Pages

Pages

Pages

Tuesday, 15 April 2014

JK, BASATA, MNYIKA WAMLILIA GURUMO

Marehemu Muhidin Gurumo
WAKATI mwili wa mwanamuziki nguli, Muhidin Maalim Gurumo, ukitatajiwa kusafirishwa leo kwenda Kijiji cha Masaki, Kisarawe, Pwani kwa mazishi, Rais Jakaya Kikwete, amemtumia salamu za rambirambi waziri mwenye dhamana na michezo kutokana na kifo hicho kilichotokea jijini Dar es Salaam juzi.
Taarifa kutoka Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, inaeleza kuwa, Rais Kikwete amesikitishwa na kuhuzunishwa na taarifa za kifo hicho, kwa kuwa alikuwa msanii aliyeweza kulitumikia taifa kwa kipindi kirefu.
“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa na taarifa za kifo cha Muhidini Maalim Gurumo, ambaye alikuwa mmoja wa wasanii wa muziki wa dansi nchini waliolitumikia taifa hili kwa bidii tangu miaka ya 1960, kupitia sanaa ya muziki katika bendi mbalimbali za muziki wa dansi, kuanzia Bendi ya Nuta Jazz, Mlimani Park Orchestra, Orchestra Safari Sound (OSS), na Msondo Ngoma ambayo ameitumikia hadi alipostaafu mwaka 2013,” alieleza Rais Kikwete katika taarifa yake.
Rais Kikwete alisema mchango wa marehemu Gurumo kwa taifa hili ni mkubwa na wa kuigwa kupitia kipaji alichojaaliwa na Mwenyezi Mungu, ambacho alikitumia kikamilifu kwa manufaa ya wananchi.
Alisema binafsi anaungana na familia ya marehemu kuomboleza msiba huo mkubwa, kwa kutambua kuwa msiba wao ni wa wote  na kuwaomba wanafamilia ya marehemu kuwa na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha kuomboleza msiba wa mpendwa wao, kwa kutambua kwamba, yote ni mapenzi yake Mola.
Aidha, Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), nalo limeelezea kupokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa msanii nguli wa tasnia ya muziki wa dansi nchini, Muhidin Maalim Gurumo ‘Kamanda’.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jijini Dar es Salaam jana na Kaimu Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza, Baraza limesikitishwa na taarifa za kifo hicho.
“Baraza limeshtushwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa ya kifo hiki cha Muhidin Maalim Gurumo, ambaye mchango wake katika muziki wa dansi ni mkubwa mno na unahitajika sana, pengo aliloliacha ni kubwa, kwani ubunifu wake bado unahitajika katika tasnia hii,” alisema Mngereza na kuongeza:
“Baraza linatoa pole kwa familia ya marehemu na wasanii wote nchini, aidha tunawatakia moyo wa subira katika wakati huu wa majonzi ya kuondokewa na mpendwa wetu.
“Mwenyezi Mungu aipumzishe mahala pema peponi roho ya marehemu. Baraza liko pamoja na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.”
Kwa upande wake, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alisema, amepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Mwanamuziki huyo mkongwe.
Alisema, amekwishawasiliana na Shirikisho la Wasanii kwa ajili ya kuwasilisha rambirambi zake na kutoa pole kwa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (Chamudata), kwa kupoteza mshauri na mkuu wake wa Idara ya Fedha.
“Aidha natoa wito kwa wananchi wa Ubungo na Jiji la Dar es Salaam kwa ujumla, kushiriki katika kumuaga kesho (leo), nyumbani kwake Mabibo External katika Kata ya Makuburi kabla ya kwenda kuzikwa kwao Kisarawe Kijiji cha Masaki. Kwa kuwa niko katika Bunge la Katiba, nitawakilishwa katika kutoa heshima za mwisho na Diwani wa Kata ya Makuburi alipoishi marehemu,” alisema Mnyika na kuongeza.
Nichukue fursa hii kutoa pole kwa mashabiki wenzangu wa nyimbo zake kuanzia akiwa Kilimanjaro, Chacha, Rufiji Jazz, Kilwa Jazz, Sikinde na Msondo Ngoma kuanzia wakati wa Nuta, Juwata mpaka Ottu.
Naye Mkurugenzi wa Bendi ya Double M Sound, Muumin Mwinjuma, ameelezea kusikitishwa na msiba huo mzito, kwa kuwa ni mwanamuziki aliyekuwa mahiri na mkongwe aliyekuwa amebakia katika tasnia hiyo.
Alisema licha ya kuwa ni wa bendi ya Msondo Ngoma, lakini wamekuwa wakipata mwongozo na mawazo pia.
“Kwa kweli ni msanii mkongwe tunayemtegemea na binafsi nilikuwa nachota mawazo kutoka kwake, hivyo ni pigo kubwa, wameondoka wanamuziki wengi wakongwe na huyu ni kati ya wakongwe, ambaye pengo lake kwa kweli halitazibika,” alisema Mwinjuma.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bendi ya Extra Bongo, Ally Choki alisema, kwa kweli ni pigo, mbele yake nyuma yetu.
“Tulikuwa tunamtegemea katika tasnia yetu na kwa upande wangu, namkumbuka kwa mengi kwa kuwa tulifanya albamu naye, alikuwa na ushirikiano mzuri katika maonyesho yetu, ni kitu ambacho tunamkumbuka maana alikuwa ni mtu ambaye anajituma katika kazi yake,” alisema Choki.
Akizungumza na Tanzania Daima jana kuhusu taratibu za mazishi, mjukuu wa marehemu, Ramadhan Shabani, alisema kikao cha familia kilifanyika juzi na kwamba, wamepanga kusafirisha maiti leo majira ya saa nne asubuhi kwa ajili ya mazishi kijijini kwake Masaki, Pwani.
“Tutaondoka nyumbani kwake hapa Ubungo Kibangu kesho (leo), saa nne mara tu baada ya kusalia maiti na tukifika Masaki, pia tutasalia tena mwili wa marehemu na ndipo tunampumzisha babu yetu huko huko kijijini kwake Masaki,” alisema Shabani.
CHANZO: TANZANIADAIMA

No comments:

Post a Comment