Pages

Pages

Pages

Tuesday, 15 April 2014

'CCM HAINA NIA YA KUTUNGA KATIBA YA WANANCHI'

Hebron Mwakagenda
MRATIBU wa Mtandao wa kufuatilia madeni ya Serikali (CDD), Hebron Mwakagenda, amewashambulia wabunge na baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuwa wanakusudia kutunga Katiba ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) badala ya kutunga katiba ya wananchi.
Pia amesema wabunge na wajumbe hao ambao wana mlengo wa CCM ndio watakaosababisha kuwepo kwa machafuko kutokana na kupuuza mawazo ya wananchi ambayo yapo katika rasimu ya pili ya katiba.
Mratibu huyo alitoa shutuma hizo muda mfupi baada kumalizika kwa semina ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaopinga vitendo vya rushwa.
Mwakagenda alisema dalili za kupatikana kwa katiba ya CCM ambayo inalinda masilahi ya viongozi wa chama hicho na kukosa mawazo ya wananchi zimeshaanza kuonekana kutokana na misimamo ya chama na kutumia wingi wao kupinga mawazo ya wananchi na walio wachache.
Alisema kelele za wajumbe wanaotokana na chama tawala zimekuwa na malengo makubwa ya kuwalazimisha wajumbe wengine wakubaliane na mawazo yao bila hata ya kuangalia kwamba wanakwenda kinyume cha mawazo ya wananchi ambao walitoa maoni yao wakati wa kukusanya maoni.
Akiendelea kutoa ufafanuzi juu ya mfumo wa kura ambao ndio unaofanya maamuzi ya kuipata Katiba, alisema mfumo huo uliandaliwa ili kuwafanya wengi washinde hata kama mawazo yao ni dhaifu.
Mbali na hilo, amekosoa hotuba ya Rais Jakaya Kikwete wakati wa kuzindua Bunge la Katiba kwamba haikulenga kuonyesha mwelekeo mzuri, badala yake kiongozi  huyo alijikita zaidi kutoa hotuba ya msimamo wa chama chake na kuonyesha ushabiki wa serikali mbili.
“Tatizo lao wanajivunia wingi wao ndani ambao sio shida kwa kuwa waliutengeneza na haukuingia kwa bahati mbaya, kwa hiyo hatuna katiba bali tusubiri neema ya Mungu kwa wakati mwingine,” alisema Mwakagenda.
Mratibu huyo aliwataka Watanzania kukesha kwa kuombea nchi,  ili Mungu aendelee kunusuru balaa ambazo zinaweza kujitokeza kutokana na CCM kuonyesha msimamo wao wa kupinga mawazo ya wananchi.
CHANZO: TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment