INNOCENT A.
NDAYANSE (ZAGALLO)
0755 040 520 /
0653 593 546
Kizungumkuti
kinaendelea baina ya Judith na Makella anayedai anampenda wakati tayari
amekwishaamuru familia ya Judith iuawe. Je, Judith atamjibu nini? Ungana na
msimulizi wako…
Akatupa
macho juu ya meza ndogo iliyokuwa katikati ya chumba hicho. Akauona ufunguo.
Akakumbuka kuwa muda mfupi baada ya yule mfanyakazi wa hoteli kuwafungulia mlango,
alimkabidhi ufunguo Makella. Kwa vyovyote
ndio utakuwa huu, alijiaminisha.
Hata
hivyo, aliwaza, hata kama ufunguo ndio huo, bado ilihitajika akili ya ziada
katika kumzidi ujanja Makella. Akili yake ikaendelea kumjengea imani kuwa ndani
ya jokofu lililo mbele yake kuna vinywaji na miongoni mwa vinywaji hivyo ni Primus, bia inayoaminika, kukubalika na
kuheshimika kwa Wanyarwanda na Warundi wengi.
Judith
aliomba Mungu kimoyomoyo, Makella awe mnywaji, anywe Primus na huo ndio utakuwa
mwanzo wa yeye, Judith kunusurika. Kwamba atajinusuru vipi, hilo hakutaka
kulifikiria wakati huo, lakini aliamini hivyo. Na aliamini kuwa Mungu yupo na
atakuwa upande wake!
Bado
mkono wa Makella ulikuwa katika ziara mwilini mwa Judith. Sasa ulikuwa umehama
pajani na kutua kifuani ambako ulianza
kuyatomasa matiti machanga, yenye joto la uhai, joto liwezalo kumsisimua
mwanamume yeyote mkamilifu.
Judith
akiwa ni mwanadamu kamili, mwenye viungo vilivyokamilika, kwa mbali alijikuta
akisisimkwa. Ndiyo, aliuhisi msisimko mwilini mwake lakini ukawa ni msisimko
ambao haukudumu zaidi ya sekunde kumi. Angepata raha gani, angeupataje msisimko
wakati familia yake yote imeteketezwa muda mfupi uliopita?
Kwa
ustaarabu aliushika mkono wa Makella na kuutoa kifuani pake taratibu huku
akiuminyamimya kiganjani katika namna iliyomchanganya zaidi Makella.
“Judi…Judi…”
Makella alinong’ona kwa taabu huku akimvuta Judith na kumbusu shavuni. Kisha
akataka kumbusu kinywani, tendo lililokumbana na kipingamizi kutoka kwa Judith
lakini kikiwa ni kipingamizi kilichowekwa kwa namna nyingine ya kistaarabu.
Alichofanya Judith ni kuukwepesha mdomo wake kwa namna ya kuona aibu huku
akiachia tabasamu laini na kuuinamisha uso.
“Judi…”
kwa mara nyingine Makella alinong’ona, safari hii akiwa kama anayeomboleza.
“Bwana
nimechoka!” sauti ya Judith ilikuwa ya deko.
“Umechoka?”
likamtoka Makella bila ya kutarajia.
Judith
akaitika kwa kutikisa kichwa, kisha akaongeza kwa sauti, “Halafu nasikia kiu!”
“Kiu!”
Makella aliropoka. Papohapo alinyanyuka na kulifuata jokofu. Akalifungua na
kuliacha wazi. Macho yakatua ndani na kushuhudia shehena ya vinywaji
mbalimbali; soda, maji, mvinyo, bia na pombe kali.
“Kinywaji
gani mrembo?” Makella alimuuliza Judith huku bado akiwa ameuach wazi mlango wa
jokofu labda ili na Judith pia avishuhudie vinywaji hivyo.
“Maji.”
“Maji?”
Makella alishangaa. “Kwa nini usinywe bia au wine?”
“Sijazoea.”
Makella
akacheka kidogo. “Ni vinywaji vizuri na bora kwa afya,” alisema huku akitoa
chupa mbili za bia. Akaongeza, “Jaribu. Ukizoea utaitaka kila siku. Kwa leo
ukinywa moja tu itatosha. Na utachangamka kimwili na kiakili. Sipendi uwe
katika lindi la mawazo mtoto mzuri kama wewe.”
Akaziweka
chupa hizo juu ya kimeza na kuzifungua. “Nikupatie glasi?”
“Hapana,
nitakunywa hivihivi,” Judith alijibu. Wakati huo alikuwa akiwaza jinsi
atakavyojisikia pale atakapolipenyeza funda la pombe kinywani mwake kwa mara ya
kwanza maishani mwake.
“Hapo
umeonyesha kuwa wewe ni binti wa kisasa,” Makella alisema huku akiachia
tabasamu kubwa. Akaongeza, “Ningeshangaa, binti mzuri wa Kitutsi asinywe bia!
Lingekuwa ni jambo la ajabu! Hapo kwa kweli nisingekuelewa. Wasichana wa
Kitanzania ndio wenye ushamba wa aina hiyo.
“Kule
Tanzania nilishakaa kwa mwezi mmoja na kitu. Nilikuwa Dar es Salaam. Tuache
uongo, Dar es Salaam ni mji mkubwa sana…mkubwa sana kuliko Kigali hata
Bujumbura! Ni jiji kubwa, jiji lenye
wakazi wengi sana, kama milioni tano au kumi!
“Ni
jiji lenye majumba mengi, mazuri na makubwa sana! Kwa sasa kila kukicha jiji
lile linabadilika. Kama ulikuwa kule miaka mitano iliyopita leo ukiingia
utapotea! Wallahi nakuapia! Kila siku linazidi kupendeza, na hayo majumba
yenyewe yanayojengwa acha tu…ni mazuri!
“Dar
es Salaam pia ni jiji lenye mambo mengi kama ambavyo lina wakazi wengi. Ni jiji
lenye maraha na karaha. Kuna baa nyingi na kumbi nyingi za starehe na pia kuna
bendi nyingi za dansi, taarabu na bongo fleva. Ukilinganisha na huku kwetu, ni
majirani zetu tu wa Burundi ambao miaka ya themanini walikuwa na vikundi vya
taarabu ambavyo kwa kweli vilitikisa sana katika Ukanda wa Maziwa Makuu.
Kulikuwa na vikundi vya Jasmine Musical Taarab na Shani Musical Taarab ambavyo
vilitisha!
“Lakini
siyo leo…! Leo Tanzania ina vikundi vya taarabu vinavyopiga huu mtindo mpya wa
morden…mmmh acha tu! Watu wanakata viuno kama wanamuziki wa Kikongo!
Hahahahahaha…” kicheko chake kikatisha badala ya kupendeza masikioni mwa
Judith.
Itaendelea kesho...

No comments:
Post a Comment