Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Thursday 14 August 2014

ALICHOKISEMA WAZIRI MKUU MALECELA BUNGENI KUHUSU SERIKALI TATU APRILI 30, 1992


Wako watu wanaodhani kuwa pendekezo la Tume ya Nyalali la kutaka Shirikisho la Serikari Tatu, linatokana na maoni au matakwa ya watu. Hiyo si kweli hata kidogo. Lakini watu wanaotaka tuamini kwamba wasemavyo ni kweli si watu waongo, ni wajinga tu, maana nadhani hawajasoma Ripoti ya Tume ya Nyalali. Hotuba ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, ya tarehe 30 Aprili, 1992, katika Bunge Ia Muungano inaeleza vizuri sana ukweli ulivyo:

Mheshimiwa Spika, mojawapo ya mapendekezo makubwa yaliyotolewa na Tume ya Nyalali lilihusu mfumo wa Muungano na Ushirikiano kati ya Tanzania, Visiwani. Tume ya Nyalali ilipendekeza kuubadili mfumo wa Muungano ili kuanzisha mfumo mpya ya Shirikisho lenye Serikali Tatu. Yaani, Serikali ya Shirikisho, Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar. .

Mheshimiwa Spika, hili ni pendekezo kubwa na la msingi ambavyo kama ilivyofanya Tume, Chama Cha Mapinduzi na Serikali zimelitafakari kwa undani zaidi. Katika kufanya hivyo, historia ya Muungano tangu tarehe 26 Aprili, 1964 hadi sasa imezingatiwa. Muungano kama mnavyofahamu Waheshimiwa wabunge chimbuko lake ni mapatano ya “Article of Union” yaliyotiwa sahihi na waasisi.wa Muungano, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mzee Abeid Amani Karume, Mungu aiweke roho yake pema.

Mapatano hayo yalifanywa kwa manufaa ya wananchi wote wa Tanza­nia. Hilo halina ubishi. Miungano mingi ya aina hii duniani, imefanywa na viongozi kwa njia hii au nyingine kwa niaba ya wananchi, bila kuhojiwa na hapana sababu ya kuhojiwa kitendo hicho. Kwa msingi huo, wale wachache wanaohoji na kutaka kura ya maoni juu ya suala hili; hawaitakii mema nchi hii. Hoja hiyo haikubaliwi na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi) Mheshimiwa Spika, tangu kuanzishwa kwa Muungano wa nchi zilizokuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzi­bar na Jamhuri ya Watu wa Tanganyika, ziliungana na kuwa nchi maja na Taifa moja. Narudia tena, ziliungana kuwa nchi moja na Taifa moja. Kwa lugha ya kigeni, 'One Sovereign State'. Hivyo imejenga msingi imara wa umoja kati ya wananchi wa Tanzania. Tanzania Bara na Visiwani, zimekuwa zikifaidika kisiasa, kiuchumi na kiulinzi chini ya mfumo uliopo wa Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakubaliana na baadhi ya sababu zilizotolewa na Tume ya Nyalali kuwa ndizo ambazo mara nyingine zimesababisha hali ya kutoridhika na mfumo wa Muungano. Matatizo yapo, mengi ya matatizo hayo ni ya utekelezaji yaliyojitokeza wakati wa kushughulikia mambo ya Muungano. Na bila ya kuyaficha baadhi ya matatizo hayo ni mambo yanayohusu suala la uraia, milki ya fedha za kigeni, ukusanyaji na mgawanyo wa mapato kutokana na kodi na ushuru wa forodha, tatizo la for­mula ya kuchangia gharama za Muungano. Hakuna shaka kwamba haya ni matatizo na mara nyingine yanakera:

Hata hivyo, kwa heshima zote kwa Tume Waheshimiwa Wabunge watakubaliana nami kuwa utatuzi au ufumbuzi wa matatizo hayo, hautapatikana kwa kuanzishwa Shirikisho la Serikali tatu. Kinyume chake hiyo itakuwa ni chanzo cha kufifia umoja wa mshikamano wa Tanzania uliojengeka tangu mwaka 1964. Inatoa mwanya kwa wasiopenda umoja huo hatimaye kuuvunja. Hiyo siyo kwa manufaa ya wananchi wa Tanza­nia nzima. (Makofi) Mheshimiwa Spika, matatizo ni lazima yatatuliwe. Hivyo ni azma ya Chama Cha Mapinduzi na Serikali kuelekeza nguvu zake zote katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo bayo. Serikali na Chama zitaendelea kutafuta ufumbuzi wa matatizo hayo halisi na kuyaondoa kwa manufaa ya wananchi wote wa Tanzania chini ya mfumo wa sasa. Hivyo kwa sasa Serikali inaifanyia kazi maeneo yanayohusika. Uhusiano wa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na hasa katika maeneo yanayohusu matatizo niliyoyaainisha.

