INNOCENT A.
NDAYANSE (ZAGALLO)
0755 040 520 /
0653 593 546
Ilipoishia jana:
Makella
yuko na Judith, anaamini kwamba binti huyo sasa atampenda kutokana na ukweli
kuwa yeye ndiye aliyeushikilia uhai wake. Anaanza kusimulia mambo mbalimbali
ikiwemo uzoefu wake wa kuishi Dar es Salaam. Judith anaendelea kumsikiliza. Ungana
na msimulizi wako…
Akaendelea,
“Na siyo taarabu tu, pia kuna wapenzi wa
bongo fleva ambao ni vijana wa kishkaji-shkaji na wengine nd’o wanapenda dansi.
Kuna bendi za Kikongo zilizolowea hapo Dar na nyingine ni za hapohapo Tanzania
kama kongwe za Msondo Ngoma, Mlimani, African Stars na nyingine ndogondogo.”
Ukimya
mfupi ukatawala. Makella akanyanyua chupa na kuipeleka kinywani. Akagugumia
funda kadhaa na kuirejesha juu ya kimeza. Akayagandisha macho usoni pa Judith
kama vile anayemuuliza, “mbona na wewe
hunywi?”
Judith
hakuwa mbumbumbu wa fikra. Dhamira yake ya kuhakikisha kuwa anailinda heshima
na uhai wake ilikuwa palepale! Na hakukuwa na binadamu wa kuweza kuitengua.
Alimtazama mara moja tu Makella na kubaini ni kipi alichohitaji. Kwamba anywe
bia yake hiyo iliyokwishafunguliwa.
Hakutaka
kumfanya Makella ahisi tofauti yoyote. Bado ilikuwa ni mapema hivyo Judith
alijali kuwa makini ili mambo yasiharibike. Alitaka afanye kila jambo kwa
uangalifu na umakini wa hali ya juu ili kisiharibike kitu. Akaitwaa chupa hiyo
na kuipeleka kinywani. Akameza funda moja
kwa jitihada kubwa. Mwili ukamsisimka lakini akajitahidi kutoukunja uso.
Akataka aonekane kuwa ni mtu aliyekwishakizoea kinywaji hicho.
Hakuwa
na kumbukumbu sahihi za maisha yake wakati akiwa mtoto mdogo. Lakini alikumbuka vizuri kuwa
tangu aanze kuwa na akili ya kutambua jema na baya, hadi usiku huu, hakuwahi
kupitisha tone la pombe kinywani mwake. Katika umri huu mkubwa aliokwishafikia,
aliwahi kusikia kuwa baadhi ya wazazi huwa na tabia ya kuwanywesha watoto wao
wachanga kijiko kimoja cha pombe kali kwa kile walichodai kuwa ni ‘kuua
michango.’
Hakuwa
na hakika kuwa na yeye alifanyiwa hivyo na wazazi wake. Hakujua na kwa usiku huu
asingeweza kujua na hakuwa na haja ya kujua. Alichojua hapo ni kwamba, kwa mara
ya kwanza anaipitisha pombe kinywani mwake na kuiruhusu iteremke tumboni mwake!
Mara ya kwanza kunywa pombe!
Funda
la kwanza lilipopenya kooni alihisi kanywa shubiri. Akajikaza kisabuni,
akainama kidogo na kwa sekunde chache akaukunja uso katika namna ambayo Makella
hakumwona na punde akaunyanyua na kumtazama sawia.
Hata
hivyo haikumwingia akilini Makella kuwa kinywaji hicho kilimsumbua Judith hata
kidogo. Aliamini hivyo na ndivyo akili yake ilivyomtuma kuamini kuwa kila
Mhutu, kila Mtutsi na yeyote wa kabila lolote nchini humo, pombe ni sehemu ya
maisha yake.
Hivyo,
yeye pia aliitwaa chupa yake ya bia na kunywa funda kadhaa kwa pupa kabla
hajaitua kwenye kijimeza.
Kisha
akaendelea, “Turudi kwenye hoja yetu. Cha kushangaza, wanawake wengi wa
Tanzania, wana tabia za ajabu. Utakuta mwanamke kaingia baa tangu saa sita
mchana na kuganda akinywa ile mimaji yao ya chupa! Shaa! Sijui wako-aje? Au
labda…” akasita na kukunja uso.
Akamtazama
Judith kwa macho makali. Kisha akasema, “Ndiyo, nina shaka huenda wengi wao
wako kwenye dozi kubwa.” Akacheka kicheko cha dhihaka.
Kicheko
hicho kilimshangaza Judith kiasi cha kumuuliza, “Dozi kubwa?! Una maana gani?”
Kwa
mara nyingine Makella alicheka. Kisha kwa sauti ya bezo akasema, “Wengi
wameshaukwaa…!” akacheka tena, safari hii kwa sauti ya chini zaidi. Akaongeza, “Hili gonjwa la Ukimwi
limeharibu mambo. Utakuta mwanamke mzuri…lakini kumbe yuko kwenye dozi ya zile
dawa ya kuongeza siku za kuishi. Mtu unakunywa kila siku mpaka siku yako ya
mwisho ya kuishi. Na zamani nasikia ilikuwa ukishaanza kunywa midawa ile, wewe
na bia basi! Yaani wewe na raha za dunia nd’o basi tena! Unakuwa mtu wa kula
sana na kuhakikisha kila siku unakunywa dawa hizo! Lakini siku hizi nasikia mtu
anaweza kuwa anapiga hizo dawa…wenyewe wanaziita ‘karanga’ na bia akanywa na
hata sigara anavuta!”
“Hee!”
Judith alishangaa, mkono kaziba mdomo, macho yamemtoka, akimtazama Makella.
“Basi
tuachane na mambo hayo,” Makella alisema huku akitwaa chupa yake na kugugumia
tena kinywaji chake.
Judith
hakutaka makuu. Naye alitwaa chupa na kuipeleka kinywani, akashusha kooni funda
dogo la kinywaji hicho kisha akamtazama Makella. Akamwona jinsi anavyojisikia
kuwa huru zaidi.
“Nadhani
nikaoge,” Makella alisema huku akiimaliza bia yake chupani.
Akasimama
na kuchojoa nguo zake. Papohapo harufu kali ya jasho ikajitokeza na kumfanya
Judith akunje uso kidogo na kwa siri.
“Sasa
hivi?” Judith aliilazimisha sauti yake. Kwa ujumla swali hilo lilimtoka tu wala
hakuwa amepanga kuhoji chochote, na ukweli ni kwamba hakuwa mtu wa kuzungumza
chochote na Makella.
“Ndiyo,
ni vizuri nikaoge sasa hivi. Pilikapilka za mchana kutwa zimenifanya nijisikie
ovyo na kunitia kichefuchefu. Nadhani nikioga nitajisikia fresh kiasi.
Nitakunywa bia kwa starehe na tutaongea kwa amani na utulivu, eti mpenzi?”
Itaendelea kesho...

No comments:
Post a Comment