Pages

Pages

Pages

Thursday, 17 April 2014

UKAWA WAIMBA: 'CCM INTERAHAMWE'



Dodoma. Nje ya Ukumbi wa Bunge, wajumbe hao kutoka Ukawa na baadhi ya wajumbe kutoka kundi la wajumbe 201 walioteuliwa na Rais, walitoka wakiimba “CCM Interahamwe”.
Pia walitumia falsafa maarufu ya Mchungaji Mtikila ya “Saa ya ukombozi ni sasa,” kuchagiza safari yao ya kutoka Ukumbi wa Bunge Maalumu la Katiba hadi Ukumbi wa Pius Msekwa uliopo eneo hilohilo la Bunge.
Wakiwa ndani ya ukumbi huo, wajumbe hao waliendelea kuimba nyimbo mbalimbali ikiwamo wimbo wa mshikamano (Solidarityforever) unaoimbwa na wafanyakazi kuonyesha mshikamano.
Pia waliimba: “Vijana msilale bado mapambano... Ukawa msilale bado mapambano.” Halikadhalika, wajumbe hao waliimba nyimbo mbalimbali za kumshutumu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi na baadhi ya nyimbo hizo zilisikika “Lukuvi mbaguzi” na “Lukuvi mchochezi.”
Interahamwe ni kikundi cha wanamgambo wa Kihutu wa Rwanda ambacho kilichochea mbegu za ukabila na kusababisha mauaji ya halaiki ya Rwanda dhidi ya Watutsi.
Wajumbe hao walitoka nje ya ukumbi huo wa Bunge la Katiba wakiongozwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa wa vyama vya siasa akiwamo Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF na Freeman Mbowe wa Chadema.
Viongozi wengine wa kitaifa ni Emmanuel Makaidi wa NLD, James Mbatia wa NCCR-Mageuzi na Mchungaji Christopher Mtikila wa DP na viongozi wa vyama vingine ambao majina yao hayakupatikana.
Ndani ya Ukumbi wa Msekwa, Profesa Lipumba aliwashukuru wajumbe wote waliowaunga mkono wakiwamo baadhi kutoka kundi la 201 na kueleza kuwa kauli ya Lukuvi ndiyo kiini cha mgogoro huo mpya wa kisiasa. Alivitaja vyama vingine vya upinzani vilivyowaunga mkono kuwa ni NRA, Chauma na UDP.
“Imebidi tutoke… kwa namna tulivyokuwa tunakwenda ilikuwa hamna tija yoyote na hatuwezi na sisi kuungana nao (CCM na makundi yaliyobaki) kufanya maasi dhidi ya Watanzania,” alisema.
Profesa alipendekeza wajumbe wote wakutane leo saa 4:00 asubuhi kwenye Ukumbi wa Hoteli ya AfricanDreams ili kujadili na kuweka msimamo wa mwelekeo wa baadaye wa umoja huo.
Profesa Lipumba alisema baada ya kikao cha leo, watakwenda mapumziko ya Pasaka na hawatahudhuria tena mkutano huo wa Bunge la Katiba hadi mwafaka wa kisiasa utakapopatikana.
Lukuvi
Akizungumza na gazeti hili jana, Lukuvi alisema: “Hao wanatafuta gia ya kuondokea kwenda kula Pasaka na wanafanya hivyo baada ya kukosa hoja za maana. Kumbukeni kwamba mwanzoni hoja ilikuwa ni hati ya Muungano, sasa baada ya kusikia imepatikana hawana tena jipya.”
Kuhusu tuhuma kwamba alifanya uchochezi wa kidini katika Kanisa la Methodisti mjini Dodoma, Lukuvi alisema si kweli kwani alichokisema ni kuonyesha jinsi mfumo wa serikali tatu unavyoweza kusababisha changamoto ya kibajeti kwa serikali ya shirikisho.
“Hiyo ni hofu yangu mimi kwamba lazima serikali ya shirikisho iwe na uwezo kifedha na mimi nilitoa mfano kwamba ikiwa nchi washirika zitakataa kutoa fedha, ina maana kwamba serikali hiyo haitaweza kujiendesha ikiwa ni pamoja na fedha za kuendesha taasisi kama jeshi,” alisema.
Alisema katika mazingira ya kukosa fedha, jeshi haliwezi kuvumilia na badala yake linaweza kutwaa madaraka ili kulazimisha upatikanaji wa fedha.
“Kwa hiyo maelezo yangu yalikuwa katika muktadha huo na wala siyo vinginevyo, halafu kama kweli hiyo ndiyo sababu, sasa mbona Rais (Kikwete) aliposema hawakutoka nje?” alihoji.
Askofu Mkuu
Askofu Mkuu wa Kanisa la Methodist, DkMathew Byamungu alipoulizwa jana ni nini hasa Lukuvi alichokizungumza kanisani, alisema suala la jeshi kuchukua nchi alilitolea kama mfano.
“Hajatamka kwamba serikali tatu zikiundwa jeshi litachukua nchi… alitolea mfano tu kuwa serikali zikiwa tatu mzigo wa kuziendesha utakuwa mkubwa na kushindwa kuzihudumia taasisi zake hasa Jeshi,” alisema.
“Akasema jeshi litakapokosa matumizi inawezekana kabisa kutokana na uzoefu linaweza kufanya vinginevyo lisiitii hiyo serikali, likajichukulia madaraka na huo ndiyo mfano alioutoa,” alisema.
Askofu Byamungu aliwasihi wajumbe wa Bunge hilo waliotoka nje jana kurejea kujadili Rasimu ya Katiba na kwamba matamshi ya Lukuvi yalikuwa ni mfano tu katika kuonyesha faida na hasara ya serikali tatu.
Habari zote zimeandikwa na Neville Meena, Daniel Mjema, Ibrahim Bakari, Sharon Sauwa, Beatrice Mosses na Habel Chidawali.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment