INNOCENT A.
NDAYANSE (ZAGALLO)
0755 040 520 /
0653 593 546
ILIPOISHIA:
Simulizi
zimemnogea Makella na sasa anaamua kunywa pombe. Anamlazimisha Judith naye
anywe. Kwa woga na hofu, anaamua kunywa pombe kwa mara ya kwanza maishani
mwake. Makella anasimulia mengi na kuwaponda wanawake wa Tanzania. Anajiuona
yuko huru zaidi. Hatimaye anaamua kwenda kuoga. Je, nini kitaendelea hali
Judith naye akiendelea kunywa pombe? Ungana na msimulizi wako…
Judith
hakujibu. Alitwaa tena chupa yake na kuipeleka kinywani. Sasa alikunywa bia
hiyo kama anywaye maji ya kawaida. Hakikuwa kinywaji kigeni. Ulimi ulishazoea.
Funda tatu zikapita kooni kwa mkupuo. Na Makella aliamini kuwa, kama Judith
ataimaliza bia hiyo basi lazima atakuwa hoi, na hatakuwa na kipingamizi
chochote cha kutendwa vyovyote. Zaidi, atatoa ushirikiano mkubwa bila ya woga
wala aibu.
“Wewe
endelea,” Makella alimwambia Judith. “Ikiisha, s’o vibaya ukiongeza moja.
Nakuhakikishia, kinywaji hicho kitakufanya ujisikie vizuri sana kisaikolojia.”
Alipomaliza
kuchojoa nguo, alitwaa taulo iliyokuwa imetundikwa kwenye eneo maalum, taulo ya
hoteli, akajifunga kiunoni na kuelekea bafuni.
**********
DAKIKA
ya kwanza baada ya Makella kuingia bafuni Judith alikuwa ameduwaa. Dakika ya
pili ndipo akili yake ilipochangamka. Akazitazama zile chupa za bia zilizokuwa
mbele yake. Akatema mate chini huku kakunja uso. Akasimama haraka na kutupa
macho kitandani ambako bunduki ilikuwa imetulia. Akayahamishia macho kwenye
nguo za Makella. Papohapo akazifuata na kuanza kuzipekua.
Sasa
alikwishabadilika. Hakuwa yule Judith mwenye macho yaliyolegea kiasi cha
kumfanya Makella ajiamini na kuwa na matumaini ya kustarehe kwa usiku huo.
Hapana. Huyu alikuwa Judith mwingine, Judith ambaye alitaka aitimize azma yake iwe,
isiwe! Kiwango cha bia aliyokunywa pia kikawa kinamwongezea ujasiri na
kumwondolea woga.
Mfuko
wa kwanza wa suruali hakuambulia kitu. Akauvaa mfuko wa pili. Humo akatoa
kitambulisho cha uraia, na kitambulisho cha jeshi, akavitupa zuliani na
kuukimbilia mfuko mwingine uliokuwa umetuna kidogo. Akashtuka baada ya kutoa
bulungutu la pesa! Moyo ukapiga paa! Akashusha pumzi kwa nguvu.
Noti
alizozitoa zilikuwa ni dola za Marekani 2,000. Hakuyaamini macho yake! Hakuwa
mgeni wa noti hizi. Miezi kadhaa iliyopita marehemu baba yake mzazi aliwahi
kumwonyesha sarafu na noti za Rwanda, Kenya, Tanzania, Uingereza, Ufaransa na Marekani.
Katika
zoezi hilo alimwambia, “Mwanangu Judi, pesa za Wazungu zina thamani sana, na
hasa pauni na dola. Pauni ni za Uingereza na Dola za Marekani. Hizo zina nguvu
zaidi dunia nzima! Lakini haya mafaranga yetu ya Kinyarwanda, Kirundi na
vikorokoro vya Tanzania, Uganda na Kongo mmh! Havina kitu! Afadhalli kidogo
pesa ya Kenya, ile ina nguvu kuliko zingine za ukanda huu.”
Maneno
hayo hakuyasahau, na sura za noti hizo hazikutoka katika kumbukumbu zake
kichwani tangu siku hiyo. Na usiku huo, akiwa humo chumbani, peke yake, dola 2,000
za Marekani zikiwa mkononi mwake, alijiona kishaiweka Rwanda katika himaya
yake.
Dola
2,000! Mungu ampe nini? Ndiyo, Mungu ampe nini yeye mtoto wa kike ambaye
hajawahi kumiliki dola 100?
