Pages

Pages

Pages

Tuesday 1 July 2014

RIWAYA TAMU: JUDITH…JUDITH…! - 18


INNOCENT A. NDAYANSE (ZAGALLO)

0755 040 520 / 0653 593 546 

UTANGILIZI
Judith amenunua nguo chache za kuanzia, lakini kutwa nzima hakumuona Baraki ambaye baadaye anampigia simu kupitia simu ya muhudumu wa gesti kwamba asingekuja bali wangeonana kesho yake. Kesho yake mapema Judith anaamua kwenda mjini ili akabadili fedha zake. Anafanikiwa kubadili na kukodi teksi kumrudisha Magomeni. Ungana na msimulizi wako upate uhondo wa simulizi hii… 

Dakika iliyofuata Judith alikuwa ameshaachana na teksi hiyo. Akatembea taratibu akiifuata  barabara ileile aliyoitumia asubuhi kuja hapo kituoni. Ni wakati huo ndipo alipoihisi njaa, na akakumbuka kuwa tangu asubuhi alikuwa hajatia kitu tumboni.
Akaangaza hapa na pale na kuona baa moja nyuma ya kituo cha daladala. Watu walikuwa wengi katika eneo hilo, baadhi wakinywa soda, baadhi wakinywa supu na wengine wakinywa bia.
Alikwenda na kuagiza supu, chapati mbili na soda. Wakati akisubiri huduma hiyo, mara akamwona mtu mwingine akija katika meza hiyo. Alikuwa ni mwanamume, kijana mwenye umri kati ya miaka ishirini na mitano na thelathini na mitano. Kijana huyo alipofika alimtazama Judith huku akiachia tabasamu la mbali na kisha akasema, “Samahani, sista, naweza kuketi hapa au mwenyewe katoka?”
Judith akaunyanyua uso na kumtazama mtu huyo. Akavutiwa na utanashati wake; shati jeupe la mikono mirefu, suruali nyeusi na viatu vyeusi vilivyonakshiwa vizuri. Macho ya kijana huyo yalikuwa kitu kingine kilichomvutia kiasi cha kuhisi mshtuko kila walipotazamana.
“Au kuna mtu, sista?” kijana huyo alirudia kumuuliza huku akimtazama kwa makini zaidi, tabasamu likizidi kuchanua.
“Keti tu,” Judith alijibu. “Sidhani kama kuna mtu aliyekuwa hapa. Mie nimekuta meza nyeupe.”
Dakika chache baadaye mtu huyo alikuwa akinywa soda huku Judith akifakamia supu.
“Samahani, anti, tunaweza kufahamiana zaidi?” kijana huyo aliamua kuuvunja ukimya uliokuwa umeitawala meza hiyo.
Judith alimtazama kidogo kisha akayarejesha macho kwenye bakuli la supu. Akachota mchuzi kwa kijiko na kunywa. Akafanya hivyo mara mbili zaidi, kisha akaachia tabasamu la mbali. “Inategemeana ni kufahamiana ki-vipi,” hatimaye alisema.
Kijana yule alilikuza tabasamu lake na kusema, “Ni kwa utaratibu wa kawaida tu.”
“Sijakuelewa,” Judith alisema, safari hii akiunyanyua uso na kumtazama kijana huyo kwa makini, paji la uso wake likiunda mikunjo ya mbali.
“Yaani kwa mfano,” mtu huyo alisema, “Mimi naitwa Edson. Ni jina langu halisi. Ni mzaliwa wa Kigoma. Nadhani mpaka hapo inatosha. Sijui wewe. Au nitakuwa nimegeuka Ofisa Uhamiaji au askari polisi?”
Kicheko cha mbali kilimtoka Judith. Akamtazama tena Edson na kuyasoma macho yake, akitaka kuthibitisha kama kuna uwiano wowote kati ya macho hayo na maneno yake. Akakumbana na macho yaliyong’ara sanjari na tabasamu dhaifu lililolandana na utazamaji wake.
Sasa Judith akajiona ameondokana na upweke. Japo huyu mtu alikuwa mgeni kabisa machoni pake, tofauti na Baraki aliyemwokoa kutoka Rwanda, hata hivyo alijiona kuwa kampata mkombozi halisi.
“Naitwa Judith,” hatimaye alisema. Hakuendelea kutoa utambulisho zaidi, alijiuliza kama ilikuwa sahihi kutoboa undani wa asili yake. Jibu lililomjia akilini ni HAPANA.
Alitambua fika kuwa uraia wa mtu ni jambo linalotiliwa umuhimu katika mataifa mengi duniani. Siyo kwamba raia au mzaliwa wa nchi moja haruhusiwi kuishi nchi nyingine, la hasha. Anaweza kuishi, lakini kwa utaratibu unaokubalika kisheria. Raia wa nchi nyingine, kama yeye Judith, anaruhusiwa kuishi Tanzania ama nchi nyingine yoyote endapo tu atakuwa amefuata kanuni husika ambazo zinatambulika kitaifa na kimataifa.
Kwa hali hiyo, yeye alipaswa kuwa hapo Dar es Salaam huku Idara ya  Uhamiaji ikiwa na taarifa yake. Isingewezekana amtamkie bayana huyu mtu kuwa yeye ni mzaliwa wa taifa la Rwanda . Hilo halikumwingia akilini wakati huo. Akaendelea kufikiria jinsi atakavyojieleza kama ataulizwa swali jingine hususan kuhusu uraia wake.
“Ni jina zuri,” Edson alimkatisha mawazo yake. Akatamka tena kwa sauti ya chini, “Judith…Judith, jina zuri kama ulivyo.”
Tabasamu jingine likamtoka Judith. Akaunyanyua uso na kumtazama kidogo Edson kisha akayaepuka macho na kuyarejesha mezani. Kwa sauti yenye taswira ya aibu, akasema, “Asante.”
“Unaishi maeneo hayahaya ya Magomeni?” Edson alirusha tena swali.
“Ndiyo.”
I see. Ni mpweke kama mimi au…?”
Judith akamtazama tena, safari hii kwa chati sana . Akakohoa kidogo na kunywa tena soda yake, kama vile hajalisikia swali hilo .
“Eti Judi,” Edson alimbana. “Umeolewa?”
“Kwa nini unauliza ivo?”
Edson alicheka kidogo kisha akasema, “Wengine ni waoga wa kupigwa risasi au kuchomwa visu na wenye mali.”
Judith naye akacheka.
Wakatazamana, macho ya kila mmoja yakiwa na kitu fulani kilichozungumza neno moja tu: MAPENZI. Judith akabibitua midomo na kuendelea kunywa supu yake. Kwa mara nyingine ukimya ukapita katika eneo hilo.
Wakatazamana tena, safari hii Judith akaachia tabasamu la kirafiki, zaidi ya urafiki wa kawaida.
“Judith,” Edson alimwita kwa sauti ya chini.
Judith hakuitika kwa sauti, alimtazama kidogo Edson kisha akauinamisha tena uso.
“Judith,” Edson aliita tena na safari hii alionekana kutojali kuitikiwa. Akaendelea, “Samahani kwa hili nitakalokuuliza kama nitakuwa nimefanya kosa.”
“Hapana, hujafanya kosa,” Judith alijibu huku akiyaepuka macho ya Edson.
“Asante. Kwa hiyo?”
“Sijaolewa,” jibu la Judith lilikuwa fupi.
Lilikuwa ni jibu lililomtia ujasiri Edson. Sasa akapata nguvu ya kuendelea kuzungumza.


Itaendelea kesho…

No comments:

Post a Comment