Dodoma. Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Jamhuri ya Hesabu za Serikali (PAC), Kabwe Zitto amependekeza kufanyika uchunguzi wa kiufundi ili kubaini sababu za kukatika kwa matangazo ya moja kwa moja ya kituo cha televisheni cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) wakati Bunge la Katiba likiendelea juzi.
Matangazo hayo yaliyokuwa yanarushwa na TBC1 wakati Tundu Lissu akiwasilisha maoni ya walio wachache katika Kamati Namba 4, yalikatishwa ghafla na kumlazimu mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta kuahirisha kikao hadi leo.
Wakati Zitto akipendekeza kufanyika kwa uchunguzi huo, Baraza la Habari Tanzania (MCT) limetaka kuwapo uthibitisho wa kitaalamu uliosababisha kukatika kwa matangazo hayo.
Hata hivyo, meneja matukio wa TBC, Mbwilo Kitujime alisema kwa ufupi kuwa hakukuwa na siasa katika suala hilo bali mitambo ilipata hitilafu, lakini akasema kwa ufafanuzi zaidi atafutwe mkurugenzi mkuu wa TBC, Clement Mshana. Mshana hakuweza kupatikana.
Kauli ya Zitto
Akizunguza na gazeti hili kwa simu kutoka nchini India jana, Zitto alisema sababu nyepesi tu kuwa “ni kutokana na hali ya hewa Dar es Salaam” hazikubaliki, hasa kutokana na mwenendo wa TBC.
“TBC inaendeshwa kwa fedha za walipa kodi. TBC ijue kuwa wao si shirika la utangazaji la serikali, bali ni Shirika la Umma. Ni matumizi mabaya ya fedha za umma kuegemea upande mmoja,” alisema.
Zitto, ambaye pia mbunge wa Kigoma Kaskazini na mjumbe wa Bunge hilo, alipendekeza shughuli za TBC kipindi hiki chote cha mjadala wa Katiba ziwekwe chini ya uangalizi wa chombo huru chenye wajumbe kutoka pande zote.
MCT yahoji mfumo
Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga alisema mfumo wa sasa wa uendeshaji wa shirika hilo la umma ni mbovu na una kasoro na ndio maana wadau wa habari walipendekeza mabadiliko makubwa katika shirika hilo.
“Kitu kilichotokea jana (juzi) kinathibitisha mambo ambayo tumekuwa tukidai kwamba tutoke kwenye kitu kinachoitwa utangazaji wa serikali twende kwenye utangazaji wa huduma za umma,” alisema.
Kwa mujibu wa Mukajanga, TBC inapaswa kujiendesha kama lilivyo Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), ambalo ni huru likiwa na kasma maalumu na linawajibika moja kwa moja kwa Bunge.
Mukajanga alisema nchi inapokuwa na chombo cha utangazaji cha serikali, watangazaji wanaathiriwa na matakwa ya serikali iliyopo madarakani na ndicho kinachoipata TBC kwa sasa.
Katibu mtendaji huyo alisema watumishi wa TBC hivi sasa wako katika wakati mgumu kupima ama kufanya kazi kwa weledi au kwa matakwa ya serikali baada ya kauli ya Rais Jakaya Kikwete.
“Rais kashasema hadharani anataka serikali mbili, wao (TBC) hawawezi tena kutumia taaluma yao tunayoifahamu ya kuwajibika kwa umma na kutopendelea,” alisisitiza Mukajanga.
Naye mwandishi wa habari wa siku nyingi,Lawrence Kilimwiko alisema hatashangaa kusikia kwamba kukatishwa kwa matangazo hayo kulikuwa ni maelekezo maalumu.
Kilichotokea
Hali hiyo ilitokea juzi baada ya mjumbe wa Bunge hilo, Freeman Mbowe kuomba mwongozo kuhusu TBC1 kusitisha matangazo wakati Lissu akiwasilisha, jambo lililomfanya Sitta kuamua kusitisha shughuli za Bunge.
Imeandikwa na Daniel Mjema, Elias Msuya
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment