Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Thursday, 5 December 2013

SAFARI YA KWENDA SERENGETI INAANZA ASUBUHI HII...

 Sehemu nyingine hutakiwi kuuliza.

 Karibu tena utembelee.
 Muongoza watalii katika hifadhi ya Manyara, Elizabeth Msanya, akitoa maelezo kwa wanahabari (hawaonekani).
 Baadhi ya mifupo ya wanyama ikiwa imewekwa katika mojawapo ya maeneo ya hifadhi hiyo ya Manyara. Hapo kuna fuvu la Twiga, mguu wa Tembo, taya la Tembo na kadhalika.
 Watalii kutoka Marekani nao walikuwepo kuangalia utajiri tulionao kwenye Hifadhi ya Ziwa Manyara.
Twiga ni miongoni mwa wanyama wanaopatikana kwa wingi kwenye hifadhi hii.

Jana Jumatano tulichelewa sana kuondoka jijini Arusha kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara. Tuliwasili pale majira ya saa 10 hivi jioni, lakini hilo halikutuzuia kutembelea baadhi ya maeneo muhimu ya hifadhi hiyo.
Tukajifunza mengi tukielezwa na muongoza watalii Elizabeth Msanya. 
Kwa ujumla, hifadhi hiyo imejaa utajiri mkubwa wa rasilimali za asili, wakiwemo wanyama, ndege na mimea.
Hifadhi ya Ziwa Manyara iko katika mikoa ya Arusha na Manyara ikiwa chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).
Eneo kubwa la hifadhi hii ni ukanda mwembamba kati ya ukuta wa Bonde la Gregory na Ziwa Manyara, ziwa magadi (kama lilivyokuwa linafahamika zamani), ambalo liko upande wa mashariki mwa hifadhi.
Hifadhi hii ina ukubwa wa eneo la kilometa za mraba 330 za ardhi tambarare isiyo na miti, msitu, pamoja na ziwa magadi lenyewe ambalo linachukua takribani kilometa za mraba 200 za ardhi wakati wa msimu wa masika lakini ambalo linaonekana halipo wakati wa kiangazi.
Jana tuliwakuta ndege wengi aina ya korongo waliojazana ziwani humo, ambao ni miongoni mwa sifa kubwa za hifadhi hiyo. Tumeambiwa kwamba wakati wa masika hujazana zaidi kwenye kingo za ziwa hilo maelfu kwa maelfu lakini idadi yao hupungua wakati wa kiangazi.
Kuna aina 400 za ndege kwenye hifadhi hii na wengi wanapatikana katika majira yote ya mwaka. Wale wanaopenda kutazama ndege, basi watambue kwamba Hifadhi ya Ziwa Manyara ndiyo mahali pake ambapo wanaweza kuona zaidi ya aina 100 za ndege kwa siku yoyote ya mwaka.
Wanyama kama chui, simba, tembo, nyani wa bluu, digidigi, swala-pala, voboko, twiga na wengineo wanapatikana hapa kwa wingi. Jana tuliwakuta nyumbu wengi wakiwa wanajitafutia malisho. Kuna eneo moja ambalo lipo bwawa la viboko kwenye upande mmoja wa hifadhi ambako watalii wanapenda sana kutembelea.
Japokuwa simba ni jamii ya paka ambao kwa asili hupenda kukwea miti, lakini ni katika hifadhi hii pekee ambako unaweza kuwakuta simba na chui wakiwa juu ya miti wanapokuwa hawahitaji mawindo.
Hifadhi ya Ziwa Manyara iko umbali wa kilometa 126 kusini magharibi mwa jiji la Arusha na inafikika kwa kutumia magari kwa mwendo wa saa moja na nusu. Pia hifadhi hii inaweza kufikiwa kwa urahisi kupitia Babati. Iko jirani mno na Hifadhi ya Taifa ya Tarangire. Pia kuna uwanja mdogo wa ndege ulioko juu ya ukuta wa bonde la ufa.
Hakika, kuona ni kuamini. Nashauri kwamba, ikiwa Watanzania tutajenga utamaduni wa kutembelea vivutio vyetu vya utalii siyo tu kwamba tutajifunza mengi, bali tutawaambukiza hata watoto wetu hamu ya kutembelea vivutio hivyo badala ya kuona kama vipo kwa ajili ya wazungu.
Asubuhi hii tunajiandaa kwa safari ya kwenda Serengeti. Tutaendelea kuhabarishana.

Daniel Mbega.



No comments:

Post a Comment