Pages

Pages

Pages

Wednesday 2 July 2014

RIWAYA TAMU: JUDITH…JUDITH…! - 19


INNOCENT A. NDAYANSE (ZAGALLO)

0755 040 520 / 0653 593 546 

UTANGILIZI
Judith ameamua kuingia mjini na kufanikiwa kubadili fedha za kigeni Dola 2,000 alizomwibia Makella. Amerejea Magomeni Mapipa na sasa anakunywa supu. Ndipo anapoingia kijana Edson ambapo mazungumzo yanaendelea yanayoashiria mapenzi baina yao. Je, nini kitaendelea? Ungana na msimulizi wako upate uhondo wa simulizi hii…

EDSON alikuwa akifanya kazi Wizara ya Viwanda na Biashara. Tangu ahitimu masomo na kuanza rasmi ajira, ilishatimu miaka miwili, na kituo chake cha kwanza katika ajira hiyo kilikuwa jijini Dar es Salaam, makao makuu ya wizara hiyo.
Tangu alipobalehe Edson hakuwa mpenzi wa wanawake. Kwa ujumla hakulipa kipaumbele suala la kuwa na uhusiano wa mapenzi na wanawake. Lakini siyo kwamba aliishi vivihivi, la hasha. Kabla hajahitimu darasa la saba alidiriki kufanya mapenzi na mwanamke mmoja katika mazingira  ambayo hata yeye hakuyatarajia. Baada ya siku hiyo, ilipita miaka takriban mitatu hadi alipodiriki kufanya tena tendo hilo na wasichana wawili kwa nyakati tofauti wakati akiwa kidato cha nne.
Ndiyo, ngono ilikuwa ni burudani kwake lakini hakuichukulia kama sheria badala ya kawaida katika utekelezaji. Sasa alikuwa na miaka mitatu akiwa hajafanya tendo hilo kiuhalisia, zaidi aliziweka hisia zake kwa mmoja wa wale wasichana aliowahi kufanya nao tendo hilo, akiweweseka bafuni au popote alipopaona panastahili kwa faragha, sabuni ikiwa ndiyo nyenzo madhubuti katika kumtatulia matatizo yake faraghani.
Tangu alipoanza kazi hapo Wizara ya Viwanda na Biashara alikumbana na vishawishi vingi kutoka kwa wanawake warembo, lakini alikuwa makini, maradhi ya Ukimwi yakiwa ni tishio kubwa kwake. Nasaha zilizotolewa katika vyombo mbalimbali vya habari sanjari na kuwakumbuka baadhi ya watu aliowajua, ambao waliumwa na hatimaye kufariki akiwaona, ilikuwa ni taswira halisi ya kumfanya afikiri mara mbili-mbili kabla ya kuchukua hatua ya kumchojolea nguo mwanamke yeyote.
Ndiyo, alikuwa makini, lakini pia alitambua kuwa alipaswa kuoa. Ataishi peke yake hadi lini? Ni kwa wazo hilo la kumpata mwenzi ndipo alipoamua kutulia, akimwomba Mungu ampatie huyo atakayestahili kuwa mkewe.
Asubuhi hii akiwa na Judith kando yake, alihisi kuwa Mungu kampatia mchumba. Alimwona Judith kama mwanamke wa kipekee, ambaye hajapata kumwona tangu azaliwe.
Japo Judith hakutofautiana na wafanyakazi wenzake ambao hawajaolewa na ambao pia walionyesha dhahiri kumhitaji, wakiwa wazuri kwa sura na maumbile yao , hata hivyo akilini mwa Edson hawakustahili kuwa katika himaya yake. Japo mtaani alipoishi aliwaona mabinti kadhaa ambao ilikuwa ni kiasi tu cha kuwaambia wazazi wao, “nataka kumuoa mwanenu…” wakakubali haraka, au yeye mwenyewe kumvaa moja kwa moja binti  na kumtamkia, bado hakuwa tayari kufanya hivyo.
Alihitaji kuoa, lakini alihitaji kumuoa yule atakayempenda kutoka moyoni. Hakuhitaji kuijua historia ya huyo mke mtarajiwa, jambo hilo aliamini kuwa lingemfanya asite kuchagua yule amfaaye. Huyu Judith alimvutia kwa sura na umbo lake. Kwake, hizo zilikuwa ni sifa tosha. Hakupenda kuijua historia yake.  Isitoshe, moyo wake ulimkubali. Nini zaidi?
Kwa hali hiyo, pale alipomuuliza Judith kama ameolewa, naye akamjibu, “Sijaolewa,” kwake lilikuwa ni jibu lililomtia faraja kubwa. Na ndipo alipoamua kufungua ukurasa mpya. Akajieleza, akajieleza, akituma rasmi ombi la kuwa karibu zaidi kiuhusiano.

