Pages

Pages

Pages

Sunday 20 July 2014

RAIS KIKWETE: HATUTATUMIA NGUVU MALAWI

JK: Hatutatumia nguvu Malawi

RAIS Jakaya Kikwete, amesema kamwe Tanzania haitatumia nguvu kumaliza mvutano kati yake na Malawi kuhusu mpaka kati ya nchi hizo.
Kauli hiyo aliitoa jana alipokuwa akiwahutubia wananchi waliofika kwenye mkutano wa hadhara mjini Mbamba Bay mkoani Ruvuma.
Rais Kikwete yupo katika ziara ya siku sita mkoani humo ambako alifanya shughuli mbalimbali katika Wilaya ya Nyasa ikiwemo kuzindua Daraja la Ruhekei lililoko katika Kijiji cha Mkalole, kilomita nane kutoka mjini Mbamba Bay.
Alisema Tanzania haioni mantiki ama busara yoyote kuingia vitani na nchi yoyote jirani kwa sababu yoyote ile.
“Nataka kuwatoeni wasiwasi. Hakuna sababu ya vita. Laleni usingizi bila wasiwasi, kuleni samaki wenu, kwa sababu Tanzania haioni busara ya vita.
“Tanzania haiwezi kutumia nguvu kupata suluhisho la mvutano wa mpaka. Tuna uwezo wa kupata jawabu la tatizo hilo bila kutumia njia ya vita.
“Tanzania haioni busara hiyo ya vita. Tuna uwezo wa kupata ufumbuzi kwa njia ya majadiliano. Na wala msimamo huo siyo kwa mpaka wetu na Malawi pekee, bali kwa mipaka yote ya Tanzania,” alisema.
Kikwete pia alisema juhudi zimekuwa zinafanywa na Tanzania kutatua tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kuliomba jopo la marais wastaafu kusaidia kutafuta jawabu la mpaka kati ya nchi hizo mbili.
Marais hao, Joachim Chissano wa Msumbiji, Festus Mogae wa Botswana na Thabo Mbeki wa Afrika Kusini, wanasaidiwa na jopo la kimataifa la mabingwa wa sheria.
Aliwahakikishia wananchi wa Wilaya ya Nyasa kuwa ahadi na mpango wa serikali kuweka meli mpya katika Ziwa Nyasa uko pale pale na kwamba mipango inafanywa ya kuhamisha chelezo cha kujengea meli kutoka Mwanza kwenye Ziwa Victoria kuipeleka Itungi, Kyela, Mbeya ili kuanza ujenzi ambapo sh. bilioni 23 zimetengwa kwa mchakato huo.
Alisema kuwa michoro ya meli hiyo ya Ziwa Nyasa imelazimishwa kubadilishwa kidogo kwa sababu ya ukweli kuwa ziwa hilo lina mawimbi makali na huchafuka mara kwa mara tofauti na Victoria na Tanganyika.
Aliongeza kuwa serikali inaendelea na mipango ya kujenga reli kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay ili kuzidi kufungua ukanda wa Mtwara na kuweza kubeba chuma na makaa ya mawe kutoka Liganga na Mchuchuma.
http://www.freemedia.co.tz/daima/jk-hatutatumia-nguvu-malawi/

No comments:

Post a Comment