Pages

Pages

Pages

Saturday 26 April 2014

CCM INAVYOMKUMBATIA ‘MWANA PEKEE’ WA MWALIMU NYERERE


Na Daniel Mbega

KAMA kuna kitu ambacho Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikipigania kwa nguvu zote mpaka anaingia kaburini ni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar (Muungano wa Tanzania) ambao leo umetimiza miaka 50 tangu kusainiwa kwa nyaraka zake.
Katika miaka ya mwisho ya uhai wake hili lilionekana dhahiri ambapo alilifanya kwa vitendo, si maneno peke yake. Hatua ya kwanza ilikuwa ile ya mwaka 1994 alipozima hoja ya Mbunge wa Chunya, Njelu Kasaka, ya kudai serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano.
Hakuishia hapo, akatoa kitabu cha ‘Uongozi wetu na hatma ya Tanzania’ kilichochapishwa nchini Zimbabwe mwaka 1994 ambapo pamoja na maneno makali aliyotumia, pia alitumia tenzi kuwananga wale waliokuwa wakiupinga ama kuubeza Muungano na kutishia mustakabali wake.
Mwaka uliofuata wakati wa uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi alifikia mahali akasimama kidete, akisaidiana na wanachama wengine wa CCM (pengine waliopata nguvu kuona Nyerere yupo nyuma yao), wakazima jaribio la rais wa Zanzibar wa wakati ule Dk. Salmin Amour Juma aliyetaka kuifanyia marekebisho Katiba ya Serikali ya Mapinduzi ili apate nafasi nyingine ya kugombea urais kwa mara ya tatu ifikapo mwaka 2000.
Wakati wa uchaguzi mkuu wa CCM wa mwaka 1997 Mwalimu alilazimika kwenda mwenyewe Chimwaga, Dodoma ingawa hakuwa amealikwa, na kwenda kuzima majaribio kadhaa yaliyokuwa yameandaliwa na ‘vijana’ wa chama hicho kutaka kumng’oa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, John Samuel Malecela, na badala yake wakapanga wamchague Waziri Mkuu wa wakati huo, Fredrick Sumaye. Akafanikiwa.
Mambo haya yote yalimuudhi na kumkera sana Mwalimu kwa sababu aliamini, japokuwa hakuwa kwenye wadhifa wowote – si wa chama au serikali – kwamba kama asingesimama kidete ustawi wa Muungano, ambao ulikuwa umeanza kutishiwa tena kama ilivyokuwa miaka ile ya 1980.
Ndiyo. Kisa cha kujiuzulu kwa Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi katika nyadhifa za Makamu wa Kwanza wa Rais wa Muungano, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mwaka 1984, kulitokana na hoja za Muungano, ambazo mwaka huu – miaka 30 baadaye – tumeshuhudia zikiwalazimu wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanaojiita UKAWA wakisusia vikao hivyo kwa maelezo kwamba CCM ‘imepora rasimu’ kwa maslahi yake.
Binafsi naona hoja za Jumbe zilikuwa sahihi kabisa kama ilivyokuwa kwa hoja ya Njelu Kasaka na wafuasi wake wa G55, ingawa nao baadaye walibadilika kama kinyonga hasa baada ya kupewa vyeo mbalimbali serikalini. Mpaka leo hii si mtoa hoja au mtu yeyote wa kundi hilo aliye tayari kuitaja tena hoja ya serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano.
Lakini pamoja na kujiuzulu kwa Jumbe, hoja zile bado ziko fikrani mwa Wazanzibari mpaka kesho, kwani itakumbukwa wakati wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 1990 uliomweka madarakani Dk. Salmin Amour Juma, Wazanzibari walikuwa wamepanga kuitisha maandamano na kugomea uchaguzi huo kwa maelezo kwamba Zanzibar inakandamizwa na Bara na wananchi wa visiwa hivyo hawapati baadhi ya haki zao za msingi zilizomezwa ndani ya Muungano.
Ingawa tatizo hili limekuwa likitajwa kwamba linatokana na historia ya visiwa hivyo; Unguja na Pemba, lakini bado linagonganisha vichwa vya wengi, hata wale Wazanzibari wa Unguja ‘wenye nafasi’. Unguja ndiko kwenye maendeleo zaidi kuliko Pemba, ambako ndiko karafuu inakozalishwa kwa wingi. Wananchi wa Pemba ni maskini sana kiasi kwamba huwezi kuamini kama ni sehemu ya Tanzania ukiwalinganisha na wenzao wa Unguja.
Waunguja hawazungumzii kasoro za Muungano kwa kisingizio cha kulinda maslahi ya Chama cha Mapinduzi kwa sababu wengi wao ni wafuasi wa CCM na kule Pemba asilimia 99 ni wafuasi wa chama pinzani cha CUF. Kwa hiyo wanadhani kwamba wakiupinga Muungano na kasoro zake watawapa nguvu wapinzani, fikra ambazo kwa namna moja ama nyingine ni potofu.
Zanzibar, tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, hakuko shwari kwa sababu Dk. Salmin anaelezwa kwamba hakushinda kwa haki na CUF walikwenda mpaka kwenye jumuiya za kimataifa kupiga kelele kwamba waliibiwa kura zao. Hata uchaguzi wa mwaka 2000 na ule wa mwaka 2005, bado kilio cha CUF kimeendelea kuwa kile kile.
Katika uchaguzi wa mwaka 1995, kwa mfano, uchaguzi ulirudiwa Zanzibar, na inasemekana kwamba viongozi kadhaa wa CCM na wanasiasa wakongwe walikwenda usiku Unguja na kurejea alfajiri Dar es Salaam katika kile kilichoelezwa na wachunguzi wa mambo ya siasa kwamba ‘kuunusuru Muungano’.
Baadhi wanasema kwamba ikiwa CUF itaruhusiwa na wananchi kutawala Visiwani, basi utakuwa ndio mwisho wa Muungano, ambao Mwalimu alipiga kelele na kusema asingekubali kuona Muungano unakufa wakati yeye akiwa hai.
Alikuwa sahihi kabisa. Kwa sababu kitendo cha kushuhudia ‘mtoto wake mpendwa’ Azimio la Arusha aliyezaa Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea ‘anauawa’ rasmi mwaka 1991 kwa Azimio la Zanzibar, hakika asingekuwa tayari kuona ‘mwanawe wa pekee’ ambaye ni Muungano anakufa yeye akitazama.
Siri ya Muungano huu wanaoijua ni Nyerere na Karume tu, wote wanaosema wanaijua wanajaribu ‘kukonyeza gizani’. Yaani wanakisia na si kile kitokacho moyoni.
Leo hii CCM imeendelea kusimama kidete kuhakikisha kwamba ‘mwana pekee’ wa Mwalimu hakati roho kama baadhi wanavyoombea.
Pengine inahofia kwamba kukubali mapendekezo ya kamati ya mwafaka, ambayo ni kuwa na serikali ya mseto, kutakuwa ni hatari kama kupika mchele uliichanganyika na chuya! Ni jambo linaloonekana kuwa gumu kama kupanda mlima Kilimanjaro ukikimbia.
CCM yenyewe inajitetea kwamba hoja ya Muungano wa Tanzania inasimama juu ya msingi wa sera ya chama hicho, ambayo inaelezwa kwamba ina ncha mbili; yaani kuulinda na kuudumisha Muungano wenyewe kwa upande mmoja na muundo wa Muungano huo kuwa wa Serikali mbili kwa upande wa pili.
CCM inaushabikia Muungano na kupania kuulinda na kuudumisha kwa sababu kwanza inaamini kuwa Muungano huo ni wa watu wenyewe na pili, uliasisiwa na vyama wazazi wake, yaani TANU na ASP.  Binafsi sijui kama Muungano ulikuwa wa watu wenyewe, kwa sababu hakuna mtu aliyepata nafasi ya kuuridhia wakati huo kabla ya kufikia hatua ya kusaini nyaraka za Muungano, ambazo mpaka leo hii hazipo na hazijulikani zilipo.
Ni kweli kwamba CCM yenyewe ni matokeo ya Muungano huo na chachu ya kuziimarisha kwani tendo la kuviunganisha vyama vya TANU na ASP kuunda CCM lilitokana na utashi wa kukamilisha hatua za kuunda Muungano. Daima CCM inaunga mkono muundo wa Muungano wa Serikali mbili kwa sababu kwanza ndio ulioamuliwa na waasisi wa Muungano, Mwalimu Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.
Japokuwa CCM inajinasibu kwamba muundo wa serikali mbili umeridhiwa na Watanzania wengi, binafsi nasema siyo sahihi hata kidogo. Kwa kuchukua vigezo vya mwaka 1994 walivyofanya kukusanya maoni kwa wanachama, lazima mtu yeyote anaweza kuhisi kwamba matokeo yaliyotangazwa yalikuwa ni kwa maslahi ya chama na wale wanaoushabikia Muungano na si maslahi ya Watanzania walio wengi.
Lakini kama kweli Muungano huu unapaswa kuwa na mtazamo halisi wa utashi wa wananchi wote, kuna mambo mengi ya kufanya ili kufikia hatua hiyo ambayo haiwezi kuwa kero tena; iwe Muungano unakuwepo au unavunjika.
Kwanza; Watanzania wengi wangependa kuziona nyaraka za kwanza kabisa za Muungano ambazo zilisainiwa bila kuwepo kwa ridhaa ya wananchi wa pande zote mbili za Muungano.
Pili; serikali ya CCM inapaswa kutambua kwamba suala la Muungano siyo la chama peke yake, bali ni la Katiba ya Nchi na wananchi kwa ujumla. Chama kinaweza kutawala kwa kipindi fulani, na kama hoja za kuundwa kwake zinainufaisha zaidi CCM, lazima itambue kwamba ipo siku hata yenyewe itakuwa pembeni kama ilivyotokea kwa ZAPU, KANU na vinginevyo. Suluhisho pekee lilikuwa katika kuhakikisha kwamba mjadala katika Bunge Maalum la Katiba unaendeshwa kwa haki na siyo ngonjera, mipasho na matusi ambayo tumeyashuhudia kwa baadhi ya wajumbe. Wajumbe wengi, hasa kutoka CCM, wamekuwa ‘mabingwa’ wa kutukana na kuwakashfu wale wote wanaounga mkono mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba.
Tatu; wananchi wa pande zote wanapaswa kutoa maoni yao katika harakati za kuifanyia marekebisho Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ili watoe mapendekezo yao na muundo bora wanaodhani unafaa kama serikali moja, mbili au tatu badala ya kuegemea kwenye kura za kichama ambazo waliopiga ni wana CCM, waliohesabu ni wanaCCM wenyewe na CCM ndio waliokuwa wakipinga serikali moja na tatu.
Nne; kero za Muungano zinatakiwa kutatuliwa kiutendaji badala ya kisiasa kwa sababu hali hiyo ndiyo inayosababisha migongano na mwishowe hata wapinzani wanaonekana kama wakorofi wakati siyo sahihi.
Kwa kuyafanyia kazi haya, ambayo ndani yake yamebeba hoja nyingi za msingi, kuna uwezekano wa kuona mwelekezo sahihi wa Muungano huu ambao leo umetimiza miaka 50.
Tofauti na hapo, CCM itakuwa haitendi haki kumlinda ‘mwana pekee’ wa Mwalimu Nyerere hata kama habebeki. Itafikia mahali juhudi zao zitakuwa kama kuitundikia dripu maiti, hatua ambayo itawafanya wachekwe na mataifa mengine.


MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU IBARIKI AFRIKA!

0656 331974

No comments:

Post a Comment