**********
MJINI KIGALI

SIKU ya pili baada ya Makella kukimbiwa na Judith hakutoka nyumbani. Alijihisi kuchanganyikiwa. Hakuwa timamu. Kila alipofikiria kufanya hiki, akajikuta akiona kuwa haifai kufanya.
Tangu alipoingia chumbani mwake jana hadi saa 4 asubuhi hii hakuwa ametoka, alijikuta akimchukia kila mtu na hata kujichukia mwenyewe. 
Alijilaza kitandani huku akisonya kila wakati na tayari alikuwa amekwishavuta sigara tano kwa hasira. Akijihisi kuwa timamu kidogo kila alipovuta. Akafungua kabati na kutoa chupa kubwa ya whisky, akaifungua na kunywa funda kadhaa kisha akarudisha kabatini.
Akajiwa na wazo la kutoka ili akazimalizie hasira zake kwa Jamillah, mwanamke ambaye alikuwa na uhusiano naye wa kimapenzi ilhali akitambua fika kuwa ni mke wa askari mwenzake.
Akaiacha bunduki ndani na kutoka. Hapakuwa mbali hapo kwa Jamillah. Ni nyumba ya nne tu kutoka hapo alipoishi Makella. Na Makella alikwenda kwa kujiamini kwa kuwa alitambua kuwa Ramadhani ambaye ndiye mume wa Jamillah bado alikuwa hospitali alikolazwa kwa maradhi ya homa.
Pombe zikichangia kumpa ujasiri, Makella alitembea kwa kujiamini na kuufikia mlango wa nyumba hiyo. Taa zilikuwa zikiwaka. Akagonga mara mbili. Muda mfupi baadaye mlango ukafunguliwa. Jamillah alikuwa mbele yake.
Wakatazamana, Jamillah akiwa anaonekana kutokuwa na furaha lakini Makella akashindwa kuitambua hali hiyo. Akaingia ndani kama kwake. Akarudisha mlango na kumvuta Jamillah kisha akamkumbatia kwa nguvu.
Jamillah akajitahidi kujing’atua bila ya kutamka chochote. Makella akaendelea kumng’ang’ania na kumbusu shavuni. Hakutambua kuwa kutoka chumbani, masikio ya Ramadhani ambaye siku hiyo daktari alikuwa amemruhusu kurudi nyumbani yalinasa purukushani hiyo.
Taratibu Ramadhani alitoka kitandani na kuchungulia. Akamwona Makella akimkumbatia Jamillah. Hasira zikampanda kwa kiwango kisichokadirika. Akakumbuka tetesi alizowahi kuzisikia kuwa Makella alikuwa na uhusiano wa mapenzi na Jamillah. Hasira zikampanda. Akageuka na kurudi kwenye kabati ambako alifungua saraka moja na kutoa bastola. Papohapo akatokeza sebuleni na kufoka, “Makella…Makella….kumbe ndiyo tabia yako!”

Itaendelea kesho…


No comments:

Post a Comment