Pages

Pages

Pages

Wednesday, 16 April 2014

MWAMBUSI AGEUKA 'MBOGO'

Dar es Salaam. Kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi   amewashutumu watu waliomzushia kuwa amenunuliwa nyumba na klabu ya Azam FC, hali iliyofanya maisha yake kuwa hatarini kabla ya mchezo huo.
Kabla ya mechi kati ya Mbeya City na Azam mwishoni mwa wiki, kuliibuka maneno kwamba kocha huyp ameahidiwa kujengewa nyumba na klabu yake ikiahidiwa kununuliwa basi jipya.
Lakini Mwambusi amekanusha madai hayo na kuwataka watu wanaofanya hivyo kuachamara moja kwa kuwa wanahatarisha maisha yake.
“Hamna kitu kimeniuma kama hicho na  ukweli wachezaji wangu waliniokoa kwa mpira waliouonyesha siku hiyo ila mwamuzi ndio alitumaliza na kila mmoja aliona,” alisema kocha huyo.
“Lakini isingekuwa hivyo sijui ningetokea wapi maana mashabiki walishapanga kuja kunichomea nyumba na kunidhuru eti kwa madai nilishapanga matokeo. Mimi nawaomba sana watu waachane na mambo kama haya ya uzushi maana yanaweza yakasababisha maafa. Mtu huna uhakika unaanza kuzusha jambokubwa kama hilo. Fanyia utafiti na ukathibitisha ndipo uongee.
“Nawashukuru sana wachezaji wangu kwa soka walilolionyesha na liliwapa majibu wote waliohisi tutacheza mechi hiyo kizembe na kufungwa mabao rahisi na ndio maana hata baada ya mechi mashabiki walipoa na kuona kuwa mpira ulichezwa ila mwamuzi ndiye aliyetaka matokeo yawe vile.”
Mwambusi alisema katika maisha yake ya kufundisha soka hajawahi kupokea rushwa na hatapokea na ndio maana kila mara anawasisitiza wachezaji wake kuachana na mambo kama hayo.
“Nimefundisha soka miaka mingi na sina dhiki ya pesa kwani nina biashara zangu nyingi zinazoniingizia fedha. Sasa kwani nini nipokee rushwa eti niiachie timu fulani ishinde halafu niharibu heshima na utu wangu,” alisema Mwambusi.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment