Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, akionyesha Hati ya Muungano kwa wanahabari
SIKU moja baada ya serikali kuonyesha hati ya makubaliano ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar, wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, wamegawanyika juu ya uwepo wake.
Wakizungumza ndani na nje ya ukumbi wa Bunge mjini hapa, baadhi ya wajumbe wametilia shaka hati hizo kwa madai kuwa zitakuwa zimeghushiwa kwa lengo la kuwapumbaza Watanzania.
Mwenyekiti wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Freeman Mbowe, alisema hakuna kitu kisichowezekana kwa Watanzania ambao hivi sasa wamefikia hatua ya kughushi fedha za ndani na nje ya nchi.
Alisema watu wanaweza kughushi saini za Baba wa Taifa hayati Julius Nyerere na hayati Abeid Aman Karume, waliokubaliana kuziunganisha nchi walizokuwa wakiziongoza.
Mbowe alisema swali kubwa ambalo Watanzania wanapaswa kujiuliza ni kwanini katika kipindi chote ilichokuwa ikiuliziwa hati hiyo haikuwahi kutolewa wala kuelezwa ilipokuwa.
Alisema hawana uhakika wa hati hiyo hadi watakapoiona na pia watataka taasisi za kimataifa zichunguze uhalisia wake ili isije ikawa imeghushiwa.
“Hati inaweza kuwepo, lakini wanayoidai ipo imeridhiwa na pande zote mbili kwani inayodaiwa kuwepo ni ile iliyoridhiwa na Bunge la Tanganyika, lakini Baraza la Wawakilishi halikuridhia.
“Hati iwepo isiwepo muungano ni muhimu ila ujengwe katika misingi ya kweli, uwazi na haki. Kama kuna makosa yaliyotendeka nyuma tusiyabebe kwa ghiliba, ni ujinga kudhani hati ya muungano iliyotafutwa kwa miaka 50 iliyopita itatuelekeza kwa kwenda katika mchakato huu.
“Cha msingi ni kuhoji dhamira zetu, ni mkataba tu ambao haukuridhiwa na pande zote mbili, msingi wa muungano usiwe mchanga ambao si ridhaa ya pande zote mbili, tuepushe lawama mbele ila tushirikiane. UKAWA tunaona kuna haja ya kushirikiana, tunahitaji muungano ila turidhiane aina ya muungano tunaouhitaji,” alisema.
Julius Mtatiro, alisema anataka kuiona hiyo hati kwakuwa amesikia kuonekana kwake kupitia kwenye vyombo vya habari, lakini anashangaa kitu cha wazi kwa nchi nyingine kwa Tanzania iwe siri.
“Tuna shida ya uhalali wake, tukiona tutapeleka kwa wataalamu tulionao ambao watasema imetengenezwa lini.
Charles Mwijage, alisema hati haikuwa hoja ya msingi bali baadhi ya watu walikuwa wakitafuta kitu cha kukwamisha na kuumaliza muungano uliodumu kwa muda usiopungua miaka 50.
“Hati imeshapatikana, tufunge mjadala huu, watu waliapa kwa Bunge la Muungano sasa ni muungano upi walioapa wakati wana shaka na muungano husika?” alihoji.
Shamim Khan, alisema kuwa wale wote waliokuwa wakisema hati ya makubaliano haipo wameumbuka baada ya Ikulu kuonyesha hati halisi.
Alisema kuwa waliokuwa wakipinga hati hiyo wanapaswa kuonyeshwa na kama wakiipinga wapewe fursa ya kuonyesha mbadala wanayoijua wao.
“Tuwaonyeshe hati halali, wakiikataa basi watuambie hiyo halali iko wapi? Wasijenge hoja za chuki na uchochezi,” alisema.
Jesca Msambatavangu, alisema waliokuwa wakitaka kuonyeshwa hati ya muungano hawakuwa na nia njema bali walikuwa na dhamira ya kuuvunja muungano.
“Ukiona mke wako uliyeishi naye kwa miaka mingi ameanza kukuhoji hati ya ndoa, ujue amepata mwanamume mwingine mzuri zaidi au ana dhamira ya kwenda mahakamani kutaka kuivunja ndoa,” alisema.
Asupmta Mshama, alisema alikuwa akiamini kuwa hati ya makubaliano ya muungano ipo kwakuwa hata katika jumuiya za kimataifa Tanzania inajulikana ni muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
“Haiwezekani tukaungana bila ya kuwa na hati ya makubaliano, wale waliokuwa wakisema hati haipo, jana Ikulu imeonyesha, sasa si ajabu wakaja na hoja za kutaka hati ya muungano za visiwa vya Unguja na Pemba,” alisema.
Moses Machali, alisema hati za makubaliano zina shaka kubwa kwakuwa wajumbe waliziomba kwa siku nyingi, lakini hazikuwekwa wazi hali inayoashiria zilizopatikana ni za kughushi.
“Leo teknolojia imeendelea sana, hiyo hati itakuwa imeghushiwa maana kwa muda mrefu tuliiomba, lakini hatukupatiwa, sasa hii leo Ikulu imetoa wapi? Mimi najua zitakuwa zimeghushiwa,” alisema.
Mwinyi Haji Makame, alisema hatua ya kudai hati hizo ni dalili za wajumbe kuishiwa hoja, na hivi sasa watazusha jingine baada ya Ikulu kuzitoa hati halisi.
“Kuna watu wanataka kuvunja muungano ndiyo maana kila kukicha wanataka serikali za mkataba, serikali tatu au hati za muungano, tuwaangalie sana watu hawa,” alisema.
Majadiliano ya hati za muungano kwa muda wa wiki mbili sasa yaliteka mijadala ya Bunge ambapo baadhi ya wajumbe walikuwa wakidai hazipo, hivyo kugomea kujadili sura ya kwanza na sita za rasimu ya katiba.
Mvutano huo ulichagizwa zaidi baada ya serikali kutoa hati za kisheria za kuonyesha kuridhia muungano zilizokuwa na sahihi za hayati Nyerere na Karume zilizodaiwa kutofautiana, hivyo kuzusha hofu ya kughushiwa na kutokuwapo kwa hati halisi za muungano.
CHANZO: TANZANIADAIMA
No comments:
Post a Comment