Pages

Pages

Pages

Friday 6 June 2014

RIWAYA TAMU: JUDITH…JUDITH…! - 3


INNOCENT A. NDAYANSE (ZAGALLO)

0755 040 520 / 0653 593 546 


Mambo yameanza, chuki baina ya makabila mawili makubwa nchini Rwanda – Wahuti na Watutsi – imeshika kasi na mauaji yanaendelea. Lakini mapenzi nayo yanaingilia kati. Je, nini kitaendelea? Ungana na msimulizi wako…

Kumbukumbu hiyo ilimjia wakati yeye na wenzake wamebakiza mitaa mitatu tu kabla ya ule alikoishi Judith, huku hiyo mitaa waliyokwishaipitia wakiwa wameziacha maiti lukuki za Kitutsi, maiti ambazo Makella na wenzake walichekelea pale walipoua  kwa kutumia risasi, kunyonga kwa mikono yao hata kwa kuchoma visu.
Ilikuwa ni burudani kubwa kwao kushuhudia mtu akianguka chini na kukata roho kwa maumivu japo baadhi ya hao wanauawa  wakiomba waachwe hai, wakitumia sauti za kusihi na macho ya kubembeleza.
Makella na wenzake walifikia katika nyumba ya mzee Ndayishimiye saa 2 usiku, dhamira yao ikiwa ni ileile, kukifutilia mbali kizazi cha Kitutsi katika ardhi ya Rwanda. Wakiwa mbele ya nyumba ya mzee Ndayishimiye, walitulia, wakatazamana.
Dakika iliyofuata ndipo wakachukua hatua na kufanikiwa kuingia ndani ambako walijikuta kwenye varanda kubwa iliyosheheni sofa chakavu na mikeka. Eneo hilo lilitoa taswira ya kuwa ni sehemu isiyo rasmi kwa wageni, zaidi palitumiwa na watoto au hata watu wazima wa familia hiyo kwa kujipumzisha nyakati za mchana.
Mbele kulikuwa na mlango mwingine. Na huo pia haukuwa umefungwa lakini pazia nene lililojaa hapo liliwafanya Makella na wenzake wasiweze kuona ndani zaidi.
“Ni humo,” hatimaye aliwaambia wenzake huku akitangulia kuelekea huko ndani.
Kama awali, wenzake walimfuata.

********** 
MZEE Ndayishimiye na familia yake walikuwa ni Watutsi. Na zoezi la Makella na wenzake lililenga kuwateketeza Watutsi pekee! Lakini Makella na kundi hilo walipoifikia hii nyumba aliwahadharisha wenzake akiwaambia, “Humu kuna mwanamke wangu…ninataka kumwoa! Huyo msimguse!”
“Ni Mtutsi?!” mmoja wa watu waliomzunguka alimuuliza kwa mshangao.
“Ndiyo, ni Mtutsi!” Makella alijibu kwa msisitizo, lakini sauti yake ikiwa ya chini.
Kauli yake iliwafanya wenzake wote wamkodolee macho ya mshangao, wakionekana kutoamini wakisikiacho.
“Unataka kuoa Mtutsi?!” mwingine alimdaka.
“Hivyo hivyo!” Makella aliwaka. “Hata kama sitamuoa, lakini ni afadhali hata…” akaiacha sentensi hiyo ikielea.
Wenzake wakakosa nguvu ya kuendeleza maswali au udadisi. Muda haukuwaruhusu. Wote wakafuatana na kuingia kwa kishindo, bunduki zilizokamatwa na wawili zikiwa zimewatangulia.  Wenyeji wao walikuwa mezani wakipata mlo wa usiku. Ilikuwa ni sebule yenye mvuto, sebule ambayo kwa mgeni yeyote, wa hadhi yoyote lazima atajisikia burudani pindi atakapokaribishwa.
Kulisheheni samani aghali na zenye  kuvutia. Seti mbili za sofa zilikuwa zimeichukua robo tatu ya chumba hicho huku kabati kubwa la vyombo vya kauri na televisheni kubwa ya kisasa, iliyokuwa kwenye kijimeza chake maalumu vikiongeza ubora wa sebule hiyo. Pia kulikuwa na vijistuli kadhaa hapa na pale vilivyowekwa kwa mpangilio mzuri na kuzidi kukifaharisha chumba hicho.
Kule alikokaa mzee Ndayishimiye na familia yake kulikuwa na meza kubwa na viti maalum likiwa ni eneo maalum kwa maakuli. Kwa jumla ilikuwa ni sebule iliyostahili kuitwa ‘sebule bora.”
Makella na wenzake waliwakodolea macho yenye kila dalili ya kuua! Hawakuwa kama binadamu wa kawaida, simama yao na tazama yao ilitosha kuonyesha kuwa wako tayari kwa lolote na kwa yeyote

 “Ni yule pale! Msimguse!” Makella alisema kwa msisitizo huku akimnyooshea kidole mmoja wa wanafamilia hao, Judith.

Itaendelea kesho...

No comments:

Post a Comment