Pages

Pages

Pages

Sunday 5 January 2014

JWTZ LAMKINGIA KIFUA ASKARI WAKE ALIYEUA

JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limesema kitendo kilichofanywa na Ofisa wa jeshi hilo, Meja Abdallah Mzee, cha kuwapiga risasi vijana wanne hakikuwa cha makusudi. Kauli hiyo ilitolewa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano (JWTZ), Meja Joseph Masanja, katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari, ambapo alisema Mzee alijikuta akifyatua risasi hizo wakati akijaribu kujihami.

Masanja alisema ofisa huyo mwenye cheo cha meja, alikua akirejea nyumbani kwake Pugu Dar es Salaam akiwa ametokea katika Hospitali ya Amana na gari aina ya RAV4 ndipo alipozingirwa na kuvamiwa na watu hao aliodhani kuwa ni vibaka.
“Alikuwa akirejea nyumbani kwake usiku katika mida ya saa sita, lakini eneo ya Kinyamwezi kitendo kisicho cha kawaida alishangaa kuona watu wakimzunguka, huku waliomlazimisha kufungua milango ya gari lake.
“Katika hali hiyo meja Mzee aliamua kujihami kwa kutumia bastola yake aliyokua akiimiliki kihalali, ambapo alifyatua risasi juu akihofia kudhuriwa na kupokonya gari lake,” alisema Masanja.
Aidha katika tukio hilo, ofisa huyo aliweza kujinasua na kuondoka katika eneo hilo na kuamini watu hao wametawanyika.
Masanja alisema hata hivyo baada ya tukio hilo, inasadikiwa kuwa watu wawili walipoteza maisha na wengine wawili kujeruhiwa.
Waliofariki dunia katika tukio hilo ni Ibrahim Mohamed (16) na Abuubakar Hassan (14) wote ni wakazi wa Pugu Kinyamwenzi, ambao miili yao ilihifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Na waliojeruhiwa ni pamoja na Rupano Wanga (17) mkazi wa Pugu Makangani, pamoja na Kasim Abdul (16), ambaye ni mwanafunzi wa Sekondari ya Pugu na walipelekwa katika Hospitali ya Amana kwa ajili ya kupata matibabu.


CHANZO: Mtanzania

No comments:

Post a Comment