Akashusha
pumzi ndefu huku akizipachika kwenye mfuko wa bukta yake aliyoivaa ndani ya
sketi. Akairudia tena suruali hiyo. Akaukagua mfuko wa mwisho lakini hakupata
kitu. Akahamia kwenye mfuko wa shati. Huko akaambulia sigara tatu na kibiriti.
Akasonya na kuvirudisha.
Sasa
akayatupa macho kwenye mlango wa bafu. Ni muda mfupi tu uliopita tangu Makella
alipoingia bafuni humo, na kwa mbali alisikia michirizi ya maji, hali iliyompa
taswira kuwa tayari Makella kishaanza kuoga.
Papohapo
Judith akaifuata ile bunduki, AK-47 na kuikamata mkononi. Akaguna. Uzito wa
silaha hiyo ukamvunja moyo. Hakutaka kujidanganya kuwa anaweza kuitumia silaha
hiyo dhidi ya adui yake yeyote kama akiamua kutoroka nayo. Kwanza, ni nzito.
Pili, hajawahi hata kujifunza jinsi ya kuitumia. Akahema kwa nguvu huku
akiirudisha taratibu kitandani. Akahisi woga ukimjia, lakini akajitahidi kujipa
ujasiri, akijua kuwa hakuna mtu wa kumwokoa bali anapaswa kutumia akili yake
yote ili ajinusuru dhidi ya jahili huyo.
Huo
ulikuwa ni muda pekee ambao aliamini kuwa ndiyo angeweza kuutumia katika
kujiokoa. Akapiga ngumi kiganjani na kuamua kuondoka. Papohapo akautwaa ufunguo
na kutoka taratibu, kisha taratibu vilevile akaurudisha mlango na kuuchomeka
ufunguo kwenye kitasa. Akafunga taratibu na kwa umakini huku akiangaza macho
kushoto na kulia katika korido hiyo. Korido yote ilikuwa tulivu na hakukuwa na
mtu yeyote.
Akafurahishwa
na hali hiyo na papohapo akauchomoa ufungo katika kitasa, akautumbukiza katika
mfuko wa bukta yake. Akatoka taratibu, akipita katika korido hiyo ya ghorofa ya
kwanza ya hoteli hiyo yenye ghorofa nne, mwendo wake ukiwa ni wa mtu wa kawaida
na asiye na wasiwasi. Watu wawili aliokutana nao, mmojawao akiwa ni mwanamke wa
Kizungu hawakumtilia shaka wala kumshangaa.
Alipofika
chini alikwenda moja kwa moja mapokezi na kumtazama yule mhudumu kwa uso wa
kirafiki, huku akiachia tabasamu la mbali. Kisha, akamwambia, “Dada, natoka
kidogo. Nafika mtaa wa pili mara moja. Sitachelewa.”
“Ok,” mhudumu yule alimjibu huku
akimtazama kwa macho ya wivu, akivutiwa na umbo zuri alilojaaliwa Judith hususan yale ‘makalio ya kumimina’ ambayo yalijitupa huku na kule wakati Judith
alipokuwa akiondoka.
Ilikuwa
ni saa 5 usiku!
**********
MIONGONI
mwa kanuni ambazo Makella hakuwa tayari kuzitengua ni kuoga maji baridi. Awe na
malaria, awe amekumbwa na uchovu mkali kiasi gani au hata awe anaihisi baridi
kali maungoni, kamwe hakuwa tayari kuoga maji moto.
Usiku
huo, pale tu alipoingia bafuni hakuwa na haraka. Alifungua bomba na kuyaacha
maji yaingie kwa wingi ndani ya sinki ndipo akaingia na kuoga kwa raha zake.
Alioga
kwa utulivu, moyoni akijihisi amani, akikumbuka kuwa huko chumbani kamwacha
msichana mzuri ambaye kwa muda mrefu amekuwa akihangaika ili ampate. Leo, usiku
huu, yuko naye! Ni raha iliyoje?
Akajifariji
kwa imani kuwa, pindi watakapokiangukia kitanda, ataburudika kwa kuyanyonya
yale matiti yaliyoshiba, yenye joto la uhai na ambayo ujazo wake pale kifuani
uliongeza urembo wa Judith badala ya kutoa sura ya kuchusha. Hataishia hapo,
ataendelea kujiliwaza kwa kuyatomasa na kuyapapasa maeneo mengine nyeti ya
mwili huo unaovutia kabla ya kuhitimisha starehe kwa hatua nyingine muhimu
zaidi.
Mungu ampe nini?
Dakika
kumi baadaye alikuwa akijifuta maji mwilini kisha akajifunga taulo kiunoni kama
awali na kutoka taratibu bafuni humo.
Itaendelea kesho....

No comments:
Post a Comment