Pages

Pages

Pages

Tuesday 1 July 2014

MIRERANI KUUNDA MFUKO WA POLISI JAMII


Na Mwandishi Wetu, brotherdanny5.blogspot

MANYARA: KAMATI ya maendeleo ya Kata ya Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, imeazimia kuanzisha mfuko wa kusaidia polisi jamii wa kata hiyo kwa lengo la kuwawezesha ili wafanye kazi zao ipasavyo katika ulinzi shirikishi.
Diwani wa kata ya Mirerani, Justin Nyari akizungumza juzi mbele ya Mkuu wa kituo cha polisi Mirerani, ASP Lwitiko Kibanda, alisema wanatarajia kuomba kibali kwa Mkuu wa wilaya hiyo ili kuchangisha fedha za kutunisha mfuko huo.
“Tunatarajia kuanzisha mfuko huu baada ya OSC wa Mirerani kuleta wazo hili na sisi tuthamini kazi za polisi jamii katika kata yetu, kwani wamekuwa msaada mkubwa kwa wananchi katika kupambana na uhalifu,” alisema Nyari.
Alisema mfuko wa polisi jamii na ulinzi shirikishi utawasaidia kuwapa morali ya kufanya kazi kwa juhudi zaidi tofauti na hivi sasa ambapo hawapati kifuta jasho ili hali wanafanya kazi nzuri za kusaidia wananchi kwenye suala la ulinzi.
Naye, Mkuu wa kituo cha polisi Mirerani, Mrakibu Msaidizi wa polisi, Lwitiko Kibanda alitoa shukurani kwa uongozi wa kata hiyo kujali na kuthamini jitihada za polisi jamii wa eneo hilo, ambao wamekuwa msaada mkubwa kwa polisi.
“Tumekuwa tukiwapa mafunzo polisi jamii zaidi ya 30 hapa kituoni na wamekuwa wakitusaidia katika shughuli za ulinzi na usalama hapa Mirerani, ila tatizo ni namna ya kuwawezesha kwani sisi hatuna fungu hilo,” alisema Kibanda.
Alisema dhana ya ulinzi shirikishi na polisi jamii ilianzishwa na jeshi la polisi baada ya kuona kuwa watakuwa msaada kwa askari kutokana na idadi ndogo ya polisi waliopo nchini hivyo watashirikiana nao kuhakikisha usalama unakuwepo.

No comments:

Post a Comment