwa,
wamekuwa wakinufaika nao.
Lakini kwa upande mwingine, najiuliza bila kupata majibu, kwamba
Watanzania wanawashangaa vipi Wazanzibari wanaposema hawautaki Muungano? Au
inakuwaje Wazanzibari waanze kuchoma makanisa sasa wakidai hawautaki Muungano?
Wazanzibari wanasema kwa kipindi chote hicho wameshindwa kufanya jambo
lolote kwa maendeleo yao kutokana na kivuli cha Muungano na kila wanalotaka
kulifanya lazima wahojiwe.
Watanganyika nao wanasema rasilmali nyingi za Bara zimekuwa
zikiwanufaisha bure Wazanzibari katika kile kinachoonekana kama kujipendekeza
kwa Serikali ya CCM kulinda kwa nguvu ili Muungano usivunjike.
Kilicho dhahiri ni kwamba, Wazanzibari wanawakumbusha tu Watanzania
kwamba wao walikwishauvunja kitambo Muungano ambao muasisi wake Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere aliupigania kwa juhudi hadi mauti yalipomfika.
Kimantiki, Wazanzibari waliuvunja Muungano huu mwaka 1992, wakati
walipoamua kujiunga na Shirikisho la Nchi za Kiislamu Duniani (Organization of
Islamic Countries - OIC). Hapa ndipo hasa 'Chunusi' wa Muungano alipoingia.
SUALA LA UTAIFA:
Tangu mwaka 1992 katika jaribio la Dk. Salmin Amour Juma kuiongoza
Zanzibar kujiunga na OIC, ilionekana dhahiri lengo la SMZ lilikuwa kuifanya
Zanzibar Taifa la Kiislam wakati alifahamu suala kama hilo lilipaswa kuingizwa
kwenye Muungano na kujadiliwa kabla ya kuchukua uamuzi mzito kama huo.
Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi, hasa kutoka Tanzania Bara, waliona
wamesalitiwa na kiongozi huyo wa Zanzibar ambaye pia kikatiba, ndiye Makamu
Mwenyekiti wa chama kwa upande wa Visiwani na alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano.
Lakini uamuzi huo ukawa umewasha moto kwa Wabunge wa CCM kutoka Bara,
ambao waliona kuwepo kwa serikali mbili ndani ya Muungano kulikuwa kunawapa
kiburi Wazanzibari kiasi cha kufanya lolote wanalotaka bila kusubiri baraka za
upande mwingine.
Haikushangaza wakati wa Kikao cha Bunge la Bajeti la mwaka 1993,
aliyekuwa Mbunge wa Chunya, Njelu Kasaka, alipowasilisha hoja binafsi kudai Serikali
ya Tanganyika ndani ya Muungano ili kutoa uwiano sawa.
Tuliokuwepo wakati huo tuliuona mjadala huo pale Karimjee jinsi
ulivyopamba moto na kushuhudia Wabunge 55 wa Bara (maarufu kama G55) wakiunga
mkono kuwepo kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano.
Wabunge hao na Watanzania wa Bara walikuwa na haki ya kulizungumza
hilo, ingawa muasisi wa Muungano, Mwalimu Nyerere, aliingilia kati na kuwaita Waziri
Mkuu wa wakati huo, John Malecela, na Katibu Mkuu wa CCM wa wakati huo, Horace
Kolimba, kwamba ni wahuni na walevi. Hakuishia hapo, ndipo akaamua kutunga
kitabu cha ‘Uongozi Wetu na Hatma ya Tanzania’.
Leo hii nitashangaa ikiwa wale waliokuwa wanaiunga mkono hoja ya
Tanganyika ndani ya Muungano kama wataikana, ingawa mtoa hoja, Njelu Kasaka,
hataki kabisa kuulizwa swali lolote kuhusiana na Serikali ya Tanganyika.
Ninawakumbuka wabunge wote waliounga mkono hoja hiyo, akina Jenerali
Twaha Ulimwengu, Mateo Qaresi, Edward Oyombe Ayila, Shashu Lugeye, Dk. Mganga
Kipuyo, John Mwanga, Dk. Deogratius Mwita, Abel Mwanga, Patrick Qorro, Dk.
Ndembwela Ngunangwa, Richard Koillah, Paschal Mabiti, Luteni Lepilal Ole
Molloimet, Lumuli Alipipi Kasyupa,
Profesa Aaron Massawe, Arcado Ntagazwa.
Walikuwemo pia, Phineas Nnko, Paschal Degera, Mussa Nkhangaa,
Halimenshi Mayonga, Said Abdallah Nakuwa, Mosi Tambwe, Luteni Kanali John
Mhina, Charles Kagonji, Kisyeri Werema Chambiri, Tobi Tajiri Mweri, Aidan
Livigha, Philip Marmo, Erasto Lossioki, Shamin Khan, Raphael Shempemba, Mussa
Massomo, Jared Ghachocha na Mariam Kamm.
MAMBO WALIYOYATAKA:
Kinachojadiliwa sasa kwa kiasi kikubwa kilikwishaelezwa huko nyuma, kwa
sababu mambo ambayo akina Njelu Kasaka waliyataka ni mabadiliko katika Katiba ya
Muungano, ambao walisema ulizaliwa bila kupata baraka za wananchi na hivyo kuwa
na upungufu.
Wakaeleza kwamba, kwa wakati huo ilikuwa lazima muungano huo ufanywe
haraka haraka ili kulinda mapinduzi ya kumwaga damu ya ndugu zetu wa Visiwani;
Unguja na Pemba, kwamba Sultani Jamshid angeweza kurejea tena kwa msaada wa
kutoka kokote kule duniani. Kwa hiyo, nchi hizo ziliungana tu kwa sababu za kiulinzi
na kiusalama zaidi.
Kwa upande mwingine, mambo yanayoelezwa na Wazanzibari wa leo
wanaochoma makanisa yaliwahi kuelezwa na Aboud Jumbe Mwinyi na ndiyo
yaliyomgharimu mwaka 1984 wakati alipovuliwa madaraka yote ndani ya SMZ,
Muungano na CCM.
Wazanzibari hawako tayari hata kusikia kunakuwepo na muundo wa Serikali
Moja. Watanganyika wanaendelea kujipendekeza tu huku wakiwa wamepoteza utaifa
wao wakati ndani ya Katiba hiyo Zanzibar inatajwa na ina serikali yake.
Wazanzibari wanadai eti wakati Muungano unafanyika wao walikuwa na
serikali yao kamili! Huu ni upuuzi kwa sababu hata Tanganyika ilikuwa na
serikali yake na ndiyo iliyotangulia kujikomboa. Vinginevyo, muungano huo
ungetokea vipi kama Zanzibar haikuwa taifa kamili?
Pengine tufike mahali tuwaache Wazanzibari waendelee na mambo yao, kwa
sababu walikwishauvunja Muungano miaka mingi iliyopita.
Sisi tuijadili na kuirekebisha Katiba yetu, itufae maishani, hao
wamekwishatuulia mwana mwingine wa Mwalimu Nyerere kama walivyomuua ‘Azimio la
Arusha’ huko huko Zanzibar mwaka 1992.
If Zanzibar don't like unitary state then they should park and go! 43milion Tanzanians can do without 1.5 million Isle!
ReplyDelete