Pages

Pages

Pages

Saturday 3 May 2014

‘MICHEPUKO’ NI CHANZO CHA WENGI KWENDA KUPIMA DNA


Baadhi ya vipimo vinavyotumika katika kuchunguza vinasaba (DNA) kwenye maabara.Upimaji wa  DNA ulianza kutumika nchini niaka ya 2000. 

Isaya Kolumba  alishangazwa na tabia za mmoja wa watoto wake. Hakuwa na sura yake wala ya mama yake. Si hivyo tu bali alikwishaanza kuona dalili kubwa zinazoonyesha mtoto huyo kufanana kisura na dereva anayemuendesha mke wake.
Ili kuondoa utata na wasiwasi uliomgubika, Yakobo aliamua kwenda kupata ushauri wa daktari.
Daktari alimtia moyo na kumweleza kuwa, ukweli kamili waweza kupatikana baada ya vipimo vya vinasaba ama vinavyojulikana kitaalamu kama deoxy Ribonucleic Acid(DNA).
Baada ya serikali kutambua umuhimu wa kuanzishwa kwa sheria ya DNA itakayoitwa ‘The Human DNA Regulation Act 2008’ kikao cha Bunge  kiliwahi kujadili muswada wa sheria hiyo, ambayo serikali inadai itaweza kuondoa migongano ya hapa na pale ikiwa ni pamoja na uhalali wa mtu kumiliki mtoto.
 Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi ya Makosa ya Jinai na Vinasaba, kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu, Gloria Machuve anasema sababu kubwa ya watu kufanya vipimo vya DNA ni pale wanandoa wanapokuwa na wasiwasi katika mahusiano yao.
“Miongoni mwa kwa kesi nyingi, karibu asilimia 60 zinazoletwa ni za kujua uhalali wa baba kwa mtoto, kwa sababu kesi za jinai hazitegemei DNA pekee,” anasema Machuve
Anasema wanaume wengi zaidi hufika katika Ofisi hiyo kwa ajili ya  kupima DNA ukilinganisha na wanawake. Sababu kubwa inayotajwa ni kupata wasiwasi wa uhalali wa watoto wao.
Jambo kubwa linalotokea mara kwa mara katika vipimo hivyo ni pale wazazi, hasa wa kike wanapoamua kukimbia majibu au kuyakataa katakata.
Kwa mujibu wa rekodi za ofisi hiyo, wanawake ndiyo hukimbia zaidi ukilinganisha na wanaume.
“Lakini katika hili, ni vizuri wanandoa wakaepuka michepuko, kusimamia mienendo yao ndani ya nyumba. Wajiulize; je, mahusiano yao yapoje? Wajitathmini ndipo wafike kupima vipimo  hivi,” anasema Machuve
Takwimu za mwaka 2012 kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali zinaainisha kuwa kati ya watu 90 waliokwenda kupima DNA, 40 ambao ni sawa na asilimia 44, wameonekana kubambikiziwa watoto.
Takwimu hizo za kuanzia Januari hadi Oktoba mwaka huu, zilionyesha kuwa katika kesi 50 za waliokwenda kupima, matokeo yalionyesha kuwa ni wazazi halisi wa watoto wao.
Hata hivyo, idadi hiyo inayoonyesha kuwa kinababa siyo wazazi halisi wa watoto, imeshuka ikilinganishwa na takwimu za mwaka 2008/2009 ambazo zinaonyesha kuwa asilimia 60 ya watu waliochukua vipimo hivyo wamebainika kuwa si wazazi halisi.
Taratibu za upimaji

Machuve anasema ingawa wapo watu wanaoyakosoa majibu ya DNA na kusema kuwa wakati mwingine yanadanganya, lakini taratibu za uchunguzi na mitambo ndizo zinazotoa majibu.
“DNA ina majibu ya ukweli kwa asilimia 99.99. Wahusika wanapofika hapa ni kwamba wameamua, hivyo wanatakiwa kujua taratibu za upimaji, ikiwemo kutayarishwa na kupewa ushauri kabla ya kuanza vipimo,” anasema.
 Anasema sampuli za vipimo huweza kuwa mate, damu, majimaji ya ukeni, kucha, mizizi ya nywele na alama za vidole huchukuliwa.
Sampuli hizo huchukuliwa kulingana na aina ya shauri.
Shauri hilo huweza kuwa ni la kujua uhalali wa baba au mama kwa mtoto, makosa ya jinai, kama vile ubakaji, mauaji na wizi.
“Katika kesi za uhalali wa baba au mama, si lazima shauri lihusiane na michepuko pekee, bali huenda wanafamilia au mwanafamilia anataka kupata haki ya mirathi,” anasema.
 Hata  hivyo linapokuja suala la kujua uhalali wa baba kwa mtoto, basi mtoto hawezi kuambiwa moja moja matokeo ya majibu hasa inapobainika kuwa si mtoto halali.
“Mtoto haambiwi moja kwa moja kwa sababu matokeo ya vinasaba yanaweza kumuathiri kwa kiasi kikubwa kisaikolojia. Kwa kifupi, kipimo kinajali maisha ya mtoto,” anasema.
Uhalisia wa bei ni Sh800,000

Ingawa gharama anazochajiwa mtu anayetaka kupima kinasaba ni Sh300,000, lakini gharama halisi ambazo serikali inaingia katika upimaji ni Sh800,000
Machuve anasema kupima kila aina ya sampuli ni Sh100,000. Yaani mate, nywele, damu au majimaji ya mwili.
Gharama nyingine ni za kiuchunguzi, vitendanishi, kemikali zinazotumika, utaalamu, muda na mchakato wa uendeshaji wa mitambo.
“Lakini kwa sababu ofisi ya Mkemia Mkuu ipo chini ya Wizara ya Afya,  gharama hizi zimeshushwa hadi Sh300,000 ili kila Mtanzania aweze kuipata,” anasema
Upimaji wa jinsi tawala

Aidha, mkemia huyo alisema maabara hiyo inapima jinsi tawala ya mtu ambaye anazaliwa na kuonekana kuwa na maumbo yote mawili ya mwanamke na mwanamume.
 Alisema pia wapo watoto wanaozaliwa wakiwa na utata katika jinsia, kwa mfano ana sura ya kiume na sauti lakini ana sehemu ya siri ya kike.
“Watu kama hao wakifika hapa, tunaweza kuwapima ni jinsi ipi inatawala ili wapatiwe matibabu na kisha waitumie jinsi inayotawala. Wanaweza kufanyiwa upasuaji au kupewa vichocheo vya jinsia inayotawala,” alisema.
Mtaalamu wa afya ya jamii, na uzazi kwa vijana, Dk Ali Mzige anasema ingawa upimaji wa vinasaba ni jambo jipya nchini lakini wanajamii hawana budi kulielewa kwa undani.
“Ni suala jipya, limekuja miaka ya hivi karibuni na ndiyo maana itachukua muda au imechukua muda kwa watu wengi kulielewa,” anasema Dk Mzige
Hata hivyo, Dk Mzige anasema matokeo ya upimaji wa vinasaba kujua uhalali wa baba kwa mtoto, unaonyesha kuwa maadili yamepungua katika jamii.

Malalamiko ya wananchi juu ya kuibiwa au kubadilishiwa watoto, ndugu au jamaa kufungwa bila ya kuhusika katika mashitaka ya makosa yao kutapungua kwa kiasi kikubwa.

chanZo mwananchi

1 comment: