Pages

Pages

Pages

Thursday, 10 April 2014

MAJARIBIO MANNE YA KUVUNJA MUUNGANO


Ismail Jussa Ladhu

Dodoma. Muundo wa Muungano ni kati ya sura za Rasimu ya Katiba ambazo zimezua mjadala mzito kwa wajumbe wa Bunge la Katiba, hasa baada ya kuwapo kwa mgawanyiko wa makundi yenye msimamo tofauti.
Kamati ya Uongozi ya Bunge hilo ilipanga Sura ya kwanza na ya Pili kuwa sura za awali ambazo zitajadiliwa na kamati 12 za bunge hilo, ikiwa ni hatua ya kwanza kabla ya kuingizwa katika mjadala wa Bunge zima.
Mjadala huo ni pamoja na kitendo cha Baraza la Wawakilishi kufanya marekebisho ya katiba yake mwaka 2010 yaliyohusisha kumpa mamlaka zaidi rais wa Serikali ya Mapinduzi na kutangaza visiwa hivyo kuwa nchi, uamuzi ambao umetafsiriwa kuwa ni uvunjaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Hata hivyo, Ismail Jussa anaona kuwa wanaodai matatizo ya Muungano yameanza 2010, wanapotosha.
“Mwaka wa mwanzo wa kuundwa kwa Muungano matatizo yalianza na mgogoro wa mwanzo ulikuja wakati wa utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje,” anasema.
Anasema wakati Zanzibar inaingia katika Muungano, Ujerumani Mashariki ilikuwa ikiitambua na pia Tanganyika ilikuwa ikitambuliwa na Ujerumani Magharibi.
Jussa, ambaye pia ni mwakilishi wa Mji Mkongwe, anasema Ujerumani Magharibi ilikuwa na sera yake kuwa nchi yoyote ambayo itaitambua Ujerumani Mashariki, haitakuwa na mahusiano nayo ya kibalozi.
Anasema baada ya Muungano, kulitokea mgogoro mkubwa baada ya Tanzania kuwa na ofisi mbili za ubalozi. Mgogoro huo uliamuliwa kwa kufungwa kwa ofisi ya ubalozi wa Ujerumani Mashariki.
“Palitokea ugomvi mkubwa kwa kuwa Zanzibar ilikataa kufunga ubalozi wake nchini Ujerumani Mashariki kwa sababu hao ni watu wao na wakati huo tayari walikuwa wameshaanza kuimiminia misaada,” anasema.
Anasema mgogoro huo ulitishia kuvunjika kwa Muungano mwaka 1964, baada ya msimamo huo wa Zanzibar.
“Matokeo yake baada ya mapambano makubwa kwa mara ya kwanza Ujerumani Magharibi, ikawabidi kuvunja historia yao kwa kuruhusu Zanzibar kuendelea kuwa na ofisi Ujerumani Mashariki,” anasema.
Jussa anasema pia mgogoro mkubwa wa sarafu ambao ulijitokeza mwaka 1965 uliohusu Benki Kuu.
Anasema kadhia kubwa ilijitokeza mwaka 1971. Wakati huo Hayati Karume hakuridhishwa na uendeshaji wa Baraza la Muungano na kumuagiza Waziri wa Nchi, Abdul Jumbe, kumwandikia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akimtaka mambo matano yaondoshwe katika orodha ya mambo ya Muungano, moja likiwa ni usawa kati ya pande mbili.
Jussa anataja mambo mengine kuwa ni polisi, uraia, sarafu na alilolitaka libaki lakini kuwe na usawa ni Mambo ya Nje.
Ushahidi mwingine wa kero ya Muungano, kwa mujibu wa Jussa, ni Septemba mwaka 1975 wakati Jumbe, akiwa rais wa Zanzibar alipomwagiza Waziri wa Nchi, Ally Hassan Moyo kumwandikia Waziri wa Fedha wakati huo, Cleopa Msuya.
Moyo alimweleza Msuya kuwa Zanzibar hairidhiki na Serikali ya Muungano kufanya mazungumzo ya Ushirikiano na Jumuiya za Mataifa na kuomba misaada bila kuishirikisha.
Anasema mwaka 1984 Mzee Jumbe alifukuzwa Zanzibar kutokana na kuchafuka kwa hali ya kisiasa kutokana na kudai serikali tatu. Anasema Makamu wa kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, alifukuzwa wakati huo kwa kudai serikali tatu .
Dk. Salimin Amour naye anatajwa kuwa kiongozi mwingine aliyeingia katika misukosuko kutokana na harakati hizo baada ya Zanzibar kutaka kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC), ambayo ilisababisha kuibuka kwa hoja ya G 55.
Kero za muungano
Aidha, Jussa anasema wakati Tanganyika ikiwa imekubali kufutwa kwa utaifa wake ma kutokuwa na uongozi, watu wasitegemee Zanzibar nayo itafutwa.
“Na ndio maana unaona tangu wakati ilipoungana na Tanganyika, Zanzibar imeendelea kutunga sheria zake na ikatekeleza na kuimarisha vyombo vyake,” anasema.
Anasema Hayati Karume aliendesha mambo yake kama vile Zanzibar haipo kwenye Muungano na kwamba Profesa Issa Shivji ameeleza vizuri katika kitabu chake cha Pan Africanism.
Anatoa mfano wa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa ambaye katika hotuba yake ya kwanza mara baada ya kuchaguliwa kushika nafasi hiyo aliahidi kumaliza matatizo hayo ndani ya siku 60.
“Kaondoka baada ya miaka kumi madarakani lakini hakuna alichopunguza,” anasema.
Katiba ya Zanzibar
Jussa anasema watu wanaodhani kuwa Zanzibar inaweza kubadili katiba yao, wasahau.
“Ibara ya 80A ya Katiba ya Zanzibar inataka kuwepo kwa theluthi mbili ya kura kwa Baraza la Wawakilishi ili kubadili Katiba hiyo, CCM hawawezi kuipata,” alisema.
Anasema kama wazo la kutaka kuibadilisha katiba ya Zanzibar kuwa si nchi litapelekwa, litakutana na vizingiti viwili kwa kukosa theluthi mbili za kura za wawakilishi na kukosa kura za kuungwa mkono na wananchi ambao kamwe hawawezi kukubali kubatilishwa kwa sheria hiyo.
“Ni muhimu tutakae pamoja tuzungumze hatma ya Muungano huu ambapo umefikia hapa lakini kudanganya kuwa kuna njia ya mkato ni kujidanganya,” anasema.
Theluthi mbili
Anasema kukosekana kwa theluthi mbili katika upigaji wa kura kwenye kamati, kunaashiria hali ngumu katika Bunge la Katiba kwenye kupitisha Rasimu ya Katiba.
“Inaashiria pia Wazanzibari hawako tayari katika kupitisha uchakachuaji wa CCM katika Rasimu ya Katiba, lakini jingine kuna misingi ya Katiba iliyowekwa kwa kutaka theluthi mbili ambayo imejengwa kwenye kupata uhalali zaidi kwa wananchi,” anasema.
Alipoulizwa kuhusu hoja ya baadhi ya wajumbe kutaka wingi wa kura utumike katika kupitisha uamuzi kwenye kamati, badala ya theluthi mbili, Jussa alisema haiwezekani Katiba ikapitishwa kwa wingi wa kura kwa sababu haijengi uhalali kwa wananchi.
Anasema theluthi mbili imewekwa katika Katiba nyingi duniani ili kuweka uhalali mpana na mkubwa.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment