Pages

Pages

Pages

Tuesday 1 July 2014

CAMEROON ILIVYOIHENYESHA ENGLAND, PENALTI ZIKAIATHIRI


 Kipa Thomas Nkono akiokoa hatari katika fainali za mwaka 1990


Na Daniel Mbega

SIKU kama ya leo, yaani Julai Mosi, mwaka 1990 Afrika ilikaribia kuvunja rekodi yake ya Kombe la Dunia wakati wawakilishi wake, Cameroon (Simba Wasiofugika), walipocheza kwa umahiri mkubwa mechi yao ya robo fainali dhidi ya England.
Mechi hiyo iliyofanyika kwenye Uwanja wa San Paolo jijini Naples huko Italia mbele ya watazamaji 55,205, ilichezeshwa na mwamuzi Edgardo Codesal wa Mexico aliyesaidiwa na Vincent A. Mauro wa Marekani na Jassim Abdulrahman Mandi wa Bahrain na ilishuhudia kandanda safi lililoonyeshwa na Cameroon, ingawa baadaye penalty zikaiathiri katika muda wa ziada na England kuibuka na ushindi wa 3-2.
Ndiyo mechi pekee ya robo fainali ambayo ilikuwa na goli zaidi ya moja, kwani England ilishinda kwa mabao 3-2 baada ya dakika 120.
England ndiyo iliyoanza kupata bao kupitia kwa David Platt katika dakika ya 25. Lakini baada ya mapumziko mkongwe Roger Milla akaingizwa dakika ya 61 na kuubadili mchezo ndani ya sekunde tano ambapo Cameroon walipata penalti iliyofungwa na Emmanuel Kunde.
Baadaye katika dakika ya 65, Eugene Ekeke akafunga bao la kuongoza. Waafrika wakajua wanakwenda nusu fainali, lakini wakasababisha penalti ambayo ilifungwa na Gary Lineker katika dakika ya 83.
Mchezo ukaingia kwenye muda wa ziada na katikati ya muda huo wa ziada, England wakapata penalti nyingine katika dakika ya 105 ambayo ilifungwa na Lineker na wakafuzu kwa nusu fainali.
Vikosi vya siku hiyo vilikuwa: England: Peter Shilton, Stuart Pearce, Des Walker, Terry Butcher (nahodha) Trevor Steven 73’, Chris Waddle, Gary Lineker, John Barnes/Peter Beardsley 46’, Paul Parker, Mark Wright, David Platt, na Paul Gascoigne ‘Gaza’. Kocha alikuwa mzalendo Robert Robson.
Cameroon: Thomas Nkono, Emmanuel Kunde, Stephen Tataw (nahodha), Benjamin Massing, Bertin Ebwellé, Thomas Libiih, Emmanuel Maboang Kessaky/Roger Milla 46’, Jean-Claude Pagal, Louis-Paul Mfédé/ Eugène Ekéké 62’, François Omam-Biyik, na Cyril Makanaky. Kocha alikuwa Valeri Nepomniachi wa Urusi.
Waliopewa kadi za njano kwa Cameroon ni Benjamin Massing 28’, Thomas Nkono 104’ na Roger Milla 119’, na kwa England ni Stuart Pearce 70’.
Mechi nyingine iliyochezwa siku hiyo ni kati ya Ujerumani Magharibi na jirani zao Czechoslovakia ambapo Ujerumani walishinda kwa bao 1-0 la mkwaju wa penalti wa Lothar Matthäus katika daika ya 25.
Mchezo huo ulifanyika San Siro jijini Milan mbele ya watazamaji 73,347 na ulichezeshwa na Helmut Kohl wa Austria.

Siku kama ya leo Julai Mosi, lakini mwaka 19950 katika fainali zilizofanyika kule Brazil, wenyeji waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Yugoslavia katika hatua ya makundi (raundi ya pili) wakiwa Kundi la Kwanza.
Katika mchezo huo uliofanyika Estádio do Maracanã, jijini Rio de Janeiro na kuhudhuriwa na watazamaji 142,000 ukiwa chini ya uchezeshaji wa Benjamin Griffiths wa Wales, mabao ya washindi yalifungwa na Admeir(Ademir Marques de Menezes) 4’ na Zizinho (Thomaz Soares da Silva) 69’.

Siku kama ya leo mwaka 1982 kule Hispania kulikuwa na michezo miwili ya makundi ya raundi ya pili ambapo katika Kundi A Ubelgiji ilichapwa bao 1-0 na Urusi pale Camp Nou jijini Barcelona mbele ya watazamaji 45,000 mwamuzi akiwa Michel Vautrot wa Ufaransa. Bao la washindi lilifungwa na Oganesian dakika ya 48.
Kwenye Kundi D, Austria na Ireland zilifungana mabao 2-2 katika Uwanja wa Estadio Vicente Calderon jijini Madrid mbele ya mashabiki 20,000 ambapo mwamuzi alikuwa Adolf Prokop wa Ujerumani Mashariki.
Mabao ya Austria yalifungwa na Pezzey 50’ na Hintermeir 68’ wakati Hamilton aliifungia Ireland mabao yote mawili dakika za 27' na 75'.

Tarehe kama ya leo mwaka 2006 kule Ujerumani wakati wa hatua ya robo fainali, Brazil ilichapwa na Ufaransa bao 1-0 lililofungwa na Thierry Henry katika dakika ya 57 kwenye Uwanja wa Stadion Frankfurt mbele ya mashabiki 48,000, mwamuzi akiwa Luis Medina Cantalejo wa Hispania.
Katika mchezo mwingine war obo fainali siku hiyo, Ureno ilisonga mbele kwa mikwaju ya penalty dhidi ya England baada ya matokeo ya daika 120 kuwa 0-0.
England ilipata penalty moja tu kupitia kwa Hargreaves  wakati Lampard, Gerrard na Carragher wakikosa, na Ureno ilipata penalty tatu kupitia kwa Simão, Postiga na Ronaldo. Waliokosa ni Viana na Petit. Mchezo huo ulifanyika kwenye Uwanja wa Gelsenkirchen mbele ya watazamaji 52,000 na ulichezeshwa na Horacio Elizondo wa Argentina.


No comments:

Post a Comment