Sumbawanga. Watu wasiofahamika wamemvamia na kumuua mganga wa kienyeji, Salehe Garimoshi (65), mkazi wa Kijiji cha Milala wilayani Mpanda kwa kumpiga risasi kichwani kisha kuukatakata mwili wake kwa mapanga.
Taarifa kutoka eneo la tukio, zilizothibitishwa na Jeshi la Polisi zinadai kuwa baada ya mganga huyo kuvamiwa na watu hao, mmoja wao aliyekuwa na bunduki, alimfyatulia risasi kichwani kisha kuamuru wenzake wamkatekate kwa mapanga.
Kaimu kamanda wa polisi wa Mkoa wa Katavi, Focus Malengo alisema jana kuwa mauaji hayo yalitokea Agosti 10, saa 2:00 usiku, wakati mganga huyo alipokuwa anakula na familia.
Kabla ya mauaji hayo, inadaiwa kwamba siku hiyo mchana, watu wawili walifika nyumbani kwa mganga huyo na kumkuta Peter Martin aliyekuwa anaishi nyumbani hapo kwa ajili ya kupata tiba ya ugonjwa uliokuwa unamsumbua.
Kamanda alisema watu hao walimuuliza Martin kama mganga huyo yupo na kujulishwa kuwa hakuwepo.
“Hapo ndipo watu hao walipoamua kumpigia simu mganga huyo na kumjulisha kwamba wapo nyumbani kwake, wanahitaji kumuona ili awasaidie. Muda mfupi baadaye mganga alifika na kuwakuta watu hao ambao walimwambia mganga kuwa wana mgonjwa, lakini wamemwacha mbali kwa sababu gari lililombeba limeharibika katika Kijiji cha Kakese, hivyo watamleta baadaye,” alisimulia kamanda Malengo na kuongeza kwamba mganga huyo aliwakaribisha watu hao chakula cha mchana.
Inadaiwa ilipotimu saa 12:00 jioni, wageni hao wawili walidai kwamba wanamfuata mgonjwa wao na kuahidi kurejea nyumbani kwa mganga huyo saa 2:00 usiku.
Kamanda Malengo alisema ilipofika muda huo, mganga huyo, familia yake na wagonjwa waliokuwa wanatibiwa wakiwa wanakula chakula usiku, nje ya nyumba, ghafla walifika watu wanne kati yao wawili ni wale waliokuwa wameaga kuwa wanakwenda kumleta mgonjwa.
Alisema mmoja kati ya watu hao alimwambia mganga amtazame usoni, kisha akampiga risasi kichwani na kuwaamuru wenzake wamkatekate kwa mapanga mganga huyo kisha wakatoweka.
Alisema uchunguzi wa polisi bado unaendelea na hadi sasa chanzo cha mauaji hayo hakijafahamika.
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment