Pages

Pages

Pages

Friday 3 January 2014

HARUNA MASEBU AONDOKA EWURA

Haruna Masebu

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Haruna Masebu, amewaaga rasmi Watanzania na wanahabari baada ya kutumikia mamlaka hiyo kwa miaka minane.

Masebu alitumia nafasi hiyo alipokutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa mwaka jana.
Alisema kwa kipindi alichokuwepo EWURA, mamlaka hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika sekta ya mafuta, umeme na maji kwa kufanya mageuzi makubwa ambayo yaligusa sekta binafsi.
Alisema mageuzi hayo yalishirikisha wadau na kufuata sheria za mamlaka hiyo.
“Kwa mfano sekta ya mafuta ilikuwa na matatizo makubwa, kwa kutoa mafuta duni, kwa vipimo vidogo na bei wanayoitaka. Kulikuwa na vipingamizi vikubwa kwa kuwa watu wa sekta hii wana nguvu, lakini tulifanikiwa kuweka mageuzi,” alisema Masebu.
Kwa upande wa sekta ya maji, alisema inazidi kuboreka na kutolea mfano wa mikoa ya Arusha, Moshi na Tanga kuwa wanapata maji ya viwango.
“Tumedhihirisha kuwa mfumo huu umeweza kufanya mageuzi vizuri. Ninajivunia kuwa ninaacha taasisi yenye weledi na uzalendo wa hali ya juu. Inawezekana kila sekta ikiwa na weledi na kuwa na mabadiliko. Hivi sasa Tanzania inaweza kuigwa na nchi nyingine kwa EWURA,” alisema.
Alisema ingawa anastaafu lakini bado ana nguvu ya kulitumikia taifa, ila sheria za EWURA haziruhusu kutumikia zaidi ya miaka minane.

CHANZO: TanzaniaDaima

No comments:

Post a Comment