Kwa mtazamo huo, ndiyo maana katika marekebisho ya Katiba wakati huo, eneo linalohusu Rais wa Jamnhuri ya Muungano pamoja na uchaguzi wake na wa Makamu wake ambaye pia ni Rais wa Zanzibar linawekwa kando, likisubiri mapendekezo mapya ya Serikali kwa Bunge lako Tukufu kwa kutungiwa muswada utakaowasilishwa hapo baadaye katika Bunge lako Tukufu.

Kwa wakati huu sehemu hii ya katiba itatoshelezwa kwa muda na ibara ya 37 ya katiba ya Jamhuri. Rekebisho hili limefanywa katika Muswada na kubadili katika katiba.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia ukweli kwamba tangu mwanzo ulipoanzishwa Muungano Waasisi kwa makusudi kabisa hawakututajia muundo wa Shirikisho la Serikali tatu au Serikali moja, ni dhahiri muundo unaopendekezwa unatutoa kutoka msingi huo wa awali. Ni mfumo ambao unadhoofisha nchi nzima ya Tanzania. Kwani Shirikisho ambalo lingeweza kuundwa na nchi mbili huru zenyewe zikibakia kuwa ni Jamhuri na hivyo kuwa na Serikali tatu halitasaidia lolole katika kudumisha hali ya utulivu na usalama ya wananchi wetu. (Makofi)

Hapatakuwa na mshikamano madhubuti katika masuala ya uchumi na maendeleo ya jamii na gharama ya kuziendesha Serikali tatu, ingekuwa kubwa sana na isiyo ya lazima. Kwa sababu hizi, ndiyo maana Chama Cha Mapinduzi na Serikali yake hazikubali pendekezo la Tume ya Nyalali la kuanzisha mfumo mwingine wa Muungano wa Serikali tatu. (Makofi).

Isitoshe Mheshimiwa Spika, hata pendekezo hili silo la wananchi wengi. Kwani taarifa ya Tume inasema, na naomba ninukuu. "Zaidi ya hayo wengi wa wananchi waliotoa maoni yao kwa Tume hawakuelezea chochote juu ya mfumo wa Serikali ambao Muungano uwe nao.
Kati ya wananchi elfu tatu (3,000) waliojitokeza kwenye Tume huko Zan­zibar ni wanne (4) tu waliozungumzia jambo hilo ambayo ni asilimia (0.13) ndio waliopendekeza kuwepo kwa mfumo wa Serikali tatu. Na kati ya wananchi 32,275 waliotoa maoni yao kwa Tume ndio waliopendekeza mfumo wa Serikali tatu. Wana-Tume ambao hawakubaliani na pendekezo hilo la kuwa na Serikali tatu, walisisitiza kwamba na ningewanukuu; "Pamoja na kuelewa kuwa baadhi ya mambo mengine siyo lazima uamuzi wake kutegemea wingi wa watoa maoni lakini pia tunaona kuwa siyo busara kupendekeza mabadiliko makubwa kama haya ya mfumo wa Muungano wetu kwa kutegemea maoni ya Watanzania 49 kati ya Watanzania 36,299 walioshiriki katika mjadala wote, ulioendeshwa na Tume ya Rais. Idadi hii ni ndogo isiyo na uzito kitakwimu."

Sisi hatuoni kuwa kuna hoja ya kisheria na ya kisiasa ya kubadili mfumo wa sasa wa Serikali mbili na kuanzisha mfumo wa Serikali tatu. Tanaamini kuwa mfumo wa Serikali tatu, utadhoofisha Muungano wetu kisiasa na kiuchumi". (Makofi)

Hivyo ndivyo Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tan­zania alivyosema Bungeni tarehe 30, Aprili, 1992; akashangiliwa na kupigiwa makofi na wabunge wa Tanzania. Baadaye, kama tunavyojua, Waziri Mkuu aliisahau hotuba hii; na wabunge waheshimiwa walisahau shangwe zao na makofi yao. Wakapitisha Bungeni, "kwa kauli moja", Azimio la kutaka Serikali ya Tanzania ilete muswada wa kubadili Katiba ya Nchi yetu ili kuwa na Serikali ya Tanganyika "ndani ya Muungano", kwa madai ya kwamba hayo ndiyo " matakwa ya wananchi wa Tanzania.

Lakini ukweli wa suala hili unabaki pale pale: Wananchi wa Tanzania hawadai Serikali ya Tanganyika; na mimi nasema, ukifufua Tanganyika, utaua Tanzania. Fahari wawili hawakai zizi moja: "Yeltsin" wa Tanganyika ataua Muungano. Lakini pia sababu zile zile za ukabila na udini na tamaa za uongozi zitakazoua Tanzania hatimaye zitaiuaTanganyika nayo.
REJEA: NYERERE, J.K.; UONGOZI WETU NA HATMA YA TANZANIA (1994)

No comments:

Post a Comment