Pages

Pages

Pages

Friday 23 May 2014

GHARAMA ZA MAISHA KUBWA DODOMA: TUHOJI MATUMIZI YA WABUNGE WETU!


Ndugu zangu,
Bungu la Bajeti la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaendelea mjini Dodoma kwa mijadala ya bajeti za wizara mbalimbali.
Wakati Bunge hilo linaanza rasmi Mei 6, 2014, wiki mbili tu baada ya kuahirishwa kwa Bunge Maalum la Katiba, tuliambiwa kwamba vikao vya Bunge la Bajeti vinaanza huku waheshimiwa wetu wakilipwa posho mpya ya Shs. 300,000 kama ilivyokuwa wakati wa Bunge Maalum la Katiba.
Posho hiyo ni nyongeza ya asilimia 50 ya posho waliyokuwa wakilipwa awali, ambayo ilikuwa ni Shs. 200,000 zinazofafanuliwa kwamba Shs. 70,000 ni posho ya kikao, Shs. 80,000 posho ya kujikimuna Shs. 50,000 posho ya usafiri! Neema iliyoje hii, na waheshimiwa wengine wanaombea vikao hivyo viendelee mwaka mzima! Si wanavuna bwana!
Sababu kubwa ya nyongeza hiyo ya asilimia 50, ambayo italigharimu Bunge hilo kiasi cha Shs. 18.5 bilioni kwa siku 52 zilizotengwa kwa ajili ya Bunge la Bajeti linalotarajiwa kuhitimishwa Juni 27, ati ni kupanda kwa gharama za maisha mjini Dodoma!
Itakumbukwa kwamba, suala hili la kuongeza posho lilianza kupigiwa chapuo wakati Bunge la Katiba likielekea ukingoni, ambapo wabunge walihoji sababu za wajumbe kulipwa kiasi kikubwa cha fedha kwa kazi ile ile na katika mazingira yaleyale, wakati wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wakilipwa kiasi kidogo.
Kwa kuangalia mazingira halisi – iwe ya Bunge la Katiba au hili la Bajeti – kulipwa kiasi hicho kikubwa cha fedha kwa siku ni sehemu ya matumizi mabaya ya fedha za umma kwa sababu wabunge hao siyo wa kwanza kufanyia vikao vyao mjini Dodoma.
Nakumbuka wabunge waliwahi kupangishiwa nyumba katika Area D mwaka 1996 ili kupunguza gharama za kwenye nyumba za kulala wageni, lakini wengi walikataa kwa sababu ya ‘uhuru’ wao ulikuwa unaminywa. Nikakikumbuka kile kisa alichowahi kusimulia Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere cha Mbwa wa Manzese na Mbwa wa Masaki!
Najiuliza siku zote, kwamba ni kwa nini gharama hizi za maisha zinapanda katika vikao vya Bunge pekee! Bei ya lodge za Dodoma inafahamika vyema wakati wote, na haijawahi kupandishwa kwa msimu fulani na kushushwa msimu mwingine, iweje leo hii gharama zinapanda kwa waheshimiwa?
Tangu mwaka 1973 Serikali ilipotangaza Dodoma kuwa Makao Makuu ya nchi, hakuna hata mmoja aliyetekeleza agizo hilo la serikali kuhamishia shughuli zake huko licha ya jitihada kubwa za Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kuweka plani nzuri ya mji.
Kila mwaka tunasikia hadithi kwamba watahamia huko, lakini hakuna kinachotekelezwa. Hongera kwa wizara mbili tatu zilizothubutu kuhamia huko.
Wabunge hawa hawa wanaopigia kelele nyongeza ya mishahara ndio wako mstari wa mbele kuikosoa serikali kwa matumizi mabaya. Wengine wanasema mpaka mishipa ya shingo inawatoka huku mate yakiwatoka kama nyoka. Wanayofanya wao ni kinyume na wanayohubiri.
Hawa hawa wanaohubiri mabaya ya serikali waliwahi kulalamika ilipotolewa hoja ya kutopokea posho mbili mbili. Kwenye vikao vya kawaida na vinavyohusiana na yale wanayojadili.
Wananikumbusha mtu mmoja ninayemfahamu ambaye ni kinara wa kukosoa jamii akihubiri uadilifu, lakini nimemshuhudia yeye mwenyewe si mwadilifu hata kidogo na anaongoza kwa kuchukua posho mbili kwa safari moja! Hakika huu ni unafiki uliopitiliza.
Pengine ni wakati muafaka sasa wa kuwahoji wabunge wetu wanaosema posho haitoshi juu ya maumizi yao halisi.
Ndiyo. Tuwahoji, kwa sababu haiwezekani wakasema fedha haitoshi wakati fedha kama hiyo ama pungufu ya hiyo ndiyo anayelipwa mwalimu anaiyeishi Dodoma kwa mwezi mzima, tena mwenye familia na aliyepanga.
Hawa tuliowatuma watutee wanalilia fedha nyingi za posho wakati wakitambua kabisa Mtanzania wa kawaida kipato chake kwa siku hakizidi Dola 1 (yaani Shs. 1,600)! Badala ya kumtetea mwananchi wanatetea matumbo yao yanayozidi kufura.
Hawamkumbuki mkulima ambaye ameshindwa kupata pembejeo za ruzuku kwa sababu kule kijijini zimeletwa vocha 200 tu katika kijiji chenye watu 3,000! Wala hakuna anayejali kama mkulima huyo aliyepata shida anapata masoko ya mazao yake ama anakopwa. Zimebaki siasa na hadaa.
Nimesema hapo awali kwamba, wapo wabunge ambao wanaombea vikao vya Bunge vifanyike mwaka mzima. Waendelee kuvuna mapesa mengi kwa kugonga meza huku wakiitikia ule wimbo maarufu uliotafsiriwa na wananchi: “Wanafiki (ooo sorry – wanaoafiki) waseme ndiyoooo” Utawasikia “Ndiyooooo”!!
Wengine tumewashuhudia wakiwa wanasinzia mpaka udenda unawatoka wakati vikao vinaendelea. Wote hawa wanasema maisha magumu Dodoma, gharama zimepanda na kazi wanayoifanya ni kubwa. Naam, kazi ya kulala na kupigania tumbo!
Hakika, waunge wetu watuambie matumizi yao yanayofanya waone kwamba posho ya Shs. 200,000 kwa siku (mbali ya mshahara wao) iwe ndogo. Vinginevyo wananchi watawahukumu!

Ndugu yenu,
Daniel Mbega
Iringa, Tanzania
0656-331974

No comments:

Post a